Na Khamis Malik
MWAKILISHI wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) Dorothy Rozga, amesema Tanzania ni nchi mojawapo ambayo ni mshirika mwenye kuaminika katika mezani ya Jumuia za Kimataifa.
Mwakilishi huyo wa UNICEF, aliyemaliza muda wake, aliyasema hayo wakati akiagana na Uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana,Wanawake na Watoto katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Shangani mjini hapa.
Dorothy alisema Tanzania inajitahidi kufanikisha masuala mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kumlinda, kumuhifadhi mtoto pamoja na hifadhi ya Jamii ambapo tayari kumekuwepo na sheria ya mtoto Tanzania bara na Zanzibar.
“Nimefurahishwa na nimefarajika sana kufanya kazi nchini Tanzania na nitamueleza mtu ambae atachukua nafasi yangu kuendeleza juhudi hizo hatua kwa hatua kwa masilahi ya watoto na Jamii kwa Jumla” alieleza Dorothy.
Dorothy pia aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuendelea kuyafanyia kazi matokeo ya utafiti juu ya udhalilishaji wa watoto ili kuweza kumuhifadhi na kumlinda mtoto ipasavyo.
Mapema akitoa shukrani kwa Mwakilishi huyo wa UNICEF, Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Zainab Omar Mohammed, alisema mashirikiano mazuri na misaada inayotolewa na UNICEF kwa Serikali inahakikisha kuimarishwa kwa haki na ustawi wa watoto nchini.
Waziri Zainab alisema wakati wa kipindi cha uongozi wa Dorothy kwa misaada yake kwa Serikali wameweza kuanzisha kitengo cha Hifadhi ya Mtoto, kitengo cha mkono kwa mkono, kuandaa sheria ya mtoto Nambari. 6 ya mwaka 2011 ili kupiga vita vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia nchini.
Alisema Wizara iko katika hatua za kuandaa sera ya Hifadhi ya jamii ambapo UNICEF itasaidia sera hiyo na kufanyakazi ipasavyo.
Zainab alimzawadia Dorothy mlango wenye nakshi za Kizanzibari ikiwa ni hatua ya kudumisha upendo na urafiki kwa Dorothy na UNICEF kwa jumla.
No comments:
Post a Comment