Ni tukio liliitikisa nchi
kwa mtikiso ambao haujawahi kutokea ambapo kila familia iliguswa kwa uzito wake
kwa kupoteza baba, mama, mtoto, mjukuu, jamaa, ndugu, rafiki, jirani au sahiba.
Nchi iliijiinamia kwa
masikitiko, huzuni na simanzi huku kila mmoja wetu akitasawari na kutafakari na
kujaribu kupata maana halisi ya tukio lile kutokea katika visiwa vyetu tunapata
mazingatio gani?
Kinachonisikitisha tena
masikitiko yenye huruma kwamba tarehe hii 10/09/2012 imetupita kimya si kwa
Serikali au wananchi walioweza kutukumbusha
kwa kumbukumbu ya aina yoyote ile maafa mazito yaliyotokea tarehe hii. Tena
ni mwaka mmoja tu tokea kutokea kwake. Niwekeni sawa kama nitakuwa nimekosea.
Imenikumbusha tukio zito
lilitokea September 11 mwaka 2001 Marekani wakati miongoni mwa majengo marefu duniani
ya Twin Tower yalipodondoshwa na ndege zilizotekwa nyara. Kila ikifika tarehe
hii imekuwa ni tukio la kitaifa na kuna kumbukumbu maalum pamoja na ibada
hufanyika kwa wenzetu. Wamarekani zaidi ya Elfu tatu walifariki.
Waingereza walipofikwa na
maafa ya Julai 07 2005, kila mwaka tarehe hii hukumbukwa ambapo Waingereza takriban
52 walipoteza maisha yao katika tukio la kigaidi.
Ilipozama Mv Bukoba mwaka
1996 katika ziwa Victoria bado kuna kumbukumbu maalum ambayo hufanyika
kuwakimbuka na kuwaenzi waathrika wa ajali ile iliyotokea takriban miaka 16
iliyopita.
Alipouawawa Marehemu Abeid
Amani Karume, Rasi wa kwanza wa Zanzibar, tarehe 07/04/1972, tarehe hii imekuwa
ni tukio la kitaifa na siku ya mapumziko ambapo mpaka hii leo ikifika tarehe
hii kila mwaka, Viongozi na wananchi hukusanyika
kwa kumkumbuka na kusoma dua.
Zanzibar, tarehe hii,
ilipoteza zaidi ya wananchi 1000 ambao Mola Subhaanahu Wata’ala alishawaandikia
kwamba siku hii ndiyo watakayoondoka katika ardhi yake.
Muumba anapoleta majanga na
maangamizo ya aina yoyote hutuletea kwa lengo la kupata ‘ibra – mazingatio. Ni ‘ibra
gani tuliyoipata? Ni mazingatio gani tuliyoondoka nayo?
Tuliona vipi Viongozi wa Serikali
walivyolisimamia suala lile pamoja na kufanya jitihada za kuwapa pole wafiwa na
kupokea misaada anuwai kwa anuwai ya kihali na kimali hivi kweli tarehe hii
imepita wala habari hatuna?
Hata upande wa vyombo vya
habari kweli jambo hili liliweza kukumbukwa visiwani maana tukiangalia kwenye mitandao na magazeti
hatuoni sehemu yoyote ambayo inatukumbusha tukio la kuzama kwa Mv Spice
Islander 1.
Kukumbuka si lazima tuiweke
siku hii kuwa ya mapumziko tunaweza kufanya mapitio (review) tokea kutokea kwa
tukio lile mwaka mmoja uliopita na mpaka hivi sasa tuko wapi katika kuboresha
usalama wa vyombo vyetu vya baharini? (
Sitaki kugusia Mv Skagit hapa si pahala pake).
Tungeliweza kufanya Semina,
warsha na kuangalia hatua au mapendekezo yaliyopendekezwa na Tume
iliyochaguliwa na Rais yepi yamefanyiwa kazi na yepi yameachwa na kujaribu
kutaka kupata sababu ni kwanini.
Kukumbuka si lazima tusome
hitima, tunaweza kujaribu kuwaangalia walioathirika na maafa ya Mv Spice
Islander vipi hali zao baada ya kuondokewa na wanaowategemea, vipi misaada
walioipata iliwasaidia vipi. Vipi wameweza kukabiliana na maisha.
Kukumbuka si lazima tufanye
hauli bali ni kujaribu kuwa karibu na waathirika wa Mv Spice Islander na
kuwaonesha kwamba tukio lile ni msiba wetu wote kwa pamoja na tupo pamoja na
tutaendelea kuwa pamoja na hapa waathirika ambao wengi walikuwa ni wananchi wa
kipato cha chini wangeliweza na wao kujihisi japo kwa kiasi fulani kwamba nao
wanaenziwa na utu wao unaheshimika katika nchi waliyozaliwa kukulia na hatimae
kumaliza maisha yao.
Sijabahatika kuona tamko
lolote katika mitandao au magazeti au hata kwenye blogs ambapo kuna mmoja wetu
labda anatukumbusha kumbukumbu hii muhimu.
Hivi ni kweli ndio tayari
tumeshasahau?
No comments:
Post a Comment