HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI
SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA NANE WA BARAZA LA NANE LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR TAREHE 10 AGOSTI, 2012
Makamu wa Rais wa Pili Balozi Seif Ali Iddi
1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima, afya njema na kutujaalia amani na utulivu katika Taifa letu. Naomba pia nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa busara zako za kuweza kuliendesha Baraza lako Tukufu kwa umakini na mafanikio makubwa. Pia nawashukuru na kuwapongeza Naibu Spika na Wenyeviti wote kwa namna wanavyokusaidiaMheshimiwa Spika katika kuliongoza Baraza hili. Vile vile, nawashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati mbali mbali za kudumu kwa kazi zao nzuri wanazozifanya katika kufuatilia utekelezaji wa Taasisi mbali mbali za Serikali na kufanikisha mkutano huu.
2. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa Nane wa Baraza la nane umekuwa wa kihistoria katika nchi yetu kutokana na mashirikiano makubwa ya Viongozi na Wajumbe wa Baraza na Watendaji wa Taasisi za Serikali. Nawashukuru wote na naomba tuendelee na mashirikiano haya mazuri.
3. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais wetu mpendwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake wa busara, hekima na unaozingatia maslahi ya wananchi. Ni dhahiri kuwa bidii za Rais Shein zinaendelea kuzaa matunda ya maendeleo katika sekta za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
4. Mheshimiwa Spika, vile vile niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri kwa kuwasilisha bajeti zao vizuri na kuweza kujibu hoja mbali mbali zilizojitokeza kwa umahiri na uelewa mkubwa.
5. Mheshimiwa Spika, napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Wawakilishi wenzangu wa Baraza lako Tukufu kwa kujadili, kudadisi na hatimae kupitisha bajeti za mapato na matumizi ya Wizara zetu. Naelewa kwamba hoja zao mbali mbali walizoziibua zilikuwa na mwelekeo mzuri na nia njema ya kuisaidia Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hii imeonesha namna ambavyo Wajumbe wako walivyofahamu mafunzo mbali mbali uliyowapa. Hata wananchi wetu ambao wametutuma kuja kuwawakilisha wanafurahishwa na jinsi Wajumbe wanavyochangia na kuibua hoja mbali mbali za msingi zenye nia ya kuiletea tija nchi yetu.
6. Mheshimiwa Spika, nampongeza kwa dhati rafiki yangu Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani, Mheshimiwa Rashid Seif Suleiman kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano na namtakia mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu yake ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuiongoza sekta hii muhimu ya Miundombinu na Mawasiliano. Pia nachukua nafasi hii kumpongeza aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad ambae ni Mwakilishi wa Jimbo la Ole kwa ujasiri wake aliyouonesha wa kuwajibika kisiasa kufuatia ajali ya meli ya M.V Skagit. Yeye hakuhusika moja kwa moja na ajali hiyo, lakini ameona ni vyema kuwajibika kisiasa.
7. Mheshimiwa Spika, natoa pongezi zangu za dhati kwa Mhe. Marina Joel Thomas kwa kuteuliwa kwake kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Nachukua fursa hii kumkaribisha Mheshimiwa Marina katika kujumuika na Waheshimiwa Wajumbe wenzake katika kuchangia maendeleo ya Taifa letu. Kuteuliwa kwake huko kunaonesha imani kubwa ambayo Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anayo juu yake.
8. Mheshimiwa Spika, napenda pia nimshukuru Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ndugu Yahya Khamis Hamad pamoja na watendaji wake wote kwa juhudi kubwa wanazozichukua katika kutekeleza majukumu yao, juhudi ambazo zimepelekea kufanikiwa kwa mkutano huu wa Nane wa Baraza hili. Aidha, napenda kumpongeza Katibu wetu wa zamani, Ndugu Ibrahim Mzee Ibrahim kwa kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Namtakia kila la kheri na mafanikio mema katika kazi yake hiyo mpya yenye changamoto nyingi.
9. Mheshimiwa Spika, vile vile nachukua nafasi hii kuvishukuru vyombo vya habari vyote hasa Shirika la Habari la Zanzibar kupitia redio na TV ambavyo vilirusha moja kwa moja maendeleo na shughuli za Baraza na kuwezesha wananchi wetu kufuatilia kwa makini hoja, michango na mijadala iliyokuwa ikiendelea Barazani hapa. Aidha, nachukua fursa hii kuwashukuru wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi zao nzuri walizozifanya kutafsiri mijadala kwa ishara ili wananchi wetu wenye ulemavu wa kutokusikia, nao waweze kufuatilia mijadala yetu.
10. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niwashukuru wananchi kwa kuonesha shauku ya kufuatilia mijadala na michango mbali mbali iliyokuwa ikiendelea katika Baraza hili. Hii inaonesha jinsi wananchi walivyohamasika katika kuitumia haki yao ya kupata habari mbali mbali na taarifa za Serikali.
