Habari za Punde

BANC ABC yazigonganisha Duma, Mtende Rangers. Duma yapanda ngazi TFF kudai haki

Na Masanja Mabula, Pemba
KLABU ya soka ya Duma, inakusudia kukata rufaa katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupinga uamuzi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), wa kuiengua kushiriki michuano ya BANC ABC Super 8 na badala yake nafasi hiyo kupewa timu ya Mtende Rangers.

Katibu wa Duma inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kisiwani Pemba Salim Abdallah, ameliambia gazeti hili kuwa, hatua hiyo inalenga kuitaka ZFA itende haki kwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na TFF juu ya timu zinazostahili kucheza michuano hiyo.

Amesema kitendo cha ZFA kuiteua Mtende Rangers kucheza mashindano hayo, kinainyima haki timu yake ambayo alidai ndiyo inayostahili kuwa miongoni mwa timu zitakazomenyana katika kinyang’anyiro hicho kutokana na kufanya vizuri kwenye ligi ya daraja la kwanza Taifa Pemba.

"Tunashangaa kwa uamuzi wa ZFA kuiteua timu ya Mtende Rangers kushiriki michuano ya Super 8 wakati kwa mujibu wa TFF, Duma ndiyo yenye haki hiyo. Tunajiandaa kupeleka rufaa yetu TFF ili tupewe haki yetu hiyo”, alisema Katibu huyo.

Aidha, alieleza kuwa, kutolewa kwa timu yake kwenye patashika hiyo, kunawavunja moyo wachezaji wake ambao walikuwa wameanza mazoezi kujiandaa na ligi hiyo, na kuongeza kuwa, hali hiyo huenda ikawaathiri kisaikolojia wachezaji wake.

Alisema, uamuzi wa timu hiyo kupiga hodi TFF, umelenga zaidi katika kutetea maslahi ya timu, na kuzitaka klabu nyengine kuunga mkono hatua hiyo ya Duma, kwani vitendo kama hivyo vinaweza kutokea kwa klabu yoyote.

"TFF imesema wazi kuwa timu zilizoshika nafasi za juu kwenye ligi kuu ndizo zitakazoshiriki michuano hiyo, zikiungana na timu moja iliyofanya vizuri katika ligi daraja la kwanza Taifa, kwa hali hiyo Duma ndiyo yenye haki na sio Mtende Rangers", alifahamisha.

Katika msimamo wa ligi daraja la kwanza Taifa Pemba msimu uliopita, Duma ilicheza mechi 26 na kushinda 22, ikapoteza michezo mitatu na kutoka sare moja, ikimaliza ikiwa na pointi 67.

Nayo Mtende Rangers ilimaliza ligi hiyo Unguja ikiwa imekusanya pointi 45.
Mapema, Katibu Mkuu wa ZFA Kassim Haji Salum, alikaririwa akisema uamuzi wa kuiteua Mtende Rangers kushiriki michuano hiyo, unalenga kuweka uwiano wa kila upande kati ya Unguja na Pemba, kutoa timu mbili.

NAYE AMEIR KHALID anaripoti kuwa, timu ya Mtende Rangers imeanza maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 8, mwaka huu katika viwanja vinne tafauti.



Msemaji mkuu wa timu hiyo Ibrahim Karaby, amesema, wao hawaumizi kichwa na suala la timu ipi ishiriki, bali huo ni uamuzi wa ZFA, ambao anaamini ni sahihi.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.