Habari za Punde

China yaikabidhi Abdalla Mzee vifaa uchunguzi

Na Bakari Mussa, PEMBA
SERIKALI YA watu wa China imekabidhi msaada wa vifaa mbali mbali vya matibabu vyenye thamani ya shilingi milioni 80 kwa hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo Mkoani, Pemba.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya serikali ya Watu wa China, kiongozi wa timu ya madaktari wa Kichina, Dk. Sun Yong Hu, alisema kuwa kutolewa kwa misaada hiyo kwa wananchi wa Pemba ni ishara ya ushirikaino na uhusiano mwema ulipo kati ya nchi hiyo na  Zanzibar.

Dk. Hu alisema kutokana na kuwathamini wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla, wamelazimika kuleta vifaa hivyo vikiwemo vya uchunguzi wa maradhi mbali mbali yanayowasumbuwa wananchi.

Alifahamisha kuwa vifaa vya uchunguzi ambayo ni miongoni mwa msaada vitasaidia kubaini matatizo mbali mbali ya kiafya yanayowakabili wananchi na kuepuka kusafiri nje ya Pemba kufuata huduma hizo.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni Getroscopy ambayo itatumika kwa uchunguzi wa maradhi ya tumbo, mashine ya kuchunguzia maradhi ya koo, mashine ya kuchunguzia mifupa pamoja na vifaa vyengine.

Alisema vifaa hivyo ni vya mwanzo kuwepo katika hospitali za Zanzibar na vitakuwepo katika hospitali hiyo tayari kutoa huduma kwa wananchi.

Dk. Hu, aliwataka wananchi wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla kufuata huduma hizo katika hospitali ya Mkoani, ambapo uchunguzi na matibabu yake yatatolewa kwa thamani ndogo.

“Tunawataka wananchi wa Zanzibar kufuata huduma zetu katika hospitali ya Mkoani ili kupunguza kufuatia huduma hizo nje ya Zanzibar kwa vile vifaa hivo kwa sasa tunavyo”, alisema.

Kwa upande wake Dk. Shi Xilo Hud, ambae ni mtaalamu wa maradhi ya koo, alisema kifaa ambacho wamekipata hospitalini hapo kitawasaidia wananchi wa Zanzibar kufanya uchunguzi wa uhakika wa maradhi hayo kutokana na kwamba kitaingizwa katika mwili wa mgonjwa kupitia mdomoni hadi tumboni.

Aidha Daktari dhamana wa hospitali hiyo, Dk. Mohammed Ali Jape, akipokea msaada huo kwa niaba ya wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema wamefarajika vya kutosha kupatiwa msaada huo na kuahidi kwamba watautumia kwa maslahi ya wananchi.

Alisema kuwa ni wazi kuwa serikali ya Watu wa China inathamini juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutoa huduma za afya kwa wananchi wake na ndio ikapata hamu kubwa ya kuleta misaada hiyo.

“Tutaendelea kuthamini misaada inayotolewa na wafadhili mbali mbali, ikiwemo serikali ya Watu wa China katika kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wananchi wetu”, alisema  Dk. Jape.

Alisema ana matumaini kwamba wananchi wa Pemba, watautumia msaada huo kama walivyoelezwa na madaktari hao na kuondokana na usumbufu waliokuwa nao wakufuata huduma hiyo nje ya kisiwa cha Pemba.

Misaada uliotolewa na serikali ya Watu wa China ni pamoja na mashine  za uchunguzi wa maradhi mbali mbali ikiwemo na dawa ya binaadamu.

 

                                    

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.