Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akifuatana na Balozi wa India nchini Tanzania Debnath Shaw alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,kujitambulisha kwa Rais leo.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi wa India nchini Tanzania Debnath Shaw alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,kujitambulisha kwa Rais leo.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya India na Zanzibar unahitaji kuimarishwa zaidi kutokana na mafanikio makubwa yaliopatika kwa pande zote mbili.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa nchini Tanzania Mhe. Debnath Shaw, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi mbili hizo ambao uhusiano huo umeweza kuimarika na kuleta manufaa ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika sekta kadhaa za maendeleo.
Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya elimu, India imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza fani mbali mbali ikiwa nji pamoja na kusaidia kutoa nafasi za masomo ya muda mrefu na mfupi kwa Zanzibar.
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuwepo kwa mashirikiano kwa Taasisi za elimu ya juu hasa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), na vyuo vikuu vya India na Taasisi nyengine za elimu nchini humo kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu pamoja na kuweza kubadilishana uzoezi wa kitaalamu.
Alisema kuwa hatua hiyo itapelekea kubadilishana uzoefu baina ya pande mbili hizo kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu hasa kwa upande wa vyuo vikuu.
Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dk. Shein alipongeza hatua zilizofikiwa na India katika sekta hiyo na kueleza kuwa iwapo nchi hiyo itaiunga mkono Zanzibar hatua hiyo itaisaidia sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kufikia lengo lake ililokusudia katika kufanikisha kwa mradi wa kuimarisha mawasiliano serikalini kwa kupitia mradi unaoendelea hivi sasa wa Mkonga wa Taifa (E-Government).
Dk. Shein aliishukuru na kutoa pongezi kwa serikali ya India kwa kuendelea kupokea wagonjwa wengi wa rufaa kutoka Zanzibar na kusisitiza haja ya nchi hiyo kushirikiana na Zanzibar ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekenwa nchini humo kwa kusaidia kuleta wataalamu wake pamoja na kuwapa mafunzo wataalamu wazalendo.
Aidha, Dk. Shein alieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
Pia, Dk. Shein alimueleza Balozi Shaw kuwa ipo haja kwa Ubalozi wa nchi hiyo uliopo hapa Tanzania kuendelea kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na Zanzibar kuwa na vivutio vingi pamoja na kushabihiana kiutamaduni.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza kuwa, wataalamu kutoka Zanzibar wanatarajiwa kukutana na Balozi huyo hivi karibuni, hivyo katika mkutano wao masuala kadhaa yatazungumzwa yakiwemo ujenzi wa baadhi ya barabara za Unguja na Pemba, mradi wa kudhibiti maji machafu na ujenzi wa mitaro, mradi wa uimarishaji wa huduma za afya pamoja na kufufua mradi wa Maeneo huru ya Kiuchumi Zanzibar.
Nae Balozi Shaw alitoa shukurani wka Dk. Shein kwa mapokezi yake aliyoyapata ikiwa ni mara yake ya mwanzo kufika Zanzibar na kumuhakikishia kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar pamoja na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo.
Aidha, Balozi huyo mpya wa India nchini Tanzania, alimueleza Dk. Shein kuwa kwa upande wa sekta ya elimu nchi yake itaendelea kutoa nafasi za masomo mbali mbali kwa Zanzibar pamoja na kutoa nafasi maalum kwa wafanyakazi wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Balozi huyo alieleza kuwa Tanzania imekuwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofaidika zaidi kutokana na nafasi za masomo zinazotolewa na Serikali ya India ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili waendelee kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Pamoja na hayo, Balozi huyo aliyaunga mkono maelezo ya Dk. Shein katika kukuza na kuendeleza mashirikiano katika sekta mbali mbali pamoja na miradi ya maendeleo huku akipongeza kwa kufurahishwa kwake na hali ya Zanzibar ya kuona watu wenye asili mbali mbali wamekuwa wakiishi pamoja na amani na utulivu mkubwa na kuwa na mashirikiano yasio na mfano
No comments:
Post a Comment