Habari za Punde

Duma yalia na mwamuzi


Na Haji Nassor, Pemba

BAADA ya kupoteza mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu ya soka Zanzibar kwa kuchapwa magoli 2-0 na Jamhuri, klabu ya Duma imemgeukia mwamuzi wa pambano hilo Ali Omar Kisaka, ikidai aliwapa wapinzani wao penelti kwa kushawishika na zogo la mashabiki.
 
Kocha wa wajenga uchumi hao Asaa Khamis, amesema katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Gombani, penelti ya kwanza haikuwa sahihi, na kwamba hakufikiria kama mwamuzi engelishawishika na kelele za mashabiki wa Jamhuri hasa kwa vile alikuwa mbali na eneo lililotokezea kadhia hiyo, ingawa baadae aliamuru ipigwe penelti.
 
Hata hivyo, alisema kwa ujumla mchezo huo haukuwa mbaya kwa upande wa wachezaji wake hasa kwa vile ni wageni kwenye michuano hiyo pamoja na baadhi yao kuwa ni wapya nab ado hawajazoeana vya kutosha.
 
“Mchezo haukuwa mbaya, lakini nashangaa kuona mwamuzi kwanza alikuwa mbali, kisha alishangaa kidogo kutoa uamuzi, lakini baada ya zogo na kelele nyingi za wapenzi wa Jamhuri, aliamua kuizawadia penelti, na kila  anayefahamu sheria za soka, aliona mwamuzi ameboronga”, alifafanua kocha huyo.
 
Hata hivyo, alisema amekubali matokeo hayo na kuahidi kufanya vyema kwenye michezo ijayo, huku akiwataka wapenzi wao kujitokeza kwa wingi ili kuwapa nguvu wachezaji kila timu hiyo itakaposhuka dimbani.
 
Kwa upande wake, kocha wa klabu ya Jamhuri Ameir Machano ‘Chua’, alikiri kuwa Duma sio timu ya kubeza licha ya timu yake kushinda, na kusema vijana hao wanacheza kwa nguvu dakika zote za mchezo, ingawa baadae walichoka na kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
 
Wakitupa karata yao ya kwanza katika ngarambe za ligi kuu msimu wa 2012/13 inayodhaminiwa na kampuni ya TBL kupitia kinywaji cha Grand Malt, maafande wa Duma walikubali kichapo cha magoli 2-0 mbele ya Jamhuri, huku mabao yote hayo yakifungwa kwa njia ya penelti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.