Habari za Punde

Mahiza ataka madereva wazembe washughulikiwe

Na John Gagarini, PWANI
ZAIDI ya ajali 15 zimeripotiwa katika barabara ya Dar es Salaam – Morogoro na Chalinze - Segera kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva unaotokana na utumiaji vileo ikiwemo viroba na konyagi.

Mbali ya ajali hizo pia imetajwa robo tatu ya ajali zinazotokea mkoani
humo kuwa zinatokana na kupishana kwa magari.

Kutokana na kukithiri kwa ajali hizo, Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantum Mahiza, amewajia juu baadhi ya madereva wasiofuata sheria za barabarani na wamiliki ambao wanaajiri madereva hao bila kuzingatia vigezo na sifa za udereva.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha, alisema umefika wakati wa yeyote atakayekiuka sheria za barabarani achukukuliwe hatua kali ili kukomesha ongezeko la ajali zinazopoteza raslimali watu na ongezeko la watu wenye ulemavu.

Mkuu huyo alisema miezi michache iliyopita ajali za barabarani ziliweza kudhibitiwa kwa aslimia 30, lakini hivi sasa madereva wamonekana kupunguza kasi ya kuwa makini na kujisahau.

Mahiza aliwataka madereva kuzingatia kanuni na taratibu kwani ajali nyingi zinatokea kwa kutofuata misingi hiyo na hivyo kuipa wakati mgumu serikali kwa kupoteza bajeti kubwa kwa kushughulikia ajali zinazotokea.

Hata hivyo alisikitishwa na baadhi ya wananchi ambao huwa wakishabikia mwendo kasi jambo ambali limekuwa liwapa madereva munkari wa kuongeza mwendo kasi na kusababisha ajali.

Mbali na ajali Mahiza alizungumzia masuala kadhaa ikiwemo zoezi la sensa linaloonekana kukumbwa na vishawishi vya kisiasa na kidini vinavyoshawishi wananchi kutoshiriki katika zoezi hilo muhimu la kimaendeleo.

Kwa miezi mitatu iliyopita ajali 3 hadi 5 zilikuwa zikitokea katika barabara ya Dar es Salaam –Morogoro na Chalinze- Segera kwa siku wakati kwa wiki tatu mfululizo ni ajali zaidi ya 5 hutokea kwa siku katika barabara hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.