Habari za Punde

Maalim Seif akutana na balozi wa Uholanzi nchini

  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Dk. Ad Koekkoek ofisni kwake Migombani mjini Zanzibar.


 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Dk. Ad Koekkoek ofisni kwake Migombani mjini Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa ubalozi wa Uholanzi uliofika ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar. (Picha, Salmin Said, OMKR)
 
Na Hassan Hamad OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema lengo la serikali la kuhamasisha uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ni kuandaa nafasi za ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.
 
Amesema vijana wengi wa Zanzibar bado wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira kutokana na mtazamo finyu uliopo kwa vijana kutegemea ajira kutoka serikalini, na kwamba kazi kubwa iliyopo sasa ni kuwawezesha vijana na kubadili mtazamo huo, ili waweze kujiajiri katika sekta binafsi.


Akizungumza na ujumbe wa ubalozi wa Uholanzi huko ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema serikali imejipanga kuwawezesha vijana kupitia Wizara ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika, pamoja na kuimarisha sekta za kilimo, uvuvi na utalii ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kuweza kujiajiri.
 
Ameyataja maeneo mengine yanayoweza kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kuwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji katika viwanda vidogo vidogo pamoja na kuimarisha utalii kwa wote.
 
Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais amesema serikali inakusudia kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kutimiza azma yake ya kuondokana na utegemezi wa chakula.
 
Amesema ili kufikia azma hiyo, serikali inakusudia kukiimarisha chuo cha kilimo Kizimbani hasa katika eneo la utafiti kwa lengo la kubaini maeneo na mbegu bora, na kuiomba Uholanzi kushirikiana na Zanzibar katika eneo hilo ili iweze kufikia azma yake ya kumwagilia ekari elfu nane (8000).
 
Maalim Seif amebainisha kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika awamu ya saba ya uongozi Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watoto wote waliotimia umri wa kwenda skuli kuanza masomo katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba.
 
Pia ameelezea juu ya kuimarika kwa sekta ya afya ambapo huduma za afya zimesogezwa karibu na makaazi ya wananchi na kuwaondolea usumbufu wa kufuata huduma hiyo katika maeneo ya mbali.
 
Hata hivyo amesema bado sekta ya elimu inakabiliwa na tatizo la kutoa elimu bora kwa wanafunzi, na kwamba serikali inafikiria juu ya namna ya kuifanya elimu inayotolewa kuwa bora na yenye manufaa zaidi kwa wahitimu.
 
Kuhusu afya amesema bado sekta hiyo inakabiliwa na upungufu wa madaktari wenye sifa pamoja na wauguzi, na kupongeza mchango wa baadhi ya nchi zikiwemo India na Cuba katika kusaidia kupunguza tatizo hilo.
 
Nae balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Dk. Ad Koekkoek amesifu mipango imara iliyowekwa na serikali katika kuwakomboa wananchi.
Amesema serikali inapaswa kuweka kipaumbele katika uwekezaji na kuwajengea mazingira bora wawekezaji waliopo ili waweze kuwa mabalozi wa wazuri kwa wawekezaji wengine kutoka nje ya nchi.
 
Balozi Koekkok pia ameelezea umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya uwekezaji, na kurejea kauli yake kuwa mashirika ya ndege ya nchi hiyo tayari yameonesha nia ya kufanya safari zake moja kwa moja hadi Zanzibar.
 
Nchi hizo mbili zimeahidi kuendeleza mashirikiano ya muda mrefu yaliyopo kwa maslahi ya pande hizo mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.