Habari za Punde

Super Falcon, KMKM zajikosha


Na Haji Nassor, Pemba
BAADA ya kuanza michuano ya ligi kuu ya soka Zanzibar msimu wa mwaka 2012.13 kwa kuchapwa mabao 2-0 na Chipukizi, mabingwa watetezi Super Falcon, wamesema bado ni mapema kuhukumiwa kwa kipigo hicho.

Kocha msaidizi wa klabu hiyo Suleiman Saleh, amewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kutulia na kutokuwa na wasiwasi kwani bado safari ni ndefu na chochote kinaweza kutokea.

Akitoa tathmini ya mchezo huo, alisema timu yake haikuwa imezidiwa, bali kilichojitokeza ni kwa wapinzani wao kuwahi kutumia nafasi chache walizozipata kuandika magoli hayo.

“Wachezaji wetu walicheza vizuri, na timu yetu kwa ujumla ni nzuri, hatuna shaka yoyote kwamba tutaweza kutetea ubingwa tuliotwaa msimu uliopita”, aliwatoa wasiwasi wapenzi wa timu hiyo.

NAYE MWAJUMA JUMA, amemkariri Kocha Mkuu wa timu ya KMKM Ali Bushiri, akisema kuwa pamoja na kufungwa timu bao 1-0 na Mafunzo katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo, bado ana imani kikosi chake kitafanya vizuri katika michezo inayofuata.

Akizungumza mara baada ya kumaliza mchezo kati ya timu hizo uliopigwa juzi uwanja wa Amaan, kocha huyo alisema ameridhika sana na kiwango cha wachezaji wake, na makosa aliyoyaona katika mechi hiyo atayafanyia marekebisho.

“Vijana wangu walionesha soka safi ingawa walikosa magoli mengi, lakini nina imani mechi ijayo tutaekebisha kasoro hizo na kushinda”, alijipa moyo mlinda mlango huyo mstaafu wa kimataifa.

Hata hivyo, alisema akiwa kocha, hakuridhika na kitendo cha wachezaji Sadik Habib na Aziz Shaweji kwa kitendo chao cha kupigana uwanjani na kusababisha mwamuzi Makame Chirau kuwatoa nje kwa kadi nyekundu.

Katika mechi zao zijazo Septemba 15, Super Falcon itaivaa Duma huko Gombani, wakati KMKM itajaribu bahati yake mbele ya Malindi katika uwanja wa Amaan.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.