SERIKALI ya Zanzibar imesema haina mpango wa kuweka trekta maalum kwa ajili ya Wananchi wa kijiji cha muyuni pekee bali matrekta yatayokuja yatatumika kwa kusambazwa Zanzibar nzima.
Waziri wa Kilimo na Maliasili, Suleiman Othman Nyanga, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, aliyetaka kujua kama serikali itaweka trekta kwa ajili ya wananchi wa kijiji hicho kutokana katika msimu uliopita wa kilimo kuonekana kufanya vizuri.
Waziri huyo, alisema hivi sasa serikali imeamua kununua matrekta mapya lakini yatasambazwa kwa nchi nzima na sio kijiji kimoja kutokana na idadi ya mahitaji ni makubwa.
Alisema matrekta hayo nayatarajiwa kuingia nchini wakati wowote na itahakikisha baada ya kuyasambaza itawalimia wananchi wa kwanza waliokosa huduma hiyo katika msimu uliopita.
Akijibu suala la Mwakilikishi wa Wawanawake Mwanajuma Faki Mdachi, aliyetaka kujua serikali itawasaidia vipi wakulima waliokosa huduma ya kulimiwa Waziri huyo alisema ni wakulima kidogo ambao bado hawakuweza kupata huduma hiyo.
Alisema fedha za wakulima hao Wizara hiyo imeziweka katika akaunti maalum ya wizara hiyo na tayari imewaagiza maafisa kilimo wa Wilaya kuorodhesha idadi yao ili kuweza kufanyiwa kazi hiyo baada kuanza msimu wa kilimo ujao.
No comments:
Post a Comment