11. Mheshimiwa Spika, Baraza hili la Bajeti kwa mwaka 2012/2013 limefanyika bila ya kuwa na wenzetu wawili Mheshimiwa Mussa Khamis Silima (aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini) na Mheshimiwa Salum Amour Mtondoo (aliyekuwa Mwakilishi wa Bububu) ambao wametangulia mbele ya haki. Tutaendelea kuwakumbuka kwa michango yao mikubwa waliyoitoa katika Baraza hili. Ninamuomba Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na kuziweka roho zao mahala pema peponi, Amin. KUIMARIKA MFUMO WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA:
12. Mheshimiwa Spika, hivi sasa inakaribia miaka miwili tangu kuwa na Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa. Ni jambo la faraja kuona nchi yetu inaendelea katika hali ya amani na utulivu. Nachukua tena fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa umahiri wake katika kuiongoza nchi yetu. Pia nampongeza sana Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa jinsi anavyotekeleza majukumu yake vizuri ya kumshauri na kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Aidha, shukurani za kipekee nazitoa kwa Viongozi wote wa Serikali, Vyama vya Siasa na wananchi kwa jumla kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
13. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa Serikali yetu. Waheshimiwa Wawakilishi wameonesha kuwa na upeo mkubwa wa majadiliano na udadisi katika utoaji wa hoja na michango yao ndani ya Baraza. Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa kina katika masuala mbali mbali yaliyojadiliwa katika Baraza hili, jambo ambalo linadhihirisha kukuwa kwa demokrasia na kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji wa Baraza letu.
14. Mheshimiwa Spika, ningependa kuelezea tatizo la utoro wa baadhi ya Wajumbe wa Baraza lako Tukufu, na hata baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri ambapo wakati mwengine unalazimika kuakhirisha shughuli za Baraza kwa muda kama ilivyotokea tarehe 25 Julai, 2012 ili kungojea Wajumbe watimize akidi (quorum) kabla ya kuendelea na shughuli zake. Ninawasihi sana Waheshimiwa Wajumbe wenzangu kuacha tabia hii kwani wananchi waliotutuma kuwawakilisha hapa wanatuona na kutushangaa.
15. Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe nikiwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Barazani, nawajibika pia kuwepo Barazani kwa muda wote Baraza linapoendelea. Lakini kwa nafasi yangu nikiwa Kiongozi wa Kitaifa wakati mwengine nalazimika kukosekana Barazani sio kwa sababu ya kupanga kwangu au kudharau shughuli za Baraza, bali ni kwa sababu ya kutekeleza majukumu mengine ya Kitaifa ambayo yanahitaji mahudhurio yangu na wakati mwengine kutakiwa hata kumuwakilisha Mheshimiwa Rais katika shughuli za Kitaifa ambazo asingeweza kuhudhuria yeye mwenyewe. Hata hivyo, kukosekana kwangu Barazani
Mheshimiwa Spika anakuwa na taarifa zangu zote. Hata hivyo, utaratibu upo wa Serikali kupata hoja za Wajumbe kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri. Ni vyema nikawakumbusha Waheshimiwa Wajumbe kwamba kama Kiongozi wa Kitaifa, mbali na jukumu hili la Baraza bado nakabiliwa na majukumu mengine ya kitaifa ambayo yanahitaji kushughulikiwa sambamba na jukumu hili la Baraza. Mambo yote hayo, yana nia ile ile ya kuwatumikia wananchi wetu.
MASUALA MUHIMU YALIYOJITOKEZA KATIKA BARAZA:
16. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa Nane wa Baraza lako Tukufu, Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara zetu zote walipata fursa ya kuwasilisha na kupitishiwa bajeti zao za makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013 pamoja na kueleza programu mbali mbali watakazo zitekeleza kwa kipindi hicho. Aidha, katika mkutano huu Miswada miwili ya Sheria imewasilishwa ambayo ni:
1) . Mswada wa Fedha (Finance Bill);
2) . Mswada wa Matumizi (Appropriation Bill);
Aidha, katika mkutano huu Waheshimiwa Wajumbe wamepata fursa ya kushiriki katika semina tano muhimu zilizolenga kuwaongezea Wajumbe uzoefu na taaluma katika masuala yafuatayo:
1. Semina kuhusu Mfumo wa Bajeti na Kanuni zinazoongoza Mijadala ya Bajeti.
2. Semina ya Kuwawezesha Wajumbe Wanawake katika Masuala ya Jinsia na Mawasiliano.
3. Semina ya Mashauriano baina ya Wenyeviti wa Kamati za Baraza na Maafisa Utafiti wa Baraza.
4. Semina ya Kupitia Ripoti za Wataalamu kuhusiana na “database” ya Wadau wa Kamati ya Baraza na Uwezo wa Wajumbe katika utungaji Miswada.
5. Semina kuhusu Elimu ya Katiba kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
17. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe kwa ushiriki wao katika mijadala ya Miswada ya Sheria na katika mada za Semina zilizowasilishwa, na ni imani yangu kwamba Wajumbe wamepata uwelewa mzuri wa masuala yaliyowasilishwa na hivyo itawasaidia katika shughuli zao ndani ya Baraza. Nakupongeza Mheshimiwa Spika, kwa juhudi uliyochukua mpaka kufanyika kwa Semina hizo.
MSIBA WA KUZAMA KWA MELI:
18. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 18 Julai, 2012 nchi yetu ilikumbwa na msiba mwengine mkubwa wa kuzama kwa meli ya M.V Skagit kwenye mkondo wa Kibaazi (meli saba kutoka kisiwa cha Chumbe). Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuja Zanzibar ilisadikiwa kuwa na abiria 290. Idadi hii ni kwa mujibu wa manifest iliyotolewa na wamiliki wa meli hiyo. Katika ajali hiyo, jumla ya waliokolewa wakiwa hai ni watu 146 na hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2012 ni maiti 136 wamepatikana ambao maiti 75 wametambuliwa na jamaa zao na 61 hawakuweza kutambuliwa na hivyo mazishi yao yamesimamiwa na Serikali. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahala pema peponi, Amin. Kwa wale waliokolewa wakiwa hai tumuombe Mwenyezi Mungu awazidishie uzima na awape afya njema. Aidha, Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na subira wale wote walioguswa na msiba huo kwa kupoteza ndugu na jamaa zao.
