Habari za Punde

Balozi Seif awaasa wana CCM kuepukana na Rushwa

 
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Blozi Seif Ali Iddi amesema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuwa salama iwapo Wanachama na Viongozi wake watadumisha haki na wajibu kwa kuzingatia kuiepuka Rushwa.
 
Balozi Seif aliyasema hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Singida uliofanyika katika Bwalo la Chuo cha Utumishi wa Umma Kiliopo Mjini Singida.
 
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pia Mlezi wa Mkoa huo wa Singida Kichama alisema Serikali zote mbili pamoja na Chama zimekuwa zikipigika vita Rushwa kwa vile inavuruga Maendeleo ya Umma.
Alifahamisha kwamba Kiongozi anayetaka Uongozi kwa kutumia rushwa hafai na anaweza kukigawa Chama Vipand e vipande kwa sababu ameshalenga kujilimbikizia mali baada ya kuchaguliwa.
 
“ Kuleni fedha zao na kura katika uchaguzi mnazozifanya mpeni Yule mwenye uwezo wa kuongoza. Tena msiziache katu maana hawana uchungu nazo”. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Tifa ya CCM alisema wana CCM hawawezi kwenda kinyume na Sera na Ilani walizo zitengeneza wao wenyewe.
 
Alieleza kwamba suala hilo hufanikiwa vyema kiutekelezaji pale wanachama wenyewe wa CCM wanapoamua kuwachagua Viongozi wenye nguvu za kutetea Maendeleo yaliyopatikana kutokana na Sera za Chama cha Mapinduzi.
 
Balozi Seif aliwakumbusha wana CCM hao kwamba hakuna Mtu wala Kikundi cha Watu kitakachoweza kutetea Sera na Ilani za Chama hicho isipokuwa wanachama wenyewe wa Chama cha Mapinduzi.
 
Aliwapongeza Wanachama wa Chama hicho kutoka sehemu mbali mbali ndani ya Mikoa ya Tanzania walioamua kuomba nafasi tofauti za Uongozi ndani ya Chama hicho kwa lengo la kuimarisha nguvu za Chama chao.
 
Balozi Seif alisema Vikao vya juu vya Chama hicho vilifikia wakati kutengua kanuni kutokana na uwezo makini wa wanachama walioomna nafasi za Uongozi.
“ Taratibu zilikuwa zikiongoza namna ya idadi ya wagombea kwa kiwango kilichowekwa lakini umadhubuti wa wanachama hao ulipelekea idadi ya wagombea kutopunguzwa kwa mujibu wa Kanuni.
 
Katika Mkutano huo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif katika kuupa Baraka Mkutano huo ametoa mchango wa shilingi laki tano { 500,000/- } kusaidia harakati za uchaguzi Mkuu huo wa CCM Mkoa Singida.
 
Mapema Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Singida Mama Naomi Kapambala akitoa muhtasari wa Taarifa za Chama za Mkoa huo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya 2007 hadi 2012 alisema kumekuwa na Mafanikio makubwa kimaendeleo ndani ya Mkoa huo.
 
Mama Naomi Kapambala alisema ushahidi wa maendeleo hayo ni suala la bara bara zenye kiwango kinachokubalika kilichopelekea kuongezeka kwa harakati wa Kiuchumi mara dufu.
 
“ Miaka mitano iliyopita ilikuwa mashaka kufika Singida kutokea Mjini Dodoma, Abiria au magari yalikuwa yakichukuwa takriban muda wa zaidi ya masaa manane kufika Mkoani humo”.Alifafanua Mama Naomi.
 
Katibu wa CCM WA Mkoa huo alielezea kwamba hatua hiyo inatokana na Sera na Ilani sahihi ya Chama cha Mapinduzi katika utekelezaji wake kuanzia shina, Jimbo, Wilaya Mkoa hadi Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.