Waingereza walipotaka
kuwalemaza wananchi wake wasijihusishe na siasa waliandaa mfumo maalum ambao
uliwashughulisha wananchi wengi wa kawaida na huku wakiwaachia tabaka dogo la
mabepari na walio kwenye matabaka ya juu
(upper class) kushiriki siasa.
Walichokifanya ni kuwajengea
mazingira ya kupenda michezo kwa ujumla na hasa mpira wa miguu na kuujengea
ushindani mkubwa mpaka imekuwa ndiyo siasa ya wananchi wa kawaida kuzungumzia
mipira kila kona na kila sehemu. Homa
hii siku hizi ipo hata nyumbani ambapo mtoto mdogo anaweza kukuelezea kuhusu
ligi ya Uingereza na wachezaji wake kwa upeo mkubwa.
Pia baada ya pirika pirika
za kwenda mbio na maisha siku za wikiendi wamewawekea sehemu za kujifurahisha
kwa vinywaji na miziki ya kila aina ili izidi kuwasahaulisha na msongamano wa
mawazo wa wiki nzima na hivyo kuwa na muda mchache kuzungumzia siasa za nchi.
Naam waingereza walifanikiwa
vizuri sana maana sera hii inazidi kuendelezwa na huku wanaoshiriki katika
maamuzi muhimu na nyeti ya nchi ni kundi la wanasiasa wachache wanaotoka katika
matabaka maalum.
Wazanzibari walipotaka
kuwalemaza wananchi wake waliwajengea maskani na mabaraza ya mazungumzo ili
wapate muda mwingi wa kuzungumzia siasa na yanayojiri huku na kule katika
mkondo hatari wa siasa.
Wanasiasa wakaichukua siasa
na kuitoa pahala pake inapopaswa iwepo wakaipeleka sehemu isiyopaswa kuwepo na
kumshughulisha kila mmoja wetu na siasa. Siasa ipo majumbani, siasa ipo
barazani, siasa ipo makazini, siasa ipo mitaani, siasa ipo kanisani, siasa ipo
misikitini almuradi siasa wee siasa wee. Ilifika wakati majirani walishindwa kuzikana kwa sababu ya siasa, ndugu kukhasimiana kwa sababu ya siasa.
Wanasiasa wakajisahau
wakiona muradi umepatikana kila ikizungumzwa siasa kila kona wao huchekelea na
kuendelea na siasa yao bila ya kujali siasa inayoendelea kwengine.
Siasa hii ya mitaani sasa
imekuwa. Mitaani imekuwa hakuwatoshi tena hasa baada ya kukosa sehemu ya kutoa
joto lao tokea vyama viwili vikuu vya siasa kuamua kuacha tofauti zao za
kisiasa walipounda serikali ya umoja wa kitaifa.
Vijana wengi hawana ajira, serikali imeshindwa kujifunza
jinsi Uingereza ilivyoweza kuwadhibiti vijana wake angalau kwa waliokuwa hawana
ajira kuwapatia Misaada ( Benefits)
wajikimu wakati wakitafuta ajira.
Vijana wengi mitaani ambao
ndiyo asilimia kubwa ya wakaazi hawana vivutio vya kuwapumbaza haswa siku za
mapumziko kama ilivyo Uingereza ambapo wamewekeza katika michezo kwa kiasi
kikubwa wakiwa na malengo yao. Vijana
hawa huishia vijiweni na mwishowe kujiundia vikundi vya kihuni kama ubaya
ubaya, mbwa mwitu, kimya kimya na kutishia jina zuri la Zanzibar pamoja na sifa
yake kuwa visiwa vya amani. Wengine, Mola awarehemu, kujiingiza katika madawa
ya kulevya.
Athari za kujionea mambo
yanayofanyika katika nchi za nje iwe kwenye televisheni au kwenye mitandao
imewaingia vijana wetu mpaka sasa kukitokea fujo la aina yoyote basi , usalama,
amani hupotea haraka sana, maduka kuvunjwa, mali kuporwa, vifaa kuharibiwa kwa
kile ambacho vijana wamekuwa wakikisubiri tu kitokee na wao kuanza kazi zao.
Mambo haya yalikuwa hayapo Zanzibar, yametokea wapi? Hili ndilo la kujiuliza
kama ni Serikali.
Hivi ni kweli wafuasi wa
uamsho ndio wanaovunja Baa na kisha kuonekana wakigida bia na ulevi hadharani?,
Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio waliokwenda kuitia moto maskani mama ya
kisonge?, Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio wanaoweka vizuizi katika
barabara na kisha kuwapora watu kwa nguvu? Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio
waliomkamata na kumkata mapanga askari wa FFU?
