Na Haji Nassor, PembaMABINGWA wa soka Zanzibar timu ya Super Falcon, jana walianza vibaya kampeni za kutetea taji lao, baada ya kusalimu amri mbele ya Chipukizi kwa kuchapwa mabao 2-0.
Katika mchezo huo wa kufungua msimu uliofanyika uwanja wa Gombani, Chipukizi ilionesha dhamira ya kutoka na ushindi kwa kutandaza kabumbu safi lililowavutia mashabiki waliojazana uwanjani.
Hata hivyo, ushindi huo haukuwa rahisi kupatikana, kwani wanaume hao walibanana vyema na kwenda mapumziko wakiwa hawajafungana.
Kilipoanza kipindi cha pili, iliwachukua Chipukizi dakika 25 kuzifumania nyavu, kwa bao la Abdulhakim Ali, alilofunga katika dakika ya 70.
Huku Super Falcon ikihaha kutafuta bao la kusawazisha, nyavu zake zikachanwa tena katika dakika ya 88, mara hii likifungwa na Faki Mwalimu.
Mwamuzi Ramadhan Ibada Kibo aliyepuliza kipyenga katika mtanange huo, alilimudu vyema pambano hilo ambapo mashabiki waliohojiwa walieleza kuridhishwa na kiwango cha uamuzi.
NAYEAMEIR KHALID, anaripoti kutoka uwanja wa Amaan kuwa, Mafunzo ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya mabaharia wa KMKM.
Bao hilo pekee lilipachikwa kimiani mapema katika dakika ya tano mfungaji akiwa Mohammed Abdulrahman aliyeunganisha kwa shuti mpira wa adhabu uliochongwa na Ali Juma.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa, huku wachezaji wa timu hizo wakikamiana, hali iliyosababisha mwamuzi Makame Chirau kupata wakati mgumu kuwatuliza.
Rafu za mara kwa mara, zilimfanywa mwamuzi huyo kupoteza uvumilivu, na kuwafurusha nje kwa kadi nyekundu, mchezaji Sadik Habib wa Mafunzo na Azizi Shaweji wa KMKM baada ya kukunjana mashati katika dakika ya 74.
Ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya TBL kupitia kinywaji cha Grand Malt, itaendelea tena leo, ambapo katika uwanja wa Amaan, masarahange wa Malindi wataoneshana kazi na wavuta nanga wa Bandari, na huko Gombani, Jamhuri itawavaa wajenga uchumi wa Duma
No comments:
Post a Comment