19. Mheshimiwa Spika, Serikali inawashukuru kwa dhati wale wote walioshiriki kwa njia moja ama nyengine katika operesheni za uokozi, mazishi na huduma nyengine zote zinazohusiana na maafa haya. Aidha, Serikali inapenda kuwashukuru wale wote waliotoa michango yao ya hali na mali kwa ajili ya kuwafariji na kuwasaidia waathirika wa ajali hii.
20. Mheshimiwa Spika, wakati wa msiba huu mzito Viongozi Wakuu wa nchi yetu walikuja kutufariji akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyemaliza muda wake Mhe. Dkt. Asha Rose Migiro.
21. Mheshimiwa Spika, vile vile nachukua fursa hii adhimu kutoa shukurani za Serikali kwa Waheshimiwa Mabalozi mbali mbali, Wakuu wa Makampuni na Mashirika mbali mbali kwa kutufariji na kwa misaada yao. Tunatoa shukurani nyingi kwa Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi, KMKM, Chuo cha Mafunzo na Kikosi cha Zima Moto na Uokozi kwa jitihada zao kubwa katika operesheni za uokozi. Tunawashukuru pia vikundi vya wazamiaji wa kujitolea vya Island Marine ya Malindi, Easy Blue Divers ya Jambiani na Jumuiya ya Wavuvi wa Kojani (KOFDO) kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi chote cha uokozi. Aidha, tunawashukuru wenzetu wa Red Cross, Wizara ya Afya, Wamiliki wa Mahoteli, Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini, vijana wetu wa Skauti, Viongozi wa Dini, Kamisheni ya Wakfu, Ofisi ya Mufti na Wajumbe wote wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa kwa mashirikiano yao makubwa katika kukabiliana na maafa haya.
22. Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshaunda Tume ya kuchunguza kuzama kwa meli ya M.V Skagit ili kupata taarifa sahihi juu ya ajali ya meli hiyo. Tume hii ya watu kumi inaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mhe. Abdulhakim Ameir Issa. Nawaomba wananchi pamoja na Taasisi zitakazohitajika kutoa taarifa wawe na mashirikiano na Tume ili kuweza kufanikisha kazi hii. Serikali inawaomba wananchi wawe wastahamilivu wakati Tume ikiendelea na kazi zake.
23. Mheshimiwa Spika, Serikali yetu itaendelea kujitahidi kuchukua hatua zinazostahiki ili kuhakikisha kwamba tunajenga uwezo wetu wa kujikinga na kukabiliana na majanga kama haya. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuifanyia mapitio Sheria ya Kuanzishwa Mamlaka ya Kusimamia Usafiri wa Vyombo vya Baharini na kusimamia kikamilifu utekelezaji wake. Aidha, Serikali imechukua hatua ya kuvisimamisha baadhi ya vyombo vya usafiri wa baharini kutokana na tatizo la uchakavu na kutokidhi viwango vya huduma za usafiri wa majini. Serikali pia kuanzia sasa haitaruhusu meli yoyote kuingizwa nchini mpaka Mamlaka husika kutoa kibali cha kuingizwa nchini meli hiyo. Aidha, Serikali haitaruhusu meli kuingizwa nchini iliyozidi umri wa miaka 15.
24. Mheshimiwa Spika, Serikali yetu pia inafanya juhudi za kununua meli kubwa ya abiria itakayokidhi mahitaji ya usafiri wa baharini katika Visiwa vyetu na katika maeneo ya mwambao wa nchi jirani kwa kupitia bajeti yetu hii tuliyokwisha ipitisha. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo tayari amekwisha elezea Barazani humu namna atakavyoweza kuzipata fedha hizo.
MASUALA YA MUUNGANO:
25. Mheshimiwa Spika, suala la Muungano limejitokeza sana katika mkutano huu. Hali hiyo imetokana na umuhimu wake kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano. Serikali zetu mbili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimesikia hoja za Waheshimiwa Wajumbe na hoja hizo zitaendelea kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
26. Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali, napenda kuzidi kutoa wito kwa wananchi wote wajitokeze kwa wingi kushiriki ipasavyo katika zoezi la utoaji wa maoni juu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanayoitaka.
27. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja na Kusini Pemba kwa kuitumia fursa yao vizuri na kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika hali ya amani na utulivu. Nawaomba wananchi wa Mikoa mingine kuendeleza utamaduni huu ili suala hili liweze kwenda salama na kwa mafanikio kwa Mikoa yote ya Zanzibar. Jambo muhimu ni kuvumiliana na kuheshimu mawazo ya kila mmoja wetu.
