Habari za Punde

Balozi Seif aupongeza Umoja wa Mataifa kutimiza miaka 67

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Alberic Kacou kufuatia Umoja wa Mataifa kutimia Miaka 67 tokea kuasisiwa kwake. Pongezi hizo alizitoa hapo Ofisini kwake katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa aliyepo Tanzania Bwana Alberic Kacou akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwakilishi Mpya wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar Bibi Anna Senga


Na Othman Khamis Ame

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Umoja wa Mataifa { United Nation } kwa kutimia miaka 67 tokea kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1945.

Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati akisalimiana na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo { UNDP } hapo Ofisini kwake katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Ujumbe huo wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa ulioongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa aliyepo Nchini Tanzania Bwana Alberic Kacou uliambatana pia na Mwakilishi wa Shirika hilo aliyepo Zanzibar Bibi Anna Senga.

Balozi Seif alisema Umoja huo umeundwa maalum kwa lengo la kutoa huduma itakayokidhi mahitaji ya Mataifa yote Wanachama wa Umoja huo hasa katika masuala ya kustawisha Amani na ustawi wa Jamii.


Alieleza kwamba Taasisi zilizoundwa chini ya mwamvuli wa Umoja huo zimekuwa zikiendelea kutoa huduma mbali mbali kwa Mataifa Wanachama zilizopelekea kupiga hatua kubwa za Maendeleo hasa katika Nchi za Dunia ya Tatu.

Alisema Jamii za Kimataifa zimekuwa zikishuhudia ufanisi huo hasa katika miradi ya Afya, Chakula na lishe, Maji, sambamba na kudhamini Mafunzo ya Elimu ya Uraia kwa lengo la kutandika Demokrasia Duniani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwamba Zanzibar bado inahitaji kuendelea kuungwa mkono na Taasisi za Umoja huo katika harakati zake za Maendeleo na Ustawi wa Jamii.

Alifahamisha kwamba mradi wa huduma za maji safi na salama katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba umepewa kipaumbele katika jitihada za kuweka miundo mbinu.

Aliutaka Uongozi wa Taasisi hizo za Umoja wa Mataifa licha ya juhudi zinazoendelea kuchukuwa za kuiunga mkono Zanzibar lakini bado ina nafasi ya kusaidia miradi mengine katika Sekta ya Elimu, Kilimo sambamba na Elimu ya Uraia { Sivic Education }.

Mapema Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa aliyepo Nchini Tanzania Bwana Alberic Kacou alimueleza Balozi Seif kwamba Umoja huo kupitia Mashirika yake ya Umoja huo { UNDP } yatajitahidi kuendelea kuangalia mazingira ya kusaidia sekta ya Afya, Chakula na Lishe. Bibi Anna Senga anatarajiwa kufanyia kazi zake za Shirika la Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa { UNDP } Hapa Zanzibar ambae ni mwakilishi wa Shirika hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.