Habari za Punde

Madaktari, wakunga lawamani kusababisha kifo

Na Hafsa Golo
MADAKTARI na wauguzi katika hospitali Cottege ya Kivunge wilaya ya Kaskazini "A" Mkoa wa kaskazini Unguja wameingia lawamani baada ya kudaiwa kufanya uzembe uliosababisha kifo cha mtoto mchanga, ambaye inasemekana alifariki kabla ya kuzaliwa.

Hayo yameelezwa na mzee Daudi Pili Daudi ambaye ni baba mzazi wa mgonjwa aliyefikishwa hospitali kwa ajili ya kujifungua wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi  wa habari hizi huko nyumbani kwake Mkokotoni Kibaoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema uzembe na dharau iliyowatawala waguzi na madaktari wa hospitali hiyo katika wodi ya wazazi kumesababisha kumpoteza maisha ya mtoto huyo ambaye yeye ni mjukuu wake, bila ya kuzingatia na kujali kwamba wananchi wanahitaji kupewa huduma bora.

Akisimulia mkasa huo ulivyokuwa Daudi alisema kuwa alimfikisha mtoto wake Anisha Daudi hospitalini hapo August 27, majira ya saa 6:00 za usiku, mara tu baada ya kuuguwa hasa baada ya kuzingatia kuwa mtoto huyo ni mimba yake ya kwanza hivyo amuwahishe kituo cha afya mapema ili kwa lengo la kuepusha matatizo ambayo yangeweza kujitokeza.

Aidha alisema ilipofika siku ya pili mnamo majira ya saa 5:00 asubuhi wakati huo aliikuta hali ya mtoto wake ikiwa mbaya sana na aliamua kuwatafuta wauguzi ili waweze kumsaidia lakini alishindwa kuwasiliana nao kwani hakujua wapi walipojichimbia wauguzi hao.

"Nilipomuona mtoto wangu anapiga kelele akiita madaktari wamsaidie niliranda kila sehemu kuwatafuta lakini ilishindikana sikuweza kuwajua walipo nikafika hadi maabara nikakutana na mtu wa maabara nikamuelezea akawapigia simu, na hapo walichukuwa saa moja na nusu hawakutokezea huku hali ya mtoto ikiendelea kuwa mbaya", alisema baba mzazi.

Alisema kuwa jambo lililomshangaza kwa wauguzi hao kudai shilingi elfu kumi za vifaa kwa ajili ya kujifungulia na baada ya kutoa pesa hizo yeye hakuwaona kutoka kwenda kununua na alipohitaji risiti yake waligoma kumpatia.

Sambamba na hayo alidai kuwa Agosti  29 majira ya saa 12:30  alifika hopitali kwa kumkaguwa mtoto wake na akakuta hajapatiwa huduma yoyote hali ambayo ikamsababishia kulalamika kwa muuguzi na hatimae akatakiwa kuondoka na mgonjwa wake akamtafutie haspitali nyengine.

Kwa upande wake Daktari dhamana Dk. Tamimu Hamad Said amekiri kuwepo kwa kesi hiyo ya kufariki kwa mtoto kabla ya kuzaliwa hali ambayo alidai kuwa  ni suala la kawaida kutokea kwenye uzazi.

"Nimeikuta hiyo kesi ilitokezea mtoto alifariki kabla ya kuzaliwa na baada ya kuzaliwa sco imeonesha" 0",kwa maana tayari mtoto huyo alikuwa amekufa tangu tumboni",alisema

Daktari huyo alikanusha madai ya baba huyo kwamba waliweka kikao cha dharura, kwa vile jambo hilo  kwao ni desturi kufanyika kikao cha asubuhi, ili kutathimini taratibu za kazi, pia kutolewa chumba cha kuzalia na kupelekwa wodini ni utaratibu wa kawaida na kila mzazi baada ya kujifunguwa.

Akizungumzia suala la mama mjamzito kulalamika wakati anapokuwa akikaribia kujifungua alisema ni jambo la kawaida hivyo hakuona kama  polikuwepo na kitendo cha kudharauliwa au kapuunzwa.

"Mtu akiwa na maumivu huachiwa aendelee mpaka wakati unapofika wa kijifungua, na yeye amefanyiwa huduma zote baada ya kufika hospitali"alisema.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Tiba, Dk. Mohamed Dahoma alikiri kupokea kwa taarifa hiyo kutoka kwa mlalamikaji na hatuwa za kisheria zitachukuliwa baada ya kuthibitika kutokea kwa kosa hilo.

Kaimu huyo alisema kuwa serikali imeweka huduma kwa wananchi hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kupatiwa huduma bora bila ya kikwazo chochote hususan kinamama wajawazito.

"Taarifa hiyo imenifika muda sio mrefu na tayari nimeshaanza kuifanyia kazi, nimewaita maofisa wangu waifatilie kwa kina na ikithibitika hali hiyo imefanyika hatiwa zitafata na  hasa linapoimngia suala la uzazi hakuna kumfumbia macho atakae fanya uzembe wa makusudi", alisema.     

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.