Habari za Punde

UVCCM yalaani vipeperushi kuhusu muungano

Madina Issa na Hafsa Golo
UMOJA wa Vijana wa CCM Zanzibar (UVCCM), umesema kuwa haukubaliani na vitendo vya kihuni vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaosambaza vipeperushi vyenye lengo la kuwachanganya wanaCCM juu ya kupinga msimamo wa chama hicho wa serikali mbili.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar, Jamal Kasssim Ali alieleza hayo jana katika ofisi ya Umoja huo ulipo Gymkhana mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kaimu huyo wa UVCCM amewalaani watu wenye tabia ya kusambaza vipeperushi hivyo ambavyo lengo lake ni kuwachanganya wanaCCM juu ya msimamo wa kuunga mkono serikali mbili katika Muungano.

Alisema vipeperushi hivyo vinavyowapotosha wanaCCM vimepambwa kwa picha za viongozi na nembo ya CCM ambavyo vina ujumbe wa kuondokana na mfumo wa muungano wa serikali mbili.

Alifahamisha kuwa msimamo wa CCM utabakia kama ulivyo kuwa ni serikali mbili katika muungano na kuwataka wanaCCM kuvipuuza vipeperushi hivyo ambayo vinalenga kuwapotosha.

Alisema kuwa CCM ina jukumu la msingi la kuulinda muungano uliokuwepo kwa thamani yoyote, kwani muungano ndio ulioleta ustawi wa wananchi wa Zanzibar na Tanzania bara.

Kaimu huyo alikiri kuwepo kasoro mbali mbali ambazo zinahitaji kurekebishwa, lakini hakubaliani na msimamo wa kuvunjwa na kueleza kuwa chama kitasimama mstari mbele kuhakikisha kasoro hizo zinafanyiwa kazi kwa kurekebishwa.

“Pamoja na kuwa hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro tunajua kuwa muungano huu una kasoro lakini una faida nyingi ambazo zinatulazimisha kuendeleza kuulinda na kuuenzi, kwa upande wa vijana tunaamini kuwa kasoro zilizopo zinarekebishika”, alisema.

Jamal alisema kimsingi UVCCM kinakubaliana na suala la kuyaondoa katika orodha ya muungano yale yote yanayaoikwaza Zanzibar katika uchumi ikiwemo masuala la mafuta, ushuru wa forodha na mikopo ya nje.

Katika hatua nyengine wazee wa chama cha Mapinduzi Zanzibar, wamesikitishwa na tabia ya baadhi ya makundi ya vijana wanaopinga muungano na kusababisha vurugu.

Taarifa ya wazee hao iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la wazee Zanzibar, Makame Mzee Suleiman, alisema vipo vikundi vya watu vyenye kupita mitaani juu ya kufanya vurugu kwa kisingizio cha kuukataa muungano.

Alisema njama za kijasusi zinazotumiwa na wasioutaka muungano hazitaifikisha nchi kwenye upatikanaji wa katiba mpya, jambo ambalo linaweza kusababisha vurugu.

“Wazee tunashauri tuache wananchi waingie kwenye mchakato wa katiba watoe maoni yao juu ya katiba hatimaye Tanzania ifikie kwenye lengo tulilolikusudia, tusichafue mazuri tuliyonayo tukajiletea janga”,ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.