Othman Khamis, OMPR
MBUNGE wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Iddi amewataka vijana wa jimbo hilo kujiepusha na tabia ya kuwa watoto wa mitaani na badala yake kushughulikia taaluma itakayowajengea hatma bora ya maisha yao ya baadae.
Balozi Seif alisema elimu ndio msingi wa maendeleo ya mwanadamu ambayo upatikanaji wake unahitaji juhudi na maandalizi ya pamoja katika jamii.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo nyumbani kwake Mazizini wakati akizungumza na vijana 17 wa kijiji cha Mgambo walioamua kurejea katika masomo yao baada ya kutoroka skuli kwa kipindi kirefu.
Alisema watoto wengi mitaani wanafikia uamuzi wa kuacha masomo yao kutokana na ushawishi wa baadhi ya vigenge vya kihuni vinavyowazunguka katika maeneo wanayoishi.
Balozi Seif aliwataka vijana hao kuacha mchezo na kujikita zaidi katika kutafuta elimu kwani kukimbia skuli ni sawa na kuyakimbia maisha mazuri hapo baadaye.
Alieleza faraja yake kuona watoto wengi wa kijiji hicho wameamua kurejea katika masomo yao baada ya kukaa nje ya skuli kwa kipindi kirefu.
“Ukweli nimesikitika sana kuona watoto wengi walioamua kutoroka skuli wanatoka kijijini kwangu nilikozaliwa, hii inanitia uchungu sana,” alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba si jambo la kawaida kwa jamii kusimama imara katika kusaidia kuwarejesha masomoni baadhi ya watoto waliotoroka maskulini.
Mapema Msaidizi Mwalimu Mkuu wa skuli ya msingi ya Mgambo, Salim Seif Salim alisema skuli ya Mgambo hivi sasa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi ndani ya wilaya ya Kaskazini B.
Alisema tayari watoto karibu 180 wametoroka skuli.
Alisema hali ya mazingira ya kijiji cha Mgambo ya kuwa na vishawishi vingi ndio inayochangia ongezeko kubwa la utoro wa wanafunzi katika skuli hiyo.
Alifahamisha kwamba uongozi wa skuli pamoja na wazazi imefikia hatua ya kuitumia Kamati ya polisi jamii kukabiliana na watoto wanaozurura mitaani ili warejee maskulini.
Kwa upande wake mke wa Mbunge huyo, mama Asha Seif Iddi aliwataka vijana hao kupunguza vibaraza vinavyochangia watoto kujiingiza katika vigenge viovu.
Aliwaasa vijana hao kutambua kwamba wao ndio wanaotarajiwa kuwa viongozi watakaoliongoza jimbo na kijiji hicho hapo baadaye.
Balozi Seif katika kuunga mkono juhudi za vijana waliowashajiisha watoto hao kurejea skuli amesaidia mikoba, viatu, mabuku, sare na fedha za ushoni kwa vijana hao 17 ambao baadhi yao wanaonekana kuwa katika mazingira magumu.
No comments:
Post a Comment