Habari za Punde

Balozi Seif aagana na Balozi wa Cuba nchini

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mke wa Balozi wa Cuba Nchini Tanzania aliyemaliza muda wake Balozi Ernesto Gomez Diaz hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
  Balozi wa Cuba Nchini Tanzania aliyemaliza muda wake wa utumishi Bwana Ernesto Gomez Diaz akiwa na Mkewe kulia yake wakimuaga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza Balozi wa Cuba Nchini Tanzania aliyemaliza muda wake Bwana Ernesto Gomez Diaz kwa kazi yake nzuri iliyochangia kuimarika zaidi kwa uhusiano kati ya Cuba na Tanzania.
 
 
NA Othman Khamis Ame
 
Zanzibar itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba kutokana na Historia ya muda mrefu kati ya Mataifa hayo mawili rafiki tokea Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Ernesto Gomez Diaz aliyefika Nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar kumuaga baada ya kumalizika muda wake wa utumishi hapa Tanzania.
Balozi Seif alisema Wananchi wa Zanzibar kwa muda mrefu wameshuhudia juhudi kubwa za Cuba katika kuunga mkono Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa Zanzibar .
Aliitaja Sekta ya Afya Zanzibar kuwa ni miongoni mwa maeneo yaliyopata fursa ya kuimarika Kitaalamu na utendaji kufuatia Mpango wa Wataalamu Mabingwa wa Afya wa Cuba kuwafundisha Madaktari wazalendo hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Cuba kwamba Mpango huo unaonyesha ishara njema ya kupata Wataalamu Wazalendo wanaotarajiwa kutoa huduma za Afya mara wamalizapo mafunzo yao.
“ Kwa muda mrefu tulikuwa tukishuhudia Vijana wetu wengi wanaopata fursa za masomo ya Juu nje ya Nchi hutoweka mara wamalizapo masomo yao bila ya kujali kuwa wanaitia hasara Nchi yao kwa tamaa ya maisha mazuri zaidi”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Ernesto Gomez Diaz kwa juhudi zake za kuendelea kuunganisha nguvu ya uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Cuba.
Balozi Seif alimuahidi Bwana Ernesto Gomez kwamba Wazanzibari watahakikisha wanaendeleza mazuri yote aliyoyaacha Balozi huyo kwa kuyafanyia kazi.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Bwana Ernesto kuwa Balozi mpya wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla atakaporejea nyumbani kwa kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo Nchini ili Wawekezaji wa Cuba wapate fursa ya kuweka Vitega Uchumi vyao hapa Nchini.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba aliyemaliza muda wake Nchini Tanzania Bwana Ernesto Gomez Diaz alielezea matumaini yake kwamba Mpango wa kufundisha Madaktari Wazalendo chini ya usimamizi wa Madaktari Mabingwa wa Cuba utasaidia kupunguza uhaba wa Madaktari Zanzibar.
Bwana Ernesto alisema katika kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili Cuba inakusudia kuongeza fursa za masomo kwa Vijana wa Kitanzania hatua ambayo hata Zanzibar itafaidika na Mpango huo.
Halkadhalika Balozi Ernesto alisema Zanzibar bado ina fursa kubwa ya kujifunza kutoka Cuba katika Nyanja za Uvuvi, Utalii na Biashara kwa vile nchi hiyo tayari imeshapiga hatua kubwa za Kimaendeleo katika sekta hizo zilizoinyanyua Kiuchumi Nchi hiyo.
Aliupongeza ukarimu wa Watanzania uliomsaidia kumuwezesha kutekeleza majukumu yake hapa Tanzania kwa ufanisi zaidi .
Bwana Ernesto Gomez Diaz amemaliza muda wake wa utumishi wa Kidiplomasia Nchini Tanzania na anarejea Nyumbani Oktoba Mbili mwaka huu wa 2012 kwenda kupangiwa majukumu mengine katika Taifa lake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.