Na Haji Nassor, PEMBA
NAIBU Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar, Bihindi Hamad Khamis, amewataka wananchi wa Micheweni, kuviepuka vikundi vinavyopinga zoezi la sensa ya watu na makaazi.
Bihindi alieleza hayo huko Micheweni alipokuwa akizungumza na wazazi na wanafunzi wa vyuo 14 vya kur-an, kwenye mashindano ya kuhifadhi kitabu hicho jimbo la Micheweni yaliyoandaliwa na jumuiya ya kuhiafadhisha kur-an ya jimbo hilo.
Naibu huyo alisema msingi wa kuletwa kwa sensa, ni kutafutwa takwimu ambazo zitalisaidia taifa katika upangaji wa shughuli za maendeleo na kurahisishwa upelekaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema katika siku za hivi karibuni, kumeibuka vikundi ambavyo vinapita katika miji na vijiji, wakiwataka wananchi wasishiriki kwenye zoezi hilo, na kuwataka watu hao wanaoshawishi wapuuzwe.
Alieleza kuwa sensa ya watu na makaazi haina lengo la kujua idadi ya waislamu kama baadhi ya makundi yanavyodai, na badala yake ni kuipa taarifa na idadi halisi serikali ambapo kinyume chake ni kudhoofisha nguvu kazi ya taifa kwa wananchi wake.
“Waislamu wenzangu wa Micheweni na sehemu nyengine, tusikubali kushawishika juu ya kuligomea zoezi hilo, na siku ikifika tuwepo majumbani ili kuhesabiwa na tupeane elimu juu ya umuhimu wa zoezi hilo’’,alisema Bihindi.
Katika hatua nyengine Naibu waziri huyo aliwataka wanawake kuhakikisha wanaendeleza mema waliyokuwa wakiyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kujistiri.
Alisema ni vyema wanawake wakakumbushana na kuelimishana iwapo atajitokeza miongoni mwao ameanza kuyasahau mafundisho na mila za Kizanzibari ambazo zinaendana na maamrisho ya kiislamu.
Kuhusu jumuiya hiyo ya kuhifadhisha kur-an ya Jimbo la Micheweni, ameihakikisha kufuatilia kwa karibu ili iweze kupata usajili na kufanya kazi zake kisheria pamoja na kuweza kupata misaada.
Hata hivyo amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwasimamia watoto wao ili kuendelea kujipatia elimu ambayo ndio mkombozi kwenye maisha yao ya leo na baadae.
Nae Mwakilishi wa Jimbo hilo Subeit Khamis Faki, aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki katika mashindano hayo na kuwataka waongeze juhudi, ili kufikia juzuu hadi 30.
Awali Bihindi pamoja na Mwakilishi waliwakabidhi zawadi mbali mbali wanafunzi walioshiriki, ikiwa ni pamoja na fedha taslimu, misahafu ambapo mwanafunzi Asma Ali Haji aliibuka mshindi wa juzuu 30.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na jumuiya ya kuhifadhisha kur-an ya Jimbo la Micheweni na yameshirikisha madrassa 14 za Jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na Nur Islamia, Juhudiyya, Imaniyya, Nuru Muhammadya pamoja na Taalim atfaliyya.
No comments:
Post a Comment