Habari za Punde

TAKUKURU yanasa vigogo wa Chama cha Soka


Na Joseph Ngilisho, Arusha
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Arusha, imemtia mbaroni na kumfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani humo (ARFA), Khalifa Mgonja, (70) na Katibu wake, Adam Brown (58) kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao na kujipatia mamilioni ya fedha kinyume cha sheria.

Wakisoma mashtaka katika mahakama ya hakimu mkazi wa Arusha, Hawa Mguruta waendesha mashtaka wa taasisi hiyo Hamidu Simbano na Rehema Mteta, walidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja na kwa tarehe tafauti mwaka 2009 na 2010, walitumia madaraka yao vibaya na kujipatia mamilioni ya fedha.

Mteta alisema shitaka la kwanza ni la Mgonja ambaye Disemba 11, 2009 akiwa Mwenyekiti wa ARFA, alighushi barua kuomba Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) shilingi milioni 121, kwa ajili ya kusaidia kuinua timu ya mkoa, kinyume cha sheria.

Katika shitaka la pili inadaiwa Novemba11, 2010, Mgonja, alitumia vibaya madaraka yake na kujipatia shilingi.milioni 38 na shitaka la tatu kati ya Agosti 28, 2010, alijipatia shilingi milioni sita.

Shitaka la nne linamuhusu Mgonja na Brown kwa pamoja, ambapo Disemba 2009 na Agosti 26 mwaka 2010, wanadaiwa walijipatia shilingi milioni 33 na kuzitumia vibaya.

Baada ya kuwasomea mashtaka hayo, Mteta alisema upande wa serikali hauna pingamizi na dhamana yao na kuongeza kuwa upepelezi bado haukajamilika.

Pia aliomba Mahakama kutoa kibali cha kumkamata mshitakiwa wa tatu, Brown Francis, ambaye hajapatikana baada ya kuhojiwa na TAKUKURU na kudhaminiwa, ikielezwa kuwa, ametoweka na hajulikani aliko.

Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na Wakili wa washitakiwa hao, Alute Mughway na kusema Mahakama haipaswi kutoa kibali chochote mpaka TAKUKURU ifuate utaratibu wa kimahakama wa kuandika barua ya kuomba kuwakamata, sababu mshitakiwa huyo amekiuka sheria yao na siyo Mahakamani.

Baada ya ombi hilo , Hakimu Hawa Mguruta, aliingilia kati na kumshukuru Wakili huyo kwa kufafanua sheria na kuitaka TAKUKURU kufuata utaratibu wa kumpata mshitakiwa huyo.

Washtakiwa wapo nje kwa dhamana, baada ya wadhamini wao kujitokeza na kusaini bondi za shilingi milioni 75, ambapo mshitakiwa wa kwanza Mgonja, alitakiwa kudhaminiwa na watu wawili, na mmoja alisaini bondi ya shilingimilioni 60 na mwingine ni mtumishi serikalini.

Brown, alidhaminiwa na wadhamini wawli, kwa bondi ya shilingi milioni 15, na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 2, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.