Masuala yote majibu yake
yapo kwa suala la kimsingi la serikali kushindwa kuwa na mfumo wa kuwajengea
msingi mzuri kundi la vijana wanaotegemewa kuwa taifa la kesho. Serikali
imevuna ilichokipanda.
Yaliyojiri mwezi wa tano
mwaka huu wakati mmoja wa viongozi wa Uamsho alipokamatwa na Polisi na kuwekwa
ndani iliigharimu sana serikali kwa jina la Zanzibar kutiwa doa, kutumika
vyombo vya Dola katika kuleta utulivu na tuliamini matokeo ya vurugu zile
yalikuwa ni fundisho kwa Serikali, Polisi na Uamsho yenyewe ambayo
ilithibitisha kutohusika na vurugu zile moja kwa moja.
Miezi mitano baadae
imeonekana kwamba vyombo hivi ima vimefeli katika mtihani wake uliopita au
kimeingia kidudu mtu aliyetaka kujaribu kuirejesha ile hali ambayo Wazanzibari
wengi wanaopenda amani na utulivu wa nchi
yao wanaiona gharama yake kwa vitendo. Kitendo cha kutekwa nyara mmoja katika
viongozi wa uamsho na kuchukuliwa kusikojulikana kimeibua yaliyoibuka kama
ilivyokuwa mwezi wa tano. Mara hii tu angalau makanisa hayakuchomwa au
kuharibiwa.
Baada ya siku tatu kiongozi
kaonekana na tumesikia kauli yake yaliyojiri wakati alipotekwa nyara na akihojiwa. Kwa kuwa kauli hizi ni za upande
mmoja na zitazokosa ushuhuda wa upande wa pili zitabakia kwenye miono na maoni
tofauti kwa wenye kuzisikia.
Uamsho wanapaswa kujiangalia
tena na kurudi mezani kujitathmini kwa nia zao njema walizonazo na mazingira au
halisi iliyopo na njia zao wanazozitumia hasa ukiangalia matukio yenyewe
yanavyonasibishwa na Uamsho kwa kuwa tu hisia zinatufanya tuamini hivyo.
Hali ya Zanzibar kwa sasa ni
tete sana, tupo katika hatua muhimu ya kukusanya maoni juu ya Katiba mpya. Hali
kama hii itaakisi mawazo, fikra na maoni ya wachangiaji na hivyo kupelekea
kupata mawazo yaliyojaa hisia zaidi kuliko hali halisi
Uamsho ina takriban miaka kumi
tokea kuanzishwa kwake. miaka kumi ni
muda mzuri wa kujifanyia tathmini yakinifu.Alhamdulillah Imekuwa ikifanya
harakati nyingi zenye kuleta tija kubwa kwa Waislamu na nchi kwa ujumla kama
kushiriki kikamilifu katika kuunganisha wananchi wa visiwa hivi waondokane na
tofauti za kisiasa na hatimaye kuzaliwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Ila Uislamu ni dini ya amani
kama zilivyo baadhi ya dini nyingine, matendo maovu ya wachache yanaharibu
taswira ya Uamsho yenyewe kwanza na baya
zaidi kuharibu taswira ya Uislamu kwa ujumla.
Uislamu ndio unaopigwa vita
na si Uamsho kama inavyoonekana kwasababu ya kupelekea waislamu na uislamu
kuingizwa na kujumuishwa kwenye kapu moja la mambo mabaya.
Mimi binafsi ninakataa
katakata kwamba vurugu zilizotokea zimefanywa na wafuasi wa Uamsho, hawa ni
wahuni tu wanatumia fursa na mwanya wanaopewa na Uamsho katika harakati zake.
Mfuasi wa uamsho hana definition ni nani ni mwanachama (card holder) supporter
( anayewaunga mkono), sympathiser ni nani hivyo mtu yeyote anaweza kujinasibu
na kujilabu kwamba mimi ni Uamsho.
Kwa kuutendea haki Uislamu,
nadhani iko haja kwa Uamsho kujaribu kukaa chini ni kutafakari pamoja na
kujitathmini katika mwenendo wa matukio yanayotokea hapa nchini na jinsi jamii
iliyokosa maadili sahihi ya malezi na makuzi inavyojidhihirisha wakati wa
vurugu na fujo.
