Habari za Punde

Balozi wa Cuba aagana na Rais wa Zanzibar baada ya kumaliza muda wake

 Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekitiw a Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amezipongeza juhudi za Serikali ya Cuba za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria ikiwa ni pamoja na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.

Dk. Shein aliyasema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Mhe. Ernesto Gomez aliyafika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini akiiwakilisha nchi yake ya Cuba ambayo ni rafiki wa Tanzania kwa muda mrefu.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa mashirikiano yaliopo katika sekta ya afya ambayo yamepelekea kuanzishwa mafunzo maalum ya udaktari hapa nchini yanayosimamiawa na wakufunzi kutoka nchi hiyo kukamilika kwake kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma kwa jamii pamoja na kuimarisha zaidi sekta hiyo ya afya.

Alisema kuwa kutokana na kuanzishwa kwa programu hiyo maalum ya kuwasomesha vijana wa Kizanzibari fani hiyo hapa hapa nchini chini ya wakufunzo kutoka Cuba kutaimarisha sekta hiyo ya afya pamoja na kupanua wigo katika sekta za maendeleo kutoka nchini humo ikiwemo sekta hiyo ya afya.


Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kutimiza ile azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuanzisha kitivo cha Udaktari katika chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambapo mchakato wake unaendelea huku serikali ikiliwekea kipaumbele suala hilo kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii.

Mbali na mashirikiano hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Gomez kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza pamoja na kuzidisha ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii ambayo nchi hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa na kueleza haja ya kuwepo mashirikiano kama ilivyo kwa sekta ya afya hivi sasa.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Cuba imepata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ya utalii hasa katika ukanda wake wake maarufu wa utalii ambao una vivutio kadhaa zikiwemo hoteli za kisasa ni hatua moja wapo ya kuweza kushirikiana pamoja ili Zanzibar nayo iweze kupata mafanikio kama hayo.

Kwa upande wa sekta ya uvuvi, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Cuba imepata manikio makubwa katika sekta hiyo hivyo Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wake wa pamoja na nchi hiyo kwa lengo la kukuza sekta hiyo nchini.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuhakikisha sekta hiyo inapata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuwashajiisha wavuvi kutumia uvuvi uhusika pam oja na kuweka mikakati maalum ya kuweza kuvua uvuvi wa bahari kuu ambao ndio wenye faida na kipato kikubwa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwakarishisha wawekezaji kutoka Cuba kuja kuekeza Zanzibar kutokana na kuwepo fursa kadhaa za uwekezaji.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa juhudi zinazochukuliwa na Cuba katika kuhakikisha mashirikiano makubwa yanakuwepo juu ya sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar na kusisitiza haja ya kuendelea.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwapongeza viongozi wa nchi hiyo akiwemo muasisi wake na Mwanamapinduzi Rais Fidel Castro pamoja na Rais Raul Castro kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano mwema na Zanzibar huku akizipongeza juhudi na mikakati inayochukuliwa na nchi hiyo katika kuimarisha uchumi wake.

Nae Balozi wa Cuba nchini Tanzania , Mhe. Ernesto Gomez alimueleza Dk. Shein kuwa programu ya kuwafundisha madaktari wazalendo ambayo inasimamiwa na madaktari bingwa kutoka Cuba itazalisha madaktari wengi hapa nchini na itakuwa ya mafanikio.

Alisema kuwa ana matumaini makubwa programu hiyo ambayo ina mwaka wa tano hivi sasa iaweza kutoa madaktari wazuri hapa nchini kwa vile imekuwa ikitolewa kwa vijana kutoka Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ambayo hatimae vijana hao watakwenda kuyamalizia nchini Cuba katika chuo kikuu cha Matanzas yana malengo madhubuti katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini

Balozi hayo pia, alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuwapa mafunzo madaktari wazalendo kwa kuendelea kutoa mafunzo ya ndani ya nchi na hata nchini Cuba.

Aidha, Balozi Comez alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaengeza nafasi za masomo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatua ambayo pia itainufaisha Zanzibar kwa kuweza kupata fursa hizo za masomo mbali mbali nchini humo.

Pamoja na hayo, Baloz Comez alimuahidi Dk. Shein kuwa nchi yake iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya na sekta nyenginezo kama vile sekta ya utalii, uvuvi na vyenginezo.

Akitoa shukurani zake kwa Zanzibar, Balozi huyo alitoa pongezi kwa wananchi na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mashirikiano yao makubwa waliyompa wakati akifanya kazi zake hapa nchini na kuusifu ukarimu wa Wazanzibar huku akipongeza mashirikiano wanayopata madaktari kutoka Cuba wanaofanya kazi zao za kutoa huduma za afya hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.