KUIMARISHA SEKTA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
28. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuleta mapinduzi ya kilimo, jitihada mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa ikiwemo kuwarahisishia wakulima kupata mashine za kufanyia kazi kama vile matrekta, mashine za kuvunia na upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo. Aidha, Serikali itaendelea na jitihada zake za kuimarisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji maji kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji na kufikia azma yetu ya kuongeza uhakika wa chakula nchini. Kutokana na umuhimu wa zao la karafuu nchini mwetu, Serikali itaendelea na mkakati wa uzalishaji miche ya mikarafuu na kuwapatia wakulima bila ya malipo ili kulirudisha zao la karafuu katika hali yake iliyokuwa nayo hapo nyuma.
29. Mheshimiwa Spika, Serikali pia itaendeleza sekta ya mifugo kwa kuongeza huduma ya upandishaji ng’ombe kwa sindano, kuimarisha huduma za uzalishaji na utibabu wa mifugo na kuongeza mwamko wa ufugaji wa ng’ombe na mbuzi wa maziwa. Aidha, Serikali itaweka mkazo katika suala zima la usindikaji wa bidhaa za mifugo ili kukuza fursa za ajira na kipato kwa wafugaji.
30. Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kuendeleza wavuvi wadogo wadogo, kuhamasisha ufugaji wa kisasa wa samaki na uvuvi endelevu. Mkazo zaidi utawekwa katika kuwavutia wawekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu. Aidha, Serikali itaimarisha sekta ya mifugo kwa kuendelea sekta ya elimu ya ufugaji wa kisasa kwa jamii, kufanya utafiti wa malisho ya mifugo na kuendeleza kazi za upatikanaji wa mbegu bora za mifugo.Mheshimiwa Spika, ningependa kuchukua fursa hii kukemea uvuvi haramu. Serikali itawachukulia hatua za kisheria wavuvi wowote watakaoendeleza uvuvi wa aina hii.
MATATIZO YA KIWANDA CHA SUKARI
:31. Mheshimiwa Spika, matatizo ya uwekezaji katika Kiwanda cha Sukari cha Mahonda ni ya muda mrefu na matatizo hayo yanachangiwa zaidi na uwezo mdogo wa mwekezaji wa kuekeza katika kuimarisha kiwanda na mashamba. Aidha, matatizo hayo yamepelekea kuwepo kwa migogoro inayohusisha matumizi ya ardhi baina ya mwekezaji na wananchi wanaoishi katika maeneo ya jirani huku wananchi wakidai kuachiwa maeneo hayo kuyatumia kwa ajili ya kilimo kwa vile mwekezaji huyo ameshindwa kuyaendeleza.
32. Mheshimiwa Spika, katika kulitafutia ufumbuzi suala hili, Serikali imezingatia mkataba baina yake na mwekezaji na tayari imeshawasiliana na mwekezaji huyo kumueleza nia yake kama ikibidi kukirejesha kiwanda hicho na mashamba yake Serikalini.
UWEZESHAJI WANANCHI:
33. Mheshimiwa Spika, upungufu wa ajira kwa wananchi wetu ni tatizo linaloikabili nchi yetu. Serikali inachukua juhudi mbali mbali ambazo zitasaidia kupambana na tatizo hilo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kuweza kujiajiri hasa vijana na wanawake kwa kuwapatia mikopo, mafunzo na vifaa. Katika kufanikisha hilo, Serikali kupitia Mfuko wa Rais wa Kujitegemea hadi sasa umeshakusanya shilingi milioni 600 ambazo zitatolewa kwa wajasiriamali wadogo wadogo kwa njia ya mikopo. Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Uwezeshaji wananchi Kiuchumi na Ushirika imeandaa programu maalum ya kutoa mafunzo kwa vijana 940 ili waweze kujiajiri. Hadi sasa vijana wapatao 710 wameshapatiwa mafunzo hayo na kuweza kujiajiri wenyewe katika sekta ya kilimo, uvuvi, utalii na mazingira
34. Mheshimiwa Spika, Serikali inaelewa kwamba suala la nishati ya umeme ni tatizo katika kisiwa cha Unguja na linakwamisha shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi. Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo. Hadi sasa, kwa kupitia msaada wa Shirika la Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Corporation) Serikali imeweza kukamilisha kazi za msingi zikiwemo upimaji wa njia mpya ya umeme wa ardhini na utengenezaji wa waya wa baharini wenye urefu wa kilomita 39.5. Utekelezaji wa mradi huu unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2012.
SEKTA YA MIUNDOMBINU:
35. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wajumbe wamelalamikia juu ya utendaji wa watumishi wa sekta ya miundombinu na Taasisi zake usioridhisha. Serikali imesikia malalamiko hayo na inayafanyia kazi kwa upana wake ikiwa ni pamoja na kuzingatia taarifa ya Kamati Teule ya Baraza lako Tukufu. Hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wajumbe waiache Serikali ili iweze kuyafanyia kazi malalamiko hayo na kuchukua hatua muafaka. Hapana shaka Waheshimiwa Wajumbe wana imani na Serikali yao na hivyo wataendelea na imani hiyo wakati hoja zao zinaendelea kushughulikiwa na Serikali.
