Na Hafsa Golo
SERIKALI imesema kuwa, kukosekana wadhamini kwa ajili ya timu ya taifa ya soka 'Zanzibar Heroes', kunasababishwa na timu hiyo kutokuwa na mashindano mengi inayoshiriki kimataifa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, alipokuwa akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Nassor Salim Ali, aliyetaka kujua sababu zinazofanya timu hiyo kukosa udhamini.
Alifahamisha kuwa, kampuni zinapokubali kudhamini shughuli za michezo au timu, huhitaji kupata mrejesho kwa kutangazwa kupitia udhamini huo, jambo ambalo ili lifanyike, ni lazima timu inayodhaminiwa iwe inashiriki mashindano ya mara kwa mara.
Bihindi amesema timu ya taifa ya Zanzibar, huwa inashiriki mashindano ya Chalenji tu yanayofanyika kila mwaka kwa kushirikisha timu za ncbi za Afrika Mashariki, ambapo kama inafanikiwa kufika fainali, hucheza si zaidi ya mechi sita.
"Kutokana na hali hiyo, kampuni nyingi huona hasara kutumia mamilioni ya fedha kudhamini timu ambayo itavaa jezi zake na kuitangaza kampuni katika michezo sita tu kwa mwaka", alieleza Naibu Waziri huyo.
Mashindano mengine alisema, ni ya Kombe la Dunia ya VIVA, linaloshindaniwa na nchi ambazo si wanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) yanayofanyika kila mwaka, ambayo Zanzibar imeshiriki kwa mara ya kwanza mwaka huu na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu nchini Kurdistan Kaskazini mwa Irak.
Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikifanya juhudi kuzishawishi kampuni mbalimbali ili zikubali kuibeba timu ya taifa, lakini bado jitihada hizo hazijazaa matunda.
Katika kubuni njia za kukabiliana na kasoro hiyo, alisema wizara yake itashirikiana na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), kuandaa utaratibu maalumu wa kuitafutia timu hiyo mechi mbalimbali za kirafiki za kimataifa, ili kuipa uzoefu na kuwajengea imani wafadhili ili waweze kujitokeza kuidhamini.
No comments:
Post a Comment