Habari za Punde

Uamsho - Umefika wakati wa kujitathmini

Na  A. K Simai

Waingereza walipotaka kuwalemaza wananchi wake wasijihusishe na siasa waliandaa mfumo maalum ambao uliwashughulisha wananchi wengi wa kawaida na huku wakiwaachia tabaka dogo la mabepari na walio kwenye matabaka ya juu  (upper class) kushiriki siasa.

Walichokifanya ni kuwajengea mazingira ya kupenda michezo kwa ujumla na hasa mpira wa miguu na kuujengea ushindani mkubwa mpaka imekuwa ndiyo siasa ya wananchi wa kawaida kuzungumzia mipira kila kona na kila sehemu.  Homa hii siku hizi ipo hata nyumbani ambapo mtoto mdogo anaweza kukuelezea kuhusu ligi ya Uingereza na wachezaji wake kwa upeo mkubwa.

Pia baada ya pirika pirika za kwenda mbio na maisha siku za wikiendi wamewawekea sehemu za kujifurahisha kwa vinywaji na miziki ya kila aina ili izidi kuwasahaulisha na msongamano wa mawazo wa wiki nzima na hivyo kuwa na muda mchache kuzungumzia siasa za nchi.


Naam waingereza walifanikiwa vizuri sana maana sera hii inazidi kuendelezwa na huku wanaoshiriki katika maamuzi muhimu na nyeti ya nchi ni kundi la wanasiasa wachache wanaotoka katika matabaka maalum.

Wazanzibari walipotaka kuwalemaza wananchi wake waliwajengea maskani na mabaraza ya mazungumzo ili wapate muda mwingi wa kuzungumzia siasa na yanayojiri huku na kule katika mkondo hatari wa siasa.

Wanasiasa wakaichukua siasa na kuitoa pahala pake inapopaswa iwepo wakaipeleka sehemu isiyopaswa kuwepo na kumshughulisha kila mmoja wetu na siasa. Siasa ipo majumbani, siasa ipo barazani, siasa ipo makazini, siasa ipo mitaani, siasa ipo kanisani, siasa ipo misikitini almuradi siasa wee siasa wee. Ilifika wakati majirani walishindwa kuzikana kwa sababu ya siasa, ndugu kukhasimiana kwa sababu ya siasa.

Wanasiasa wakajisahau wakiona muradi umepatikana kila ikizungumzwa siasa kila kona wao huchekelea na kuendelea na siasa yao bila ya kujali siasa inayoendelea kwengine.

Siasa hii ya mitaani sasa imekuwa. Mitaani imekuwa hakuwatoshi tena hasa baada ya kukosa sehemu ya kutoa joto lao tokea vyama viwili vikuu vya siasa kuamua kuacha tofauti zao za kisiasa walipounda serikali ya umoja wa kitaifa.

Vijana wengi  hawana ajira, serikali imeshindwa kujifunza jinsi Uingereza ilivyoweza kuwadhibiti vijana wake angalau kwa waliokuwa hawana ajira kuwapatia Misaada ( Benefits)  wajikimu wakati wakitafuta ajira.

Vijana wengi mitaani ambao ndiyo asilimia kubwa ya wakaazi hawana vivutio vya kuwapumbaza haswa siku za mapumziko kama ilivyo Uingereza ambapo wamewekeza katika michezo kwa kiasi kikubwa wakiwa na malengo yao.   Vijana hawa huishia vijiweni na mwishowe kujiundia vikundi vya kihuni kama ubaya ubaya, mbwa mwitu, kimya kimya na kutishia jina zuri la Zanzibar pamoja na sifa yake kuwa visiwa vya amani. Wengine, Mola awarehemu, kujiingiza katika madawa ya kulevya.

