Habari za Punde

Serikali yazidisha juhudi zake kutafuta usafiri wa uhakika


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wakala wa uuzaji wa Meli Kimataifa Bwana Rubin Rajan hapo nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam. Kati kati ni Mfanyabiashara maarufu Nchini ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini Mh. Kassim Dewji.

Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Ernesto Gomez Pias akimfariji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa asilimia 20% ya mkopo wa ununuzi wa Meli kubwa itakayokidhi mahitaji ya kusafirisha Abiria na Mizigo kwa uhakika na salama kati ya Visiwa vya Zanzibar na Mwambao wa Tanzania. 

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Wakala wa mradi wa Paul Plan unaosimamia uuzaji na ukopeshaji wa Meli kubwa za Abiria na Mizigo pamoja na Boti za uokozi Bwana Rupin Rajan hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam. 


 Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachokiangalia kwa hivi sasa ni kupata Usafiri wa uhakika utakaoondosha tatizo la usafiri wa kubahatisha kwa wananchi kati ya maeneo hayo muhimu. 

 Alisema licha ya Serikali kukabiliwa na uhaba wa fedha za ununuzi wa jumla lakini alimuomba wakala huyo kuhakikisha anatayarisha mapendekezo yake ya namna atakavyokuwa tayari kukidhi mahitaji ya Zanzibar ya kupata Meli kwa njia ya mkopo. 

Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar ina Historia ndefu ya kuwa na Meli zake kubwa za Serikali kabla na Baada ya Mapinduzi ambazo zilikuwa zikihudumia Visiwa vya Zanzibar sambamba na mwambao wa Tanzania. “ Huu mpango hata sasa hivi tungekuwa na uwezo wa kifedha tungeurejesha kwa nia ya kuwahudumia Wananchi wetu bila ya matatizo”. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliongeza kwamba fursa kwa Taasisi na Makampuni ya Uwekezaji ipo lakini kinachozingatiwa zaidi na Serikali ni kwa Muwekezaji kupelekea kabla mchanganuo wake Serikalini wa aina ya Chombo anachotaka kuagiza kwa ajili ya uhakiki wa Kitaalamu. 

Mapema Wakala huyo wa Mradi wa Paul Plan Bwana Rubin Rajan alimueleza Balozi Seif kwamba Taasisi yake ina uwezo wa kuuza kwa jumla ya mkopo vyombo ya usafiri wa abiria na mizigo katika nchi mbali mbali Duniani. 

Alisema Taasisi hiyo imejipangia mipango ya kuuza vyombo vyao kwa njia ya mkopo unaochukuwa takriban miaka 15 sambamba na boti za uokozi wakati yanayotokea maafa. 

Bwana Rubin alisema Taasisi hiyo kwa kutumia wataalamu wake pia imekuwa na utaratibu wa kumtengenezea chombo cha Usafiri kama meli au boti mteja wake kwa mujibu wa anavyohitaji kulingana na mazingira ya bandari pamoja na kina cha maji ambacho chombo hicho kitatoa huduma zake. 

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Gonzale ambae alifika nyumbani kwake Namanga kwa ajili ya kumpa pole kufuatia ajali ya Meliya M.V Skagit iliyotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya Watu kadhaa. 

Katika mazungumzo yao Balozi Seif ameipongeza Jamuhuri ya Cuba kwa hatua zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kwenye harakati zake za kiuchumi na ustawi wa Jamii. Balozi Seif alisema ushahidi wa hayo ameuona wakati wa ziara yake Nchini Cuba hivi karibuni ambapo nchi hiyo imeonyesha nia ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa katika sekta ya Afya. 

Alisema ukarimu wa Watu wa Cuba kupitia Balozi wa Nchi hiyo hapa Tanzania umeongeza chachu ya ushirikiano sambamba na kuleta matumaini hasa katika ile miradi inayoungwa mkono na Nchi hiyo rafiki. “ 

Wataalamu na Madaktari wa Cuba waliopo Nchini wanaendelea kutoa huduma vyema kwa Wananchi walio wengi Nchini”. Alifafanua Balozi Seif. 

 Naye Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Ernesto GHomez Pias alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Cuba itaendelea kudumisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili. Bwana Gonzale alisema hatua hiyo inathibitisha Madaktari 10 wa Tanzania wawili kati ya hao kutoka Zanzibar wanaendelea kupatiwa mafunzo ya juu Nchini Cuba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.