Na Mwandishi Wetu, Pemba
MATARAJIO ya wadau wa soka wa Zanzibar kupumua baada ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kupata Rais mpya, yameanza kuingia doa kutokana na kuwepo dalili za mvutano mpya unaoelekea kuchipua.
Hali hiyo imebainika baada ya Kamati Tendaji ya chama hicho kisiwani Pemba, kudai kuwa haishirikishwi na wenzao wa Unguja, wakiwalaumu kwa kuchukua maamuzi mazito na ya kitaifa peke yao.
Kamati hiyo ya Pemba, ilifanya kikao Septemba 11 kujadili utendaji dhaifu unaofanywa na Kamati Tendaji ya ZFA Taifa ya Unguja, na kutoa azimio la kutoyatambua maamuzi yote yaliyochukuliwa na kamati hiyo hivi karibuni.
Maamuzi hayo yamepelekwa kwa Kaimu Rais wa ZFA Haji Ameir Haji, na Zanzibar Leo kupata nakala yake.
Barua hiyo yenye nambari ya kumbukumbu ZFA/T/M/KK/J/Q/VOL. II.P230 iliyosaidiwa na Kaimu Msaidizi Katibu Abdallah Suleman Sharif, imesema kuwa, kamati hiyo ya ZFA Pemba, imeona inabebeshwa lawama kwa maamuzi ambayo ni ya watu wachache bila yenyewe kuhusishwa.
Ikielezea baadhi ya maamuzi hayo, imesema ni pamoja na kumsimamisha Katibu Mkuu, kubadilisha kanuni ya mashindano upande mmoja jambo lilidaiwa kuathiri mapato ya upande mmoja na kuonekana kwamba kuna kanuni mbili za ligi daraja la kwanza na la pili Taifa.
Aidha, kamati ya Unguja imeelezewa kwenye barua hiyo kuwa imekuwa ikifanya dharau kwa viongozi wa juu wa ZFA Taifa Pemba, kiasi ya kuonekana hawana mamlaka ya maamuzi kutoka ZFA, jambo walilosema linaonesha kuthamini upande mmoja tu wa ZFA.
Jengine ambalo kamati hiyo imelilalamikia, ni kamati ya Unguja kujibu barua ya Waziri anayeshughulikia michezo bila kujali wadhifa wake wala kuishirikisha ZFA Taifa Pemba.
Kwa hivyo, kamati tendaji hiyo ya ZFA Pemba, imesisitiza kuwa haiyatambui maazimio yanayo na yatakayoendelea kutokea kwa upande mmoja kama haikushirikishwa.
Nakala za barua hiyo, zimepelekwa pia kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo, Katibu Mkuu (W.H.U.U.M), Katibu BTMZ na Afisa Mdhamini (W.H.U.U.M-Pemba).
Hata hivyo katika udadisi wa gazeti hili kwa mmoja wa wajumbe wa kamati tendaji ya ZFA Unguja, liliarifiwa kuwa leo wajumbe hao wanatarajiwa kwenda kisiwani Pemba, kuhudhuria kikao kilichoandaliwa na wenzao wa huko, ingawa alisema hafahamu nini ajenda ya mkutano huo.
No comments:
Post a Comment