Mwanajuma Mmanga na Mwashamba Juma
VYUO vya mafunzo Zanzibar vinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uchakavu wa majengo na vitendea kazi kwa wanafunzi wanaofikishwa vyuoni hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi kaimu Mkuu wa Utawala chuoni hapo SACP Ali Abdalla Ali alisema uhaba wa vitendea kazi kwa wanafunzi walioko mafunzoni ikiwemo vifaa vya ufundi vya kukamilisha mafunzo yao bado ni tatizo jambo ambalo limepelekea kutoa mafunzo ya aina moja tu ya kilimo.
“Zamani wanafunzi walipewa kazi za vitendo, kama ufundi seremala, vyarahani pamoja na kushughulikia viwanda vya sabuni, lakini kwa sasa vyote vimekufa kwa kukosekana kwa rasilimali na kusalia mafunzo ya kushika jembe tu” alifafanua mkuu huyo.
Alisema mrundikano mkubwa wa wanafunzi wanaowekwa rumande chuoni hapo bado ni tatizo na kupelekea chuo kutumia huduma za ziada ukiangalia bajeti iliyoko ni kwa ajili ya wafungwa tu.
Akizungumzia suala la haki za watoto zinavyotekelezwa chuoni hapo kaimu mkuu huyo alisema chuo kinazingatia haki za binaadamu kwa kuwapa watoto fursa ya kucheza kama watoto wengine pamoja na kuwapatiwa mahitaji yote ya msingi ikiwemo huduma ya afya.
“Wanafunzi wanapopata matatizo ya kiafya tuna hospitali ya wafungwa, pamoja na hospitali ya magereza lakini kwa kesi kubwa tunatumia hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa wanafunzi wa Unguja na Pemba” alifahamisha.
Alisema chuo kinategemea kuimarisha huduma bora kwa kujenga jengo jipya na la kisasa lenye kuzingatia haki zote za bianaamu kwa kugawa magereza ya wanawake, watoto na wanafunzi wakawaida, aidha alifahamisha kuwa hatua za awali za ujenzi huo zimeanza.
Akizungumzia huduma za mitondoo (kujisaidia choo kwenye ndoo) zinazotolewa chuoni hapo alisema hutolewa kwa nyakati za usiku tu lakini kukitokea tatizo kubwa msimamizi mkuu wa magereza atalazimika kuwafungulia na kutumia vyoo vya nje.
Nae Mwanasheria mkuu chuoni hapo, Seif Maabad alisema kuwekwa kwa watoto wachanga chuoni hapo wakuwatendei haki watoto hao lakini kwa kutekeleza haki ya kupatiwa malezi ya mama hulazimika kubakia chuoni hapo hadi miezi 18.
“Kwa mujibu wa mfumo wa malezi ulivyo, bado mtoto anahitaji malezi ya mama yake, hana jinsi lazima anabakia na mama, au achukuliwe na jamaa wa mama yake” alisema Mwanasheria huyo.
Alisema ikishindikana mtoto kuchukuliwa na jamaa zake wakati bado mama anaendelea kutumikia chuoni hapo, mtoto huyo hukabidhiwa Idara ya Ustawi wa jamii, Maendeleo ya Wanawake na watoto kwa matunzo zaidi.
Zaidi ya wanafunzi 300 wako rumande chuoni hapo na 150 wafungwa kati yao wanne wanawake, wanne raia wa kigeni kutoka Kenya, Comoro, Italia na Urusi, ambapo wanafunzi 10 ni watoto.
No comments:
Post a Comment