Na Husna Mohammed
WANANCHI wametakiwa kujali maslahi ya nchi kwanza na baadae chama, kwa
lengo la kuweka mustakabali mzuri wa nchi.
Hayo aliyasemwa jana na mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo, wakati
akizungumza katika mjadala kwa vyombo vya habari kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
uliofanyika hoteli ya Mazsons Mjini Zanzibar.
Alisema wananchi na hata baadhi ya viongozi wamekuwa wakinasibisha
muungano na chama jambo ambalo wamekuwa wakiwapotosha wananchi kujua ukweli wa
mambo na hivyo kuwakosesha fursa muhimu ya kudai maslahi ya nchi yao.
Alifahamisha kuwa yeye kama muasisi wa muungano hakubaliani na uamuzi
huo na kwamba iko kila sababu ya kudai maslahi ya Zanzibar pamoja na watu wake hasa
ikizingatiwa kuwa makubaliano ya muungano hayako kisheria.
"Mimi nitakuwa miongoni mwa watu watakaoulizwa kesho mbele ya
Mungu kuhusiana na mstakbali wa nchi hii kwa nini najua ukweli nisiwaeleze
wasioujua, huu ni ukweli halisi na mimi kama muasisi nabeba dhima hii mpaka
mbele ya Mungu," alisema.
Sambamba na hilo
lakini muasisi huyo alisema ukiangalia kiundani muungano huo umetawaliwa
na udugu zaidi kwa kuwa si wa kikatiba
wala kisheria.
"Tangu mwanzo muungano huu hauna mambo mazuri kwa nini tunapohoji
katika mambo muhimu yamekuwa hayatekelezwi labda kwa kuwa hauko kisheria wala
kikatiba, sheria ya Zanzibar hakuna kitu kinachozungumzia muungano, pia mawazo
ya muungano hayakuzungumzwa katika baraza la Mapinduzi wakati huo, wakati
umefika sasa kufanya mabadiliko kwa maslahi ya nchi yetu na vizazi vyetu,"
alisema.
"Kuna sehemu alitakiwa Mzee Karume kutia saini lakini hakuweka
saini hiyo na sisi wakati huo tulikwenda Tanganyika kudai baadhi ya mambo
hayati Nyerere alisema bado wakati wake, sasa wakati umefika vijana kudai ……
tumieni mwanya wa katiba mpya," alisisitiza.
Akijibu suala aliloulizwa kuhusu kurudisha kadi au kujitoa katika chama
cha Mapinduzi, Mzee Moyo, alisema yeye hawezi kufanya hivyo, na hakuna mtu wa
kumlazimisha kurejesha kadi ya chama hicho.
"Kwa taarifa yenu mimi ni mwanachama halisi mwenye kadi nambari 7
ya chama hivyo hakuna mtu yoyote atakaenihoji kurejesha kadi yangu kwa
kuzungumzia maslahi ya nchi yangu," alisema.
"Wazanzibari Muungano wanautaka lakini ni lazima kufanywe
mabadiliko na hivyo wanavyosema uamsho mara nani hataki muungano hiyo ni
kuwapotosha wasiojua nasema hivyo kwa maslahi ya nchi yangu," alisisitiza.
Nae Profesa Abdul Sharif, akiwasilisha mada juu ya wajibu wa dhima ya
vyombo vya habari katika kuripoti habari za Muungano, alionesha wasiwasi wake
kwa mambo yatakayofikiwa katika katiba mpya kama yatakubaliwa sambamba na
kutekelezwa kwa maoni ya watu wa Zanzibar.
Sambamba na hilo pia alisema kuna
uwezekano wa kutopatikana majibu muafaka kutokana na baadhi ya wananchi
kutokuwa na uelewa kueleza bayana juu ya maslahi ya Zanzibar katika mchakato wa kutoa maoni ya
katiba mpya.
Akizungumzia kuhusu mambo ya kisheria yanayopitishwa bungeni, Profesa
Sharif, alisema mambo mengi yanayopitishwa kisheria bungeni yamekuwa
yakiwanyima fursa wabunge wa Zanzibar kwa kuwa wao ni asilimia 20 na Tanzania Bara
ni asilimia 80, hivyo uwakilishi wa kuamua mambo unakuwa ni mkubwa kwao.
"Hata kama watakataa wabunge kutoka Zanzibar basi si kitu kwa
kuwa utaratibu umeonesha hivyo sheria ya bunge inahitaji marekebisho kwa kuwa
mambo mengi yamekuwa yakifanyika kwa maslahi yao," alisema.
Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
Zanzibar, alisema kimsingi mambo yaliyokuwepo sasa ni vichekesho kwa kuwa
hakuna uthibitisho wa mambo ya muungano hasa ukizingatiwa kuwa hakuna katika
katiba wala sheria.
Alisema Mwanasheria wa mwanzo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
hakupewa nafasi yake ya kuweza kuhoji mambo ya muungano, hivyo dhana ya mambo
matatu muhimu katika muungano hayapo tena ikiwa ni kwa Serikali ya Zanzibar, Tanganyika na
Serikali ya Muungano.
"Kwa kuwa mkataba ni jambo la hiyari baina ya pande zote mbili hivyo
ni lazima kukubaliana na kuridhiana baina ya pande hizo, kutokana na hilo dhima
ya Zanzibar ikishindikana ni kupigwa kura ya maoni," alisema.
Nae mwandishi wa habari wa siku nyingi Enzi Talib Aboud, alisema
Baraza la Mapinduzi limeshakaa mara mbili kutaka kufanyiwa kazi baadhi ya mambo
muhimu lakini upande mmoja unashindwa kutekeleza.
Enzi aliwataka waandishi wa habari kuijua historia ya Zanzibar hasa kwa masuala ya muungano jambo
ambalo litawawezesha kuhoji na kuuliza kuhusu mambo muhimu ya Zanziba na watu
wake.
Mapema Ofisa Mipango wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ofisi ya
Zanzibar, Shifaa Said Hassan, alisema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa
kuwaelimisha wananchi juu ya muungano.
Alisema lengo la mjadala huo ni kuona kuwa vyombo vya habari vinafanya
wajibu wake katika kuzungumzia muungano kwa umma, hasa kwa kuwa mijadala kama hiyo imekuwa ikizungumzwa siku zote.
Mjadala huo
umetayarishwa na Baraza la Habari Tanzania, ofisi ya Zanzibar ambapo uliwakutanisha waandishi wa
habari wa vyombo mbali mbali pamoja na wadau kutoka sekta ya serikali na
binafsi.
No comments:
Post a Comment