Athari za kujionea mambo yanayofanyika katika nchi za nje iwe kwenye televisheni au kwenye mitandao imewaingia vijana wetu mpaka sasa kukitokea fujo la aina yoyote basi , usalama, amani hupotea haraka sana, maduka kuvunjwa, mali kuporwa, vifaa kuharibiwa kwa kile ambacho vijana wamekuwa wakikisubiri tu kitokee na wao kuanza kazi zao. Mambo haya yalikuwa hayapo Zanzibar, yametokea wapi? Hili ndilo la kujiuliza kama ni Serikali.

Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio wanaovunja Baa na kisha kuonekana wakigida bia na ulevi hadharani?, Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio waliokwenda kuitia moto maskani mama ya kisonge?, Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio wanaoweka vizuizi katika barabara na kisha kuwapora watu kwa nguvu? Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio waliomkamata na kumkata mapanga askari wa FFU?

Masuala yote majibu yake yapo kwa suala la kimsingi la serikali kushindwa kuwa na mfumo wa kuwajengea msingi mzuri kundi la vijana wanaotegemewa kuwa taifa la kesho. Serikali imevuna ilichokipanda.

Yaliyojiri mwezi wa tano mwaka huu wakati mmoja wa viongozi wa Uamsho alipokamatwa na Polisi na kuwekwa ndani iliigharimu sana serikali kwa jina la Zanzibar kutiwa doa, kutumika vyombo vya Dola katika kuleta utulivu na tuliamini matokeo ya vurugu zile yalikuwa ni fundisho kwa Serikali, Polisi na Uamsho yenyewe ambayo ilithibitisha kutohusika na vurugu zile moja kwa moja.

Miezi mitano baadae imeonekana kwamba vyombo hivi ima vimefeli katika mtihani wake uliopita au kimeingia kidudu mtu aliyetaka kujaribu kuirejesha ile hali ambayo Wazanzibari wengi wanaopenda amani na utulivu wa  nchi yao wanaiona gharama yake kwa vitendo. Kitendo cha kutekwa nyara mmoja katika viongozi wa uamsho na kuchukuliwa kusikojulikana kimeibua yaliyoibuka kama ilivyokuwa mwezi wa tano. Mara hii tu angalau makanisa hayakuchomwa au kuharibiwa.

Baada ya siku tatu kiongozi kaonekana na tumesikia kauli yake yaliyojiri wakati alipotekwa nyara na  akihojiwa. Kwa kuwa kauli hizi ni za upande mmoja na zitazokosa ushuhuda wa upande wa pili zitabakia kwenye miono na maoni tofauti kwa wenye kuzisikia.

Uamsho wanapaswa kujiangalia tena na kurudi mezani kujitathmini kwa nia zao njema walizonazo na mazingira au halisi iliyopo na njia zao wanazozitumia hasa ukiangalia matukio yenyewe yanavyonasibishwa na Uamsho kwa kuwa tu hisia zinatufanya tuamini hivyo.

Hali ya Zanzibar kwa sasa ni tete sana, tupo katika hatua muhimu ya kukusanya maoni juu ya Katiba mpya. Hali kama hii itaakisi mawazo, fikra na maoni ya wachangiaji na hivyo kupelekea kupata mawazo yaliyojaa hisia zaidi kuliko hali halisi


Uamsho ina takriban miaka kumi tokea kuanzishwa kwake.  miaka kumi ni muda mzuri wa kujifanyia tathmini yakinifu.Alhamdulillah Imekuwa ikifanya harakati nyingi zenye kuleta tija kubwa kwa Waislamu na nchi kwa ujumla kama kushiriki kikamilifu katika kuunganisha wananchi wa visiwa hivi waondokane na tofauti za kisiasa na hatimaye kuzaliwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Ila Uislamu ni dini ya amani kama zilivyo baadhi ya dini nyingine, matendo maovu ya wachache yanaharibu taswira ya  Uamsho yenyewe kwanza na baya zaidi kuharibu taswira ya Uislamu kwa ujumla.

Uislamu ndio unaopigwa vita na si Uamsho kama inavyoonekana kwasababu ya kupelekea waislamu na uislamu kuingizwa na kujumuishwa kwenye kapu moja la mambo mabaya.

