Na Ameir Khalid
IKIONESHA kukerwa na hatua ya timu ya Yanga kuleta wachezaji wa kikosi cha pili kwenye michuano ya Kombe la Urafiki Tanzania, kamati ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) inayosimamia mashindano hayo, imeamua kuitimua timu hiyo.
Kamati hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wa Yanga, ilikutana jana kujadili kadhia hiyo, na kufikia uamuzi wa kuifuta Yanga kwenye mashindano hayo, na hivyo kulibakisha kundi A na timu tatu pekee, Jamhuri, Zanzibar All Stars na Super Falcon.
Katika mchezo wake wa kwanza uliochezwa juzi usiku, mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, walikubali kichapo cha magoli 3-2 mbele ya Jamhuri, hali iliyozusha malalamiko kutoka kwa mashabiki, kuwa timu hiyo imeleta wachezaji watoto na hivyo kuipunguzia michuano hiyo ladha iliyotarajiwa.
Gazeti hili, jana alasiri lilishuhudia wachezaji na viongozi wa timu hiyo wakipanda boti ya Kilimanjaro 111 kuelekea Dar es Salaam na kuiacha michuano hiyo na timu saba.
Ofisa Habari wa ZFA Munir Zakaria, ambaye alikuwepo bandarini kuwashindikiza wachezaji hao, alikaririwa akisema klabu hiyo imekiuka makubaliano ya awali, ambapo ilikubali kuleta kikosi kitakachocheza michuano ya Kagame iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwezi huu.
“Tulikubaliana kwamba Simba, Azam na Yanga zilete timu kubwa zitakazocheza Kombe la Kagame ili kuyapa haiba mashindano yetu, na hivyo kuvutia mashabiki wengi, kinyume chake Yanga wameamua kutuletea makinda na kuondoa mvuto wa michuano”, alieleza Zakaria.
Aidha alisema kamati hiyo imeilipa Yanga posho zake, na kuongeza kuwa hatua hiyo itakuwa fundisho kwa klabu nyengine zinazoitwa kubwa, kuheshimu makubaliano yanayofikiwa badala ya kufanya zipendavyo.
Hata hivyo, viongozi wa Yanga waliofuatana na timu hiyo, walikataa katakata kuzungumza na gazeti hili, walipotakiwa kuelezea sababu za kuleta wachezaji wadogo na hatua ya kutimuliwa kwao.
Zakaria amesema pamoja na mabadiliko hayo, mechi ya leo usiku kati ya Super Falcon na Jamhuri, inabaki kama ilivyo, ingawa hadi tunakwenda mitamboni, kamati ya mashindano hayo ilikuwa ikikutana kuangalia namna nyengine ya kupanga ratiba.
ZFA itautumia mchezo huo kuizawadia Super Falcon kikombe cha ubingwa wa ligi kuu ya Zanzibar msimu uliomalizika hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment