Na Ameir Khalid
CHAMA cha CUF kimeelezea nia yake ya kwenda mahakamani kupinga matokeo ya
uchaguzi mdogo ya Uwakilishi jimbo la Bububu, yaliyompa ushindi mgombea wa
chama cha Mapinduzi, Hussein Ibrahim Makungu (Bhaa).
Viongozi wa chama hicho wamesema hawakubaliani na
matokeo ya uchaguzi huo kwa kile wanachodai kuwa haukuwa huru na ulikuwa na ubabaishaji
mkubwa na wamepanga kwenda mahakamani katika muda wa siku 14.
Akizugumza na waandishi wa habari makao makuu ya
CUF Mtendeni Zanzibar, Mbunge wa jimbo la Mtoni, Haji Faki Makame, alisema licha
ya tume kutangaza matokeo, kamwe hawakubaliani
nayo kwa sababu ilikibeba CCM.
“Kila mmoja alishuhudia ni nani ambae atakubaliana
na matokeo yale wakati wenzetu walifanya kila hila ili kuhakikisha wanashinda,
hivyo sisi CUF tunasema kuwa hatukubaliani na matokeo yale na hivi sasa
tunajiandaa kwenda mahakamani kukata rufaa
ndani vya siku 14,”alisema.
Alisema jopo la wanasheria wa chama hicho linafanaya
mipango kuwasilisha pingamizi hilo
mahakamani.
Hivyo alisema mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote na
wanasheria wao kukamilisha kila kitu watakutana na waandishi wa habari ili
kuweza kutoa tamko rasmi la siku ambayo watakwenda mahakani, kuwasilisha
pingamizi yao.
Mbunge huyo
moja kwa moja alielekeza lawama zake kwa Tume ya Uchaguzi kwa madai kuwa kwa
kiasi kikubwa ndiyo iliyohusika kuvuruga
uchaguzi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Haki za Binadamu,
Habari na Uenezi wa chama hicho, Salum Bimani, alisema CUF kilifanya maridhiano ya kitaifa kwa lengo
la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaondokana na machafuko yanayohusiana na masuala
ya uchaguzi, lakini bado inaonekana kuwa wengine hawakubaliani na jambo hilo.
Aliongeza chama chao kitahakikisha kuwa kinailinda
serikali ya umoja ya kitaifa kwa nguvu
zote, licha ya dalili ambazo zimeonyeshwa na vyama vyengine kutokuwa tayari
kuisimamia serikali hiyo.
No comments:
Post a Comment