Habari za Punde

Milovan aweweseka na Azam


Na Calvin Kiwia, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Simba Milovan Cirkovic, amepigwa butwaa na kutamka kuwa hafahamu kilichowakuta mabeki wake wapya wa kati, Paschal Ochieng na Komanbilli Keita lakini amesema watakapokutana na Azam keshokutwa itakuwa ni habari nyingine.

Milovan amekiri kuwa katika mechi zote nne za kirafiki alizocheza dhidi ya Mathare United, JKT Oljoro zote ikishinda mabao 2-1 na Sony Sugar aliyotoka nayo sare ya bao 1-1 hazifikii ugumu wa Sofapaka iliyowakung'uta wekundu hao mabao 3-0 Alhamisi iliyopita.

"Kwenye mechi ya Ngao ya Hisani na Azam hatuwezi kucheza hivi, itakuwa ni stori tofauti kabisa. Mnatakiwa kujua kwamba Sofapaka ilikuwa mechi yetu ya kwanza tangu tutoke kambini Arusha na sikuridhika na hali halisi”, alifafanua.

"Mambo yatakuwa vyengine, tunaingia kuikabili Azam kwa mtazamo tofauti kwa kuwa tunakwenda kwenye mashindano ya msimu huu," alisisitiza kocha huyo ambaye kwenye kambi ya wiki tatu jijini Arusha aliridhishwa na kazi ya safu yake ya ulinzi na kutamka kwamba Simba haina tatizo kwenye safu hiyo hasa kwa ujio wa Ochieng na Keita.

"Timu yangu nimeifanyisha mazoezi kwa muda mrefu ninaijua na nafikiri kila mmoja yupo tayari kwa mashindano, ingawa kuna matatizo yaliyoonekana kwenye safu ya ulinzi katika mechi na Sofapaka.

Hata hivyo, alisema hawezi kumlaumu Juma Kaseja isipokuwa Ochieng na Keita walishindwa kuelewana, na kuongeza kuwa haelewi tatizo lilikuwa nini wakati kwenye mechi za nyuma walicheza vizuri.

Katika mchezo wa Alhamisi, beki Pascal Ochieng alianzishiwa mpira na Juma Kaseja lakini akajisahau na kujikuta adui akiwa ameshamfikia.

Alifanya uamuzi wa haraka na kutoa mpira huo kuwa kona iliyozaa penalti baada ya beki Keita kuunawa akiwa katika harakati za kuosha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.