36. Mheshimiwa Spika, katika mijadala ndani ya mkutano huu baadhi ya Wajumbe walionesha wasiwasi wao juu ya Makampuni ya Kichina kufanya kazi chini ya kiwango na kutokuwa na uaminifu katika mikataba na utendaji kazi wao. Ilielezwa kwamba misaada inayotolewa na Serikali ya China inakuwa na masharti ya kutumika kwa Makampuni kutoka nchi hiyo kutekeleza miradi inayotokana na misaada hiyo. Napenda kuwaeleza Waheshimiwa Wajumbe kwamba uhusiano wa nchi yetu na Jamhuri ya Watu wa China ni wa muda mrefu sasa, na wametusaidia miradi mingi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Mifano ya miradi hiyo ni ujenzi wa nyumba za mkopo nafuu, awamu ya kwanza na awamu ya pili, Kiwanda cha Sukari cha Mahonda, Uwanja wa Amani, ambavyo vyote hivi tunaendelea kuvitumia hadi sasa.
37. Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa Serikali ya China kutumia makampuni yake katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa sasa ni jambo la kawaida na hutumika na baadhi ya nchi na Mashirika yanayotoa misaada katika nchi zetu. Kama alivyosema Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mfano wa wazi ni Mashirika ya BADEA, JICA, KOICA ambayo yanatumia utaratibu huu. Jambo la msingi ambalo Serikali yetu imekuwa ikilizingatia ni kuhakikisha kuwa makampuni hayo yanakuwa na viwango na uwezo wa kufanya kazi zinazokusudiwa ili kufikia malengo na matarajio yetu.
38. Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ujenzi katika Uwanja wa Ndege, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba tayari Serikali imeshakubaliana na Mkandarasi wa jengo jipya la abiria na kuondosha utata wa kisheria uliokuwepo na vile vile Serikali inaendelea na mradi wa utanuzi wa njia ya ndege (Taxiway) kupitia Benki ya Dunia na imeanza kuwalipa fidia wananchi ambao mali zao zitaathirika katika zoezi hilo. Napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali kuipongeza sana Kamati ya Wazee wa Kiembesamaki walioshirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi iliyojitokeza katika eneo hilo. Kutokana na ushirikiano mkubwa wa Kamati ya Wazee hao wa Kiembesamaki, kazi za kuyahamisha makaburi katika eneo la uwanja imeanza rasmi jana tarehe 09 Agosti, 2012, na leo hii huenda kazi hiyo ikakamilika.
USAJILI WA MELI ZA NJE KUPITIA MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI:
39. Mheshimiwa Spika, tarehe 27 Juni, 2012 vyombo vya habari hapa nchini (The Citizen) na nchi za nje (International News Agency- Bloomberg) viliandika makala kuhusu usajili wa meli kumi za mafuta (Tankers). Kupitia makala hiyo ilidaiwa kwamba meli hizo zilisajiliwa Zanzibar na zinapeperusha bendera ya Tanzania na kwamba zinafanya biashara na Makampuni ya mafuta ya Serikali ya Iran. Jambo hili ni kinyume na Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 1429 na Amri ya Utekelezaji wa Azimio hilo (Executive Order) iliyotolewa na Serikali ya Marekani na Nchi za Jumuiya ya Ulaya.
40. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa hii Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano alitoa taarifa kwa Baraza lako Tukufu mnamo tarehe 24 Julai, 2012. Serikali ililifuatilia suala hili kwa undani na imegundulika kuwa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) kupitia kwa Wakala wetu wa Dubai Philtex ilisajili meli 36 za Iran za Mafuta (crude oil tankers) na Makasha (containership) na kupeperusha bendera ya Tanzania. Nchi ya Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Umoja wa Mataifa na iwapo itatokea nchi yoyote kuisaidia kukwepa Azimio hilo nchi hiyo nayo itawekewa vikwazo kama hivyo vilivyowekewa Iran. Hivyo, baada ya kugundua ukweli kwamba meli hizo zinapeperusha bendera ya Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika hatua za kuzifutia usajili meli hizo na pia kuifutia uwakala kampuni ya Philtex. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya uchunguzi zaidi kujua ni vipi usajili huo ulifanyika. Pamoja na tukio hilo, uhusiano wetu na Iran utaendelezwa katika mambo mengine.
UIMARISHAJI WA UENDESHAJI WA SERIKALI ZA MITAA:
41. Mheshimiwa Spika, Serikali imezisikia hoja za Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu za kutaka kuimarishwa kwa uwezo na utendaji kazi wa Serikali za Mitaa. Kwa kuona umuhimu wa suala hilo, Serikali kupitia Mradi wa mageuzi ya Serikali za Mitaa itaendelea na kazi ya kuwasogezea wananchi huduma ikiwa ni pamoja na kuunda mipaka mipya ya Mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kusimamia utekelezaji wa sera ya Serikali za Mitaa, kuunda vikundi kazi vitakavyotumika katika kupitia mfumo wa kodi na mapato wa Serikali za Mitaa na muundo wa Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali itazifanyia mapitio na marekebisho Sheria namba 1 ya mwaka 1998 ya Mamlaka ya Utawala wa Mikoa na Sheria namba 3 na 4 ya mwaka 1995 ya Serikali za Mitaa
.42. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Serikali za Mitaa na Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji imekusudia kwa dhati kabisa kutekeleza mkakati mpya wa uzoaji taka na uondoaji wa wanyama wanaozurura ovyo ndani ya maeneo ya Manispaa ya Zanzibar na vitongoji vyake kwa kushajiisha vikundi vya mazingira, kutenga eneo jipya la kutupia taka lenye ukubwa wa hekta 15, kuimarisha huduma za usafi wa mji kwa kupitia Mradi wa Huduma za Miji (ZUSP), na uendelezaji wa ukarabati wa miundombinu ya masoko yalioko katika maeneo ya Mkoani na Chake Chake.
