Habari za Punde

…Ashitaki TFF kwa kutoshirikishwa

Na Aidan Charlie, Dar es Salaam
KATIKA hali inayoonesha kizungumkuti, mchezaji Mrisho Ngassa, amesema hatambui kwamba ameuzwa, kwa kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka kwa klabu yake ya Azam juu ya hatua hiyo.

Amedai kuwa, taarifa hizo amezisikia na kusoma kwenye mitandao tafauti, lakini muajiri wake bado hajampa taarifa rasmi juu ya suala hilo.

Aidha amedai kuwa, hadhani kuwa utaratibu huo ni sahihi, akihoji vipi Azam imeweza kumuuza kwa timu nyengine bila ya kumhusisha, na namna maslahi yake yatakavyoangaliwa na kusimamiwa katika timu nyengine.

“Nashindwa kuamini kama Azam watakuwa wamefanya hivyo. Ilipaswa wanipe taarifa kwamba wananiuza kwani nina haki ya kuchagua, ama kukubali au kukataa”, alieleza.

Amefahamisha kuwa, hataki kuondoka Azam huku kukiwa kuna hali ya kutokuelewana kati yake na timu hiyo, pamoja na wapenzi wa klabu ambao amesema wamekuwa wakimsapoti kwenye kipindi chote alichokuwepo hapo.

“Waweza kujiuliza kwa nini mpaka leo mashabiki wa Yanga wanaonesha mapenzi kwangu au ninakuwa na ukaribu nao, ni kwa sababu wakati naondoka Yanga nilipewa baraka zote na klabu yangu, yaani niliondoka vizuri”, alibainisha mshambuliaji huyo.

Amehoji iweje Azam ilipomtaka ilikwenda Yanga na wakakubaliana juu ya ada ya uhamisho naye akapewa taarifa kabla kukubaliana na timu hiyo, lakini yenyewe imeshindwa kufuata utaratibu ule ule.

Kutokana na hali hiyo, Ngassa ameripotiwa kupeleka malalamiko yake katika Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, kutaka haki itendeke juu ya mustakbali wake na hatua hiyo ya Azam FC kumuuza bila ridhaa yake.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.