Habari za Punde

50m/ zahitajika kuwafidia waliounguliwa moto Pemba

Na Haji Nassor, Pemba
ZAIDI ya shilingi 50 milioni zinahitajika ili  kuwafidia wananchi kadhaa wa kijiji cha Tumbe Wilaya ya Micheweni na Madungu Wilaya ya Chake chake Pemba, ambao walipatwa na maafa ya kuunguliwa nyumba na mali zao.
 
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud  Mohamed kwa wakati tofauti huko Tumbe na Mdungu wakati alipokuwa akizungumza na majeruhi wa ajali hiyo.
 
Alisema kuwa tathimi ya kujua fidia hiyo, imefanywa na maafisa wake wa kitengo cha Maafa kwa kushirikiana na waathirika wenyewe, mara baada ya kutokezea ajali hiyo na kitengo hicho kupata taarifa hiyo.
 

Alieleza kuwa Serikali ilipokea taarifa hiyo kwa masikitiko na huzini kubwa kutokana na wananchi hao kukumbwa na janga hilo la kuunguliwa na moto nyumba zao.
 
‘’Kwakweli Serikali ilipokea taarifa hii ya kuunguliwa moto kwa wananchi wa Tumbe na ile ya Madungu na kuhuzunishwa kutokana na wananchi kukosa makaazi na kupoteza mali zao’’,alifafanua.
 
Hata hivyo amewataka wananchi hao, kuwa na moyo wa ustahamilivu  kutokana na kukumbwa na ajali hiyo na Serikali inaangalia uwezekano wa kuwasaidia.
 
Mara baada ya kuwafariji wananchi hao, alikabidhi jumla ya shilingi milion tano na laki moja (1500, 000) kwa wananchi hao wa shehia za Tumbe na shehia ya Madungu ikiwa ni ubani wa kutoka kwa Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein .
    
 Alifafanua fedha hizo waliokabidhiwa sio fidia ya maafa bali ni mkono wa pole kutoka kwa Rais na suala la fidia kwa sas atalifikisha Serikali kuu ili kuwatafautia na zikipatikana kuwakabidhi.
 
‘’Tuelewane vizuri hizi nilizokabidhi leo sio fidia bali ni mkono wa pole kutoka kwa rais wetu mpendwa amenituma niwakabidhi za fidia inaenda kutafutwa ‘’,alizidi kufafanua
Katika hatua Waziri Aboud alieleza kuwa, kwa sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina mfuko wala bajeti maalum kwa ajili ya maafa ingawa kwa sasa hilo liko katika hatua za mwisho kuwepo.
 
Alifahamisha kuwa muda mfupi ujao Afisi hiyo ya Makamu wa Pili wa rais inaandaa taratibu za kufikisha tamko lakuanzishwa mfuko maalum wa kukabiliana na maafa pamoja na kuandaa sera na sheria.
 
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi aliwataka wananchi hao, kuwa wastahamilivu kutokana na kukumbwa na janga hilo na kuwataka wamuekee Muumba zaid.
 
‘’Msijefanya lolote kutokana na kukumbwa janga hili, na badala yake mumuelekee Mwenyenzi Muungu ili mjiombee dua ili lisitokezee tena’’,alifafanua Dadi.
 
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Tumbe Rufai Said Rufai aliwataka wananchi wake kuwa wastahamilivu kutokana na kukumbwa na janga hilo na kila mmoja limemgusa kutokana na uzito wake.
 
Baadhi ya shehia za Tumbe Wilaya ya Micheweni na Madungu Wilaya ya Chake chake walipatwa na tatizo la kuunguliwa na moto nyumba zao ambapo kiasi ya nyumba 14 zilikumbwa na mkasa huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.