Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na msaidizi Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani (mambo ya Afrika) John Carlson mara tu baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika ofisi za Wizara hiyo mjini Washington.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na viongozi wa shirika la USAID mjini Washington. Kushoto ni balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mwanaidi Maajar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na badhi ya viongozi wa shirika la USAID mjini Washington
(Picha na, Mpiga picha maalum USA). Imewekwa na Hassan Hamad kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Na Mwandishi Maalum Washington
Makamu wa Kwanza wa Rais amekutana na msaidizi Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bwana John Carlson katika jengo la Wizara hiyo mjini Washington, kuzungumzia juu hali ya demokrasia na siasa za Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Maalim Seif alimueleza kiongozi huyo juu mwelekeo wa utoaji wa maoni ya katiba mpya ya Tanzania kwa upande wa Zanzibar, kwamba wananchi wamekuwa wakitoa maoni yao kwa uhuru licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo.
Amesema wananchi wengi wa Zanzibar wamekuwa na mwamko tofauti, huku wengine wakitetea muundo wa muungano wa serikali mbili kama ilivyo sasa na wengine wakitetea muungano wa mkataba ambao utaiwezesha Zanzibar kuwa na mamlaka kamili na kutambuliwa kimataifa.
Makamu wa Kwanza wa Rais pia amemueleza kiongozi huyo juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana Zanzibar tangu kuundwa kwa serikali yenye mfumo wa umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake, kiongozi huyo wa Marekani ameisifu Zanzibar kwa jitihada zake za kuimarisha demokrasia na kuwaletea maendeleo watu wake na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha demokrasia na kuleta maendeleo kwa Wazanzibari.
Maalim Seif yuko mjini Washington DC baada ya kumaliza ziara yake katika mji wa North Carolina.
Wakati huo huo Shirika la misaada la Marekani USAID limeahidi kuendeleza misaada yake kwa Zanzibar katika maeneo tofauti yakiwemo kilimo cha umwagiliaji pamoja na maktaba za vitabu katika wilaya za Unguja na Pemba.
Naibu kiongozi wa shirika hilo bibi Linda Atim, ametoa ahadi hiyo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ofisi za Wizara ya mambo ya nje ya Marekani mjini Washington.
Bibi Linda mwenye jukumu la kushughulikia masuala ya Sudan ya kusini na kaskazini pamoja na Afrika Mashariki, amesema shirika hilo limeridhishwa na matumizi mazuri ya misaada yake inayoitoa kwa Zanzibar, na kuahidi kuyafanyia kazi maombi yaliyotolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa shirika hilo.
Katika mazungumzo yake na uongozi wa shirika hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amelishukuru shirika la USAID la Marekani kwa misaada yake kwa Zanzibar, na kuliomba kuongeza misaada yake katika maeneo mengine likiwemo kuisaidia Zanzibar kuweza kujitosheleza kwa chakula kupitia mradi wake wa Feed the Future.
Pia ameliomba shirika hilo kufikiria namna ya kuisaidia Zanzibar katika kilimo cha umwagiliaji kwa ekari elfu sita ambazo hazijaanza kutumika kwa kilimo hicho
Maeneo mengine waliyojadiliana ni pamoja na uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika kuongeza uwezo wa wake wa kuhifadhi chakula, pamoja na kutanua wigo wa teknologia ya habari katika skuli za Zanzibar.
Marekani imekuwa ikisaidia miradi mbali mbali ya maendeleo kwa Zanzibar ikiwemo mradi wa kutokomeza malaria ambao upata mafanikio makubwa, mradi wa vitabu maskulini, miradi ya ujenzi wa barabara pamoja na mradi wa njia ya Umeme kutoka Dar es Salaamu hadi Zanzibar.
Pia Makamu wa Kwanza wa Rais amepata fursa ya kutembelea kitengo cha kupambana na majanga katika Makao Makuu ya Serikali ya Marekani ambapo alijionea jinsi serikali ya nchi hiyo ilivyojidhatiti katika kupambana na majanga pamoja na vitisho vya aina yoyote kutoka ndani na nje ya nchi.
Maalim Seif amesema miongoni mwa mambo ambayo Zanzibar inaweza kujifunza ni namna serikali inavyoweza kujipanga kabla ya kutokea kwa majanga, pamoja na kuwa na njia maalum za uokozi wakati majanga yanapotokea.
No comments:
Post a Comment