Na Ameir Khalid
KLABU ya Coastal Union kutoka mkoani Tanga, juzi iliangushia kipigo timu ya kikosi cha Zimamoto, kwa kuichapa bao 1-0 katika uwanja wa Ngome Fuoni.
Wagosi hao ambao wamepiga kambi kisiwani hapa kujiandaa wa ajili ya ligi kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Septemba 15, walionesha mchezo mzuri uliowafurahisha mashabiki waliofika uwanjani hapo.
Katika mchezo huo, Coastal Union ilishusha kikosi chake chote cha kwanza ambacho inakitegemea kukitumia katika msimu mpya wa ligi inayodhaminiwa na kampuni ya simu ya Vodacom.
Bao pekee lililoitoa kifua mbele Coast, lilipachikwa kimiani mnamo dakika ya 28 kupitia kwa kiungo wa zamani wa Simba SC Joseph Owino.
Akiwa nje ya 18, Owino aliachia shuti la nguvu lililotinga moja kwa moja nyavuni huku mlinda mlango wa Zimamoto akishindwa kulipangua.
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa wageni hao kutoka Tanga kupata ushindi hapa Zanzibar, ambapo kwanza iliwasasambua mabingwa wa soka wa Zanzibar Fuper Falcon kwa magoli 3-0.
No comments:
Post a Comment