Habari za Punde

Kocha Azam awashukia waamuzi

 
Na Mahmoud Zubeiry
 
BAADA ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 mikononi mwa Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii juzi, Kocha Mkuu wa Azam FC Boris Bunjak, amewatupia lawama waamuzi wa mechi hiyo, kwa kudai kuwa waliwapa mbeleko wapinzani wao.
 
Mchezo huo uliopigwa uwanja wa Taifa jjini Dar es Salaam, ulichezeshwa na Martin Sanya, aliyeisaidiwa na Omar Kambangwa na Ephron Ndissa, ambapo mwamuzi wa akiba alikuwa Oden Mbaga na Kamisaa Omary Kasinde.
 
Bunjak, aliiambia BIN ZUBEIRY  baada ya mechi hiyo, kuwa waamuzi hao walionesha mapungufu makubwa kwa kuwapendelea wazi wazi Simba na hata wakafanikiwa kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
 
“Nafikiri tulicheza vizuri, tukaongoza 2-0, baada ya hapo tukapoteza nafasi nzuri za kufunga, lakini siamini kwa nini refa alitoa penalti dakika ya mwisho (kipindi cha kwanza), kwa sababu ule mpira ulikuwa kwenye himaya ya wachezaji watatu kutoka nyuma, unaweza kuonaje nani aliucheza kwa mkono”, alihoji kwa mshangao.
 
Mserbia huyo pia alisema hata bao la pili walilofungwa lilikuwa kwa msaada mkubwa wa waamuzi, huku akidai kuwa aliiandaa timu yake kucheza dhidi ya wachezaji 10, na siyo zaidi.
 
“Mimi si kocha ninayeandaa timu kucheza dhidi ya wachezaji wengi, naweza kufanya nini? Tulicheza vizuri, tulipoteza nafasi, refa alitunyima penalti mbili, asilimia 100, nifanye nini, labda hii ni soka ya Tanzania tu”, alisema Mserbia huyo.
 
Alieleza kuwa hakuwa la kufanya zaidi, huo ukiwa ni uzoefu wake wa kwanza ofisini, lakini alidaki kushangazwa sana, kwamba Simba ni timu kubwa na nzuri, lakini Azam ilicheza vizuri na ilistahili kushinda taji hilo.
Kocha huyo alionesha kuridhishwa na bao moja tu la Simba, huku la tatu akisita kulizungumzia kabisa katika malalamiko yake.
 
Katika pambano hilo, Azam iliiruhusu Simba kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2, hivyo kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.