43. Mheshimiwa Spika, Bado tatizo kwa baadhi ya wananchi wetu kuiacha mifugo yao kama ng’ombe, mbuzi na punda kuzurura ovyo katika Manispaa ya Zanzibar jambo ambalo tayari limeshakemewa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein. Natoa agizo kwa Taasisi zote zinazohusika kuchukua hatua zinazofaa kisheria ili kuona tatizo hili linaondoka mara moja katika mji wetu.
MATATIZO YA ARDHI:
44. Mheshimiwa Spika, bado nchi yetu inaendelea kuwa na matatizo sugu ya ardhi ambayo yanatishia utulivu na amani katika nchi yetu. Serikali tayari imeshawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wizara husika kuyashughulikia matatizo ya ardhi ambapo kwa namna moja au nyengine na wao ni wahusika wa matatizo hayo. Hivi sasa ni muda muafaka kwa Serikali kufuatilia utekelezaji wa agizo hili na kwa wale watakaoonekana kutofuatilia utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo yao, Serikali haitasita kuwachukulia hatua stahiki. Natoa wito kwa mara nyengine tena kwa Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Taasisi husika kuchukua hatua za haraka za kutatua matatizo ya ardhi katika maeneo yao. Naomba kuchukua fursa hii kuwanasihi wananchi wote kuachana na tabia ya kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa Sheria katika masuala ya ardhi. Aidha, ni mategemeo yangu kwamba Kamati Teule itakayoundwa na Baraza la Wawakilishi itasaidia kuchunguza baadhi ya migogoro hiyo na kutuletea mapendekezo yao ili hatua muafaka ziweze kuchukuliwa na Serikali.
MGOGORO WA WANANCHI WA CHWAKA NA MARUMBI:
45. Mheshimiwa Spika, mgogoro baina ya wananchi wa Chwaka na Marumbi ni wa muda mrefu ambao umedumu kwa takriban miaka 31 sasa. Tatizo kubwa ni ugomvi unaotokana na matumizi ya rasilimali za bahari baina ya pande mbili hizi. Kamati mbali mbali ziliundwa huko nyuma kutatua tatizo hili na yapo mafanikio yaliyopatikana ya kuwepo kwa utulivu. Inasikitisha kuona mgogoro huu unakuwa ukiibuka mara kwa mara kwa sura tofauti.
46. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wananchi wa pande hizi mbili itazidi kuushughulikia mgogoro huu hadi ufumbuzi wa kudumu upatikane ili wananchi wa Chwaka na Marumbi waweze kuishi pamoja kwa salama na amani. Tarehe 7 Agosti, 2012 nilifanya ziara ya Marumbi na kukutana na wananchi wa eneo hilo na kukisikia kiini cha mgogoro huo. Hapo baadae kidogo, kabla ya mwisho wa mwezi huu nitafanya ziara ya kuonana na wananchi wa Chwaka ili nisikie kiini cha mgogoro huu kwa upande wao. Nikesha yasikia hayo, Serikali itatafuta namna ya kuumaliza mgogoro huo.
KUIMARISHA HUDUMA ZA JAMII:
47. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza elimu na kuzalisha wataalamu nchini, Serikali imeandaa Mradi wa Sayansi na Teknolojia ambao unatekelezwa na SUZA kwa mashirikiano na Benki ya Dunia. Mradi huu una lengo la kununua vifaa vya maabara na ICT pamoja na kusomesha wakufunzi kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili (Shahada ya Pili) na Shahada ya Uzamivu (PhD). Pia, Serikali imeongeza kima cha fedha kwenye Mfuko wa Mikopo ya Elimu ya Juu kwa lengo la kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi kujiunga katika elimu ya juu pamoja na kuzalisha wataalamu wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya shughuli za kitaalamu nchini. Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha Baraza la Upimaji na Tathmini ya Elimu ili kudhibiti tatizo la udanganyifu na kuvuja kwa mitihani. Baraza hilo kuanzia mwaka huu wa fedha litaratibu kwa karibu zaidi mitihani yote ya kidato cha nne, sita na ualimu ambayo inaendeshwa na Baraza la Mitihani la Taifa. Sambamba na juhudi hizo, Serikali inasisitiza kwamba wazazi, wanafunzi na walimu wasijihusishe katika vitendo vya udanganyifu wa mitihani
.48. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Jimbo la Sichuan ya China kwa msaada wao kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa madeski 480 ambayo tayari yamekwisha sambazwa katika skuli mbali mbali za Unguja ambazo zilikuwa na upungufu mkubwa wa madeski. Madeski hayo hayakuweza kusambazwa kwa Skuli za Pemba kwa kuhofia kuvunjika wakati wa usafirishaji. Hata hviyo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika bajeti yake hii itapeleka pesa ili madeski ya baadhi ya Skuli za Pemba yachongwe huko huko.
49. Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wake inaendelea kutekelezwa. Serikali kupitia Mamlaka ya Maji (ZAWA) inafanya juhudi za kuimarisha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji katika maeneo yote ya mijini na vijijini sambamba na kuimarisha huduma za uchunguzi wa ubora wa maji yanayozalishwa. Lengo la juhudi hizi ni kuwawezesha wananchi kupata huduma hii muhimu muda wote na kwa gharama nafuu na kwa masafa mafupi kadiri iwezekanavyo hadi kufikia mwaka 2015.50. Kwa Sekta ya Afya,
Mheshimiwa Spika, hii ni miongoni mwa sekta muhimu katika nchi yetu. Kwa kuelewa umuhimu huo, Serikali katika mwaka huu wa fedha inakusudia kuimarisha huduma za kinga katika maeneo mbali mbali, ikiwemo kutokomeza maradhi ya malaria, UKIMWI, kifua kikuu na ukoma ikiwa pamoja na kuendelea kutoa huduma za chanjo za akina mama na watoto na kutoa elimu ya afya kwa jamii. Vile vile, Serikali itaimarisha huduma za tiba, zikiwemo huduma katika kliniki maalum na huduma za damu salama. Aidha, Serikali katika mwaka huu wa fedha inakusudia kuchukua hatua za awali za kuifanya Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa Hospitali ya Rufaa na kuanza matayarisho ya kuzipandisha daraja Hospitali za Kivunge, Makunduchi, Micheweni, Wete na Abdalla Mzee.
KUIMARISHA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO:
51. Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa kwamba yametokea mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano duniani kutoka kwenye mfumo wa analogia na kwenda kwenye digitali. Ni wazi kwamba nchi yetu inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwepo kwa pengo la teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano. Kwa hivyo, si vyema kuendelea kubaki nyuma katika nyanja hii muhimu ya mawasiliano. Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na habari, sera na miongozo ya matumizi ya huduma za mawasiliano na habari itakayoendana na mabadiliko ya teknolojia hiyo duniani. Hatua hii vile vile itazigusa Taasisi zetu zote zinazotumia huduma ya habari na mawasiliano
.52. Mheshimiwa Spika, Serikali imeliimarisha zaidi Shirika la Utangazaji (ZBC) katika kutimiza lengo lake la kuwapatia habari sahihi na vipindi vya kuelimisha wananchi wa Zanzibar na nchi jirani na kurusha vipindi vya Redio na TV kwa muda wa saa 24. Hii inatokana na kufunga mitambo mipya yenye kutumika katika teknolijia ya Digital.
HIFADHI YA JAMII NA MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI WA MTOTO:
53. Mheshimiwa Spika, suala la hifadhi ya jamii na udhalilishaji wa watoto linaendelea kuwa changamoto kubwa katika nchi yetu. Kama inavyoeleweka kwamba watoto, wanawake na wazee wana haki zinazotambuliwa Kitaifa na Kimataifa. Inasikitisha kuona kwamba matukio ya udhalilishaji wa watoto kijinsia yamekuwa yakilalamikiwa siku hadi siku hasa kuhusu hatua zinazochukuliwa. Kwa azma ya kudhibiti suala hili Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii, kuandaa Sheria na kuimarisha vituo vya mkono kwa mkono (One Stop Centre) kwa kutoa mafunzo, miongozo na vifaa. Vile vile, Serikali imo katika hatua ya kuipitia Sera ya Uhai, Uhifadhi na Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2001 ili iendane na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2011.
54. Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha matunzo na huduma kwa wazee ikiwa ni pamoja na kuzifanyia ukarabati nyumba wanazoishi na kuwaongezea posho za kujikimu. Pia Serikali inaendelea na kazi ya utayarishaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii ili kuweka muongozo thabiti wa kutoa huduma bora kwa makundi maalum ndani ya jamii yetu. Katika hatua ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuongeza fursa za ajira na kupunguza umasikini, Serikali inaendelea na utaratibu wa kuanzisha Benki ya Wanawake. Hivi sasa tayari mtaalamu mwelekezi ameshaajiriwa na kuwasilisha ripoti yake ya awali ya kazi (inception report) na kuanza kazi za uchambuzi yakinifu kwa uanzishaji wa benki hiyo.
SENSA YA WATU NA MAKAAZI:
55. Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza mara nyingi katika Baraza hili kwamba mwaka huu ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makaazi hapa nchini petu. Sensa imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Nazidi kutoa wito kwa Viongozi wote wa ngazi zote katika nchi yetu wakiwemo Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kuendelea kuhamasisha wananchi katika Majimbo yao kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ifikapo tarehe 26 Agosti, 2012. Ni vyema wananchi wakaelewa kwamba Sensa ni kwa faida yetu sote na Taifa letu kwani takwimu na taarifa zinazokusanywa ni kwa ajili ya kutumika katika kuandaa sera na kupanga mipango na programu za maendeleo katika nchi yetu.
MAZINGIRA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI:
56. Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchafuzi wa mazingira hasa suala la uchimbaji wa mchanga na kifusi kiholela, ukataji wa miamba kwa ajili ya matufali na uingizaji wa bidhaa chakavu za umeme na elektroniki. Aidha, pamoja na Serikali kupiga marufuku uingizaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki, bado kuna watu wachache ambao wanaendelea kuingiza na kutumia mifuko hiyo. Natoa wito kwa Taasisi zinazohusika kuendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaoingiza na kutumia mifuko hiyo na kuharibu mazingira yetu. Kwa upande wa wananchi, kwa pamoja tuache kabisa kutumia mifuko ya plastiki kwani inaweza kutuletea madhara makubwa ya kiafya
.57. Mheshimiwa Spika, katika kuinusuru nchi yetu na athari za uchafuzi wa mazingira, Taasisi inayohusika ichukue hatua ipasavyo katika kuhakikisha kwamba sera mpya ya mazingira inakamilika pamoja na kusimamia kikamilifu utekelezaji wake.
58. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zimejitokeza katika maeneo kadhaa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kukauka kwa vianzio vya maji, uingiaji wa maji ya bahari katika mashamba ya kilimo unaotokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, kuongezeka kwa maji ya chumvi katika visima, kubadilika kwa miongo na kupanda kwa hali ya hewa. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeandaa mkakati madhubuti pamoja na kufanya tafiti juu ya athari za kiuchumi zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Napenda kuwasihi wananchi kuchukua hadhari kubwa ikiwa pamoja na kutokukata miti ovyo, kutokujenga katika vianzio vya maji, kuhifadhi mikoko na kupanda miti ili kuongeza kina cha maji ardhini ambacho kimeanza kupungua sana.
MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA:
59. Mheshimiwa Spika, matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya bado ni changamoto inayoikabili nchi yetu licha ya juhudi mbali mbali ambazo Serikali imekuwa ikizichukua katika kukabiliana na janga hili. Ili kushinda vita hivi ni wazi kuwa kila mwananchi ana jukumu la kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya janga hili. Napenda niwahakikishie wananchi kwamba Serikali itawalinda wale wote watakaosaidia katika kutoa taarifa zinazohusiana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Sambamba na hili, napenda kuchukua fursa hii kuzipongeza Taasisi mbali mbali ambazo zimekuwa zikiunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Aidha, napenda kutoa wito kwa jamii kutoa kila aina ya msaada katika huduma za marekebisho ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini (Sober houses).
MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU:
60. Mheshimiwa Spika, suala la watu wenye ulemavu bado linahitaji msukumo mkubwa katika kuhakikisha kwamba kundi hili linapata huduma zote zinazostahiki. Watu wenye ulemavu bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo udhalilishaji na unyanyapaa. Sote tunapaswa kuelewa kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yetu na wanastahiki kupata haki zote kama yanavyopata makundi mengine ndani ya jamii. Katika kulisimamia suala hili, Serikali inaendelea kuweka miongozo ya kisera na kisheria ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapatiwa huduma na haki wanazostahiki. Napenda kutoa wito kwa Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu kuendelea kushirikiana na Serikali katika suala zima la kutetea haki za watu wenye ulemavu. Aidha, natoa wito kwa wazazi na walezi kuachana na tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu katika majumba yao kwani kufanya hivyo kutawakosesha fursa ya kujumuika na jamii pamoja na kupata huduma muhimu za kijamii na kiuchumi.UKIMWI:
61. Mheshimiwa Spika, Ukimwi bado ni tatizo kubwa katika nchi yetu. Hii ni kutokana na athari zake kiuchumi na kijamii. Ni vyema wananchi tukaelewa kwamba dunia bado haina tiba sahihi ya maradhi haya thakili. Hivyo ni wajibu wetu wananchi sote kujizuia na vitendo vyote vinavyoweza kupelekea kupata maambukizi ya maradhi haya. Aidha, nawasihi wananchi kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wale wenzetu ambao kwa bahati mbaya tayari wameshapata maambukizi. Ni vyema kila mmoja wetu kuchukua hatua ya kuchunguza afya yake ili kujua kama yuko salama au amepata maambukizi ili kuchukua hatua za mapema zinazostahiki mapema.
MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN
62. Mheshimiwa Spika, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuendelea kutekeleza ibada ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Tumuombe Mwenyezi Mungu atutakabalie funga na ibada zetu na atujaalie tumalize Ramadhani kwa salama na amani, Amin
63. Mheshimiwa Spika, tukimaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhani tunakabiliwa na Sikukuu adhimu ya Idd el Fitri. Kwa vile hatutaweza kukutana hapa katika hali hii, napenda kuchukua fursa hii, kutoa mkono wa Idd Mubarak kwa Wajumbe wote na kuwatakia Sikukuu njema wananchi wote na kuwataka kufurahia sikukuu hiyo kwa furaha, utulivu na amani. Nawaomba madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuwa waangalifu wakati wanapotembea barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.HITIMISHO:64. Mheshimiwa Spika, nazidi kuwaomba wananchi waendelee kuishi kwa amani, umoja na upendo na kuacha vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria na vitakavyo ashiria uvunjifu wa amani na utulivu. Rasilimali kubwa ya Wazanzibari ni amani na utulivu. Naomba kila mmoja wetu atimize wajibu wa kulinda amani na utulivu uliopo.
65. Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, naomba kuchukua nafasi hii kwa mara nyengine tena kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi hii ya kuzungumza na Baraza lako Tukufu pamoja na wananchi. Aidha, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako pamoja na wananchi wote kwa kunisikiliza. Vile vile, napenda kuwatakia Wajumbe wote wa Baraza hili safari njema ya kurudi Majimboni mwao kwenda kuwatumikia wapiga kura wao.
Mwisho kabisa, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wake zangu, Bibi Pili Juma Iddi na Bibi Asha Suleiman Mohammed kwa kunisaidia na kunivumilia wakati wa kipindi chote cha Baraza. Shukrani za pekee ziende kwa Bi. Asha kwa kuliangalia vizuri Jimbo langu la Kitope wakati nikiwa katika shughuli za Baraza.66. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 10 Oktoba, 2012 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
67. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment