Habari za Punde

Arejeshwa rumande baada ya kukosa mdhamini

 Haji Nassor na Asha Abdallah, ZJMMC Pemba
MAHAKAMA ya Wilaya ya Chake chake chini Hakimu Omar Hamza Mcha imemrudisha tena rumande mtuhumiwa Said Rajab Hamad, baada ya kukosa mdhamini dhidi ya shauri linalomkabili la kuiba chupa mbili za chai na sahani kubwa 18.
Akisomewa shtaka lake na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Gongo Shaaban Gongo alidai kuwa, Julai 11 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni huko Makungungeni kwenye Skuli, mtuhumiwa huyo aliiba vyombo hivyo mali Skuli hiyo.
Alidai kuwa vyombo hivyo vinathamani ya shilingi 75, 000/= kwa kukisia ambapo kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Awali Mwendesha Mashitaka huyo aliiambia mahakama hiyo, yupo shahidi ambae ni mwalimu wa Skuli hiyo na Hakimu Mcha kuomba aitwe ili kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Shahidi wa shauri hilo Rashid Mohamed Mtumweni (45) mkaazi wa Machomanne Chake chake alidai kuwa, mara baada ya kufunga skuli mwezi wa sita mwaka huu na walipofunga wiki mbili baadae,waligundua vyombo hivyo havimo kwenye bweni la wanawake.
Alidai kuwa mara baada ya kuona hivyo waliripoti kituo cha Polisi cha Chake chake na baadae wakaitwa kwa ajili ya kuvitambua vyombo hivyo, ambapo walikuta chupa mbili kubwa yenye rangi warid na ndogo nyenye rangi ya maji bahari.
 
Aidha shahidi huyo alidai kuwa baada ya muda walipata taarifa kuwa vyombo hivyo alikamatwa navyo mtu mmoja aliedai kuwa ameuziwa na mtuhumiwa huyo Said Rajabu Hamad na ndipo kutiwa mkononi na Polisi na kupandishwa mahakamani.
 
Mara baada ya shahidi huyo kukamilisha ushahidi wake mbele ya Hakimu wa Mahakam hiyo Omar Hamza Mcha, Mwendesha Mashitaka Gongo Shaaban Gongo aliomba mahakama hiyo kumuonyesha shahidi vitu hivyo na pindi ikiwa anaweza kuvitambua.

Mtuhumiwa huyo mara baada ya shahidi kumaliza kutoa ushahidi wake na kuvitambua vitu hivyo, Hakimu akamuuliza mtuhumiwa iwapo ana suali lolote la kumuuliza shahidi na alijibu hana suali , ambapo Hakimu huyo alisema dhamana yake iko wazi.

Shauri hilo limeghairishwa hadi Septemba 4 mwaka huu litakaposikilizwa tena na mtuhumiwa amerejeshwa rumande baada ya kukosa wadhamini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.