Yatakiwa iilipe Azam Dola 50,000
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SAKATA la kuuzwa Simba kwa mchezaji Mrisho Ngassa, limechukua sura mpya baada ya klabu ya Azam FC, kutoa nafasi ya pili kwa Yanga, kumrejesha nyota wake huyo wa zamani, kwa kutoa dola za Kimarekani elfu 50 (zaidi ya shilingi milioni 80).
Katika taarifa ya Azam FC iliyotolewa kupitia Meneja wake Patrick Kahemele, klabu hiyo imefafanua kuwa, ilitangaza kuwa biashara ya mchezaji huyo ingefungwa siku ya Jumatano Agosti 8, 2012 saa saba mchana na kuzitaka klabu zinazomtaka mchezaji huyo kufika makao makuu ya Azam zikiwa na pesa taslimu.
Meneja huyo amesema, bei ya mauzo iliyopangwa ilikuwa ni dola 50,000, lakini katika mawasiliano ya e-mail kwa makatibu wakuu wa Simba na Yanga, Azam FC iliweka bayana kuwa ilikuwa tayari kushusha bei hiyo na ingemuuza Ngassa kwa timu ambayo dau lake lingekuwa kubwa zaidi ya mwenzake.
Kwa hivyo alisema, hiyo inaonesha kuwa biashara ya mchezaji huyo ilifanyika kwa uwazi, huku lengo la Azam likiwa ni kutoa haki kwa kila klabu yenye uwezo wa kifedha kuweza kupata huduma ya mchezaji huyo.
Aidha alieleza, Azam inataka ifahamike bayana kuwa mchezaji Mrisho Ngasa alipewa taarifa kuwa anauzwa na aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike makao makuu ya klabu hiyo na kiwango cha fedha atakachotoa.
“Ngassa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam FC itaona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa maslahi yake ya kimkataba kati yake na Azam FC yazingatiwe”, alisema Meneja huyo katika taarifa yake.
Hata hivyo, amedai kuwa hadi kufikia siku Agosti 1, 2012 saa saba mchana, ni klabu ya Simba pekee iliyojibu kwa maandishi na kuonesha nia ya kumchukua Ngassa.
Alieleza kuwa, Yanga haikuwahi kujibu e-mail, ingawa kwa majibu ya simu, mjumbe wake wa kamati ya usajili Seif Magari, alitangaza kuwa Ngassa hana thamani ya zaidi ya milioni 20, na wala haikuwa tayari kuongeza ofa yake.
Amefafanua kuwa muda wa kufungwa kwa biashara ulipofika, ni Simba pekee kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey Ngange Kaburu na Mhasibu wake ndio waliofika wakiwa na pesa taslimu shilingi milioni 25, na kuongeza kuwa, Yanga hawakuonekana na hawakutaka kupokea hata simu walizokuwa wakipigiwa kuulizwa kama wana nia na mchezaji huyo.
Kahemele alisema Azam ilifanya kikao cha dharura na kufikia uamuzi kuwa biashara hiyo imeshindikana kutokana na kutokupatikana kwa mnunuzi mwenye dola 50,000, na kwa hivyo timu hiyo iliamua kumpeleka Simba kwa mkopo.
Alisema, Simba ilipewa sharti la kuhakikisha inamlipa Ngassa mshahara wake kamili, shilingi milioni mbili pamoja na stahiki zake nyengine zote za kimkataba.
Amekanusha kuwa, klabu yake haikumlazimisha Ngassa kwenda Simba kama inavyopotoshwa, na kwamba iwapo nyota huyo anataka kuvunja mkataba wake au Yanga bado wanamuhitaji, wanapaswa kulipa dola 50,000, na Azam itawauzia, ikisema licha ya kupelekwa Simba kwa mkopo, bado Ngassa ni mali ya Azam FC.
No comments:
Post a Comment