Mwandishi wa makala hii nadhani alianza vizuri lakini kwa vile tayari akilini mwake alishajenga dhana basi ameshindwa kukaa katika mstari wa hoja yake kama alivyoanza kuieleza. si nia yangu kufanya majibizano lakini ni wazi kuwa vurugu hizi zinazotokea mara kwa mara tangu mwezi May huwezi kuwaacha uamsho nje uamsho wanahusika moja kwa moja na vurugu hizi na nilazima wawajibike kwa kila tukio. Kwa mfano, kauli za viongozi wa wa uamsho ambazo hutokea kabla ya vurugu huwa ni za kuchochea uvunjifu wa amani na zinatolewa hadharani. ama baada ya kauli hizo kinachofuata ni vurugu, sasa hapo ndugu yangu simai kama huoni uhusiano wa vurugu na uamsho itabidi nikusamehe tu na kukuombea ujaliwe kutambua hilo. Ni mara ngapi tumeona mikutano ya hadhara ikiitishwa na uamsho, je uliwahi kwenda kuuliza wale walioitikia wito ni wanachama au la, je ulishataka kujua wanahusikaje na uamsho? unapokuja na denial ya uanachama wa watu ambao hata hujafanya utafiti mdogo tu na kujua uhusiano wao ukoje unakuwa hujabalance story yako. Vurugu hizi zitakoma siku hao viongozi wa uamsho watakapokoma kufanya uchochezi, kamwe watu hawawezi kuvamia mitaa kama hawajaunganishwa kufanya hivyo. Rai yangu kuwa ni vema tutenganishe shughuli za siasa na masuala ya dini. uamsho inatakiwa irudi kwenye mstari na kujihusiha na malengo ya kuendeleza dini na imani za waumini. haya mambo ya siasa kudai jamhuri ya zanzibar wawaachie wanasiasa na jamii lakini lisiingizwe kwenye mkondo wa dini...litapoteza maana.
ReplyDeleteHowever, nakubaliana na wewe kuwa vijana wa kizanzibari ambao damu zao zinachemka hawana social activities za kuwafanya waweze kudischarge stress na mambo mengine. Leo hii michezo na burudani zanzibar inahusishwa sana na masuala ya kiimani za dini. Si vijana wote watapenda kucheza soka, kuna wengine wanapenda burudani, wanataka kwenda kucheza muziki tena wa kizazi chao. Leo hii kwa mzanzibari kwenda kwenye sehemu za burudani inaonekana ni taboo matokeo yake mambo yanayofanyika chini ya carpet yanatia aibu. Hawa vijana wakikosa wanachokitaka huishia kutumia madawa ya kulevya, kuvuta bhangi, kufanya ufuska, nk. Ningeshauri kila jambo lifanywe kwa wakati wake, kama ni wakati wa ibada basi watu wafanye hivyi lakini kama ni wakati wa burudani basi wapewe muda wa kuburudika.
Nitakupa mfano mmoja ikifika friday night zanzibar inakuwa dull hakuna shughuli za burudani kwa vijana na wengi wao wanakuwa kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na mambo mengine mabaya. Ninachosisitiza kuwa tusiwe wanafiki na kila jambo lifanywe kwa uwazi.
MCHANGIAJI WA JUU BADO NAONA HUJAMUELEWA MUANDISHI ,HIVI MATATIZO YOTE AMBAYO WANAYAFANYA SERIKALI HII KWA KUWADHULUMU RAIA WAKE HUYAONI ? MIMI NAKUOMBA USIWE MJINGA WA MAWAZO zANZIBAR SERIKALI NA WATU KAMA NYINYI AMBAO HAMUTAKI MABADILIKO NDIO MULIOTUFIKISHA HAPA. NANI ASIE JUA KAMA SERIKALI HAITENDI HAKI ? MAWAZO KAMA HAYO YAKO NDIO YANATUFANYA wAZANZIBAR KUTOJIELEWA.
DeleteThe issue here ni wewe kuja na uchambuzi wako ni kwa kiasi gani umemuelewa huyo mchangiaji, mimi nimefanyakazi yangu ya kukosoa na kuunga mkono pale palipohitajika kufanya hivyo. Huu si ukumbi wa malumbano bali ni wasaa wa kutoa hoja na fikra zako wewe binafsi ili tupige hatua.
DeleteNawashukuru wote mliochangia pamoja na kukosoa kwani zote ni changamoto za kiuandishi.
ReplyDeleteNilipoiandaa hii makala ilikuwa kabla ya machafuko na vurugu kutokea na baada ya kutokea ndipo ulipoona mwisho wa makala tulijaribu kuonesha udhaifu wa pande zote na kwa kiasi fulani ninaweza kufahamu point ya kuchochea vurugu kutokana na kauli zilizokuwa zikitolewa katika viriri na viongozi wa uamsho ni kama propaganda ambayo imewasukuma hasa vijana kujiamulia na kuchukua sheria mikononi mwao.
Au kwa maana nyengine kama UAMSHO wangetumia lugha na maneno yasiyoashiria kutishia au kuvunja amani vijana wasingeingiwa na munkari.
Shukran kwa kuchangia,tupo pamoja katika kuchangia taifa letu kwa mawazo.
A K Simai