Na Mwandishi
Wetu, Dar es Salaam
TIMU ya taifa ya soka Tanzania ya vijana wenye
umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes inashuka katika uwanja wa Taifa
kuivaa Nigeria, Flying Eagles, ikiwa mechi ya kwanza ya raundi ya pili kutafuta
tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa vijana zitakazofanyika mwakani nchini
Algeria.
Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jacob
Michelsen na nahodha wake Omega Seme, wamesema timu yao iko tayari kwa mechi
hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Kenya.
Michelsen amesema timu yake imepata mechi mbili
za kujipima nguvu dhidi ya Rwanda, lakini pia aliishuhudia Flying Eagles
ikicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) uliofanyika Julai 24 mwaka
huu jijini Kigali.
Amesema wachezaji Frank Domayo, Simon Msuva na Ramadhan
Singano ambao pia wanachezea timu A (Taifa Stars), wanatarajiwa kusaidia kwani
uzoefu wao ni muhimu kwa mechi hiyo.
Naye Kocha Mkuu wa Flying Eagles ambao ni
mabingwa watetezi wa michuano hiyo, John Obuh amesema haijui vizuri Ngorongoro
Heroes lakini anaiheshimu kutokana na ukweli kuwa inacheza raundi ya pili baada
ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.
No comments:
Post a Comment