Mimi binafsi ninakataa katakata kwamba vurugu zilizotokea zimefanywa na wafuasi wa Uamsho, hawa ni wahuni tu wanatumia fursa na mwanya wanaopewa na Uamsho katika harakati zake. Mfuasi wa uamsho hana definition ni nani ni mwanachama (card holder) supporter ( anayewaunga mkono), sympathiser ni nani hivyo mtu yeyote anaweza kujinasibu na kujilabu kwamba mimi ni Uamsho.

Kwa kuutendea haki Uislamu, nadhani iko haja kwa Uamsho kujaribu kukaa chini ni kutafakari pamoja na kujitathmini katika mwenendo wa matukio yanayotokea hapa nchini na jinsi jamii iliyokosa maadili sahihi ya malezi na makuzi inavyojidhihirisha wakati wa vurugu na fujo.

 

 

 

 

 

4 comments:

  1. Mwandishi wa makala hii nadhani alianza vizuri lakini kwa vile tayari akilini mwake alishajenga dhana basi ameshindwa kukaa katika mstari wa hoja yake kama alivyoanza kuieleza. si nia yangu kufanya majibizano lakini ni wazi kuwa vurugu hizi zinazotokea mara kwa mara tangu mwezi May huwezi kuwaacha uamsho nje uamsho wanahusika moja kwa moja na vurugu hizi na nilazima wawajibike kwa kila tukio. Kwa mfano, kauli za viongozi wa wa uamsho ambazo hutokea kabla ya vurugu huwa ni za kuchochea uvunjifu wa amani na zinatolewa hadharani. ama baada ya kauli hizo kinachofuata ni vurugu, sasa hapo ndugu yangu simai kama huoni uhusiano wa vurugu na uamsho itabidi nikusamehe tu na kukuombea ujaliwe kutambua hilo. Ni mara ngapi tumeona mikutano ya hadhara ikiitishwa na uamsho, je uliwahi kwenda kuuliza wale walioitikia wito ni wanachama au la, je ulishataka kujua wanahusikaje na uamsho? unapokuja na denial ya uanachama wa watu ambao hata hujafanya utafiti mdogo tu na kujua uhusiano wao ukoje unakuwa hujabalance story yako. Vurugu hizi zitakoma siku hao viongozi wa uamsho watakapokoma kufanya uchochezi, kamwe watu hawawezi kuvamia mitaa kama hawajaunganishwa kufanya hivyo. Rai yangu kuwa ni vema tutenganishe shughuli za siasa na masuala ya dini. uamsho inatakiwa irudi kwenye mstari na kujihusiha na malengo ya kuendeleza dini na imani za waumini. haya mambo ya siasa kudai jamhuri ya zanzibar wawaachie wanasiasa na jamii lakini lisiingizwe kwenye mkondo wa dini...litapoteza maana.

    However, nakubaliana na wewe kuwa vijana wa kizanzibari ambao damu zao zinachemka hawana social activities za kuwafanya waweze kudischarge stress na mambo mengine. Leo hii michezo na burudani zanzibar inahusishwa sana na masuala ya kiimani za dini. Si vijana wote watapenda kucheza soka, kuna wengine wanapenda burudani, wanataka kwenda kucheza muziki tena wa kizazi chao. Leo hii kwa mzanzibari kwenda kwenye sehemu za burudani inaonekana ni taboo matokeo yake mambo yanayofanyika chini ya carpet yanatia aibu. Hawa vijana wakikosa wanachokitaka huishia kutumia madawa ya kulevya, kuvuta bhangi, kufanya ufuska, nk. Ningeshauri kila jambo lifanywe kwa wakati wake, kama ni wakati wa ibada basi watu wafanye hivyi lakini kama ni wakati wa burudani basi wapewe muda wa kuburudika.
    Nitakupa mfano mmoja ikifika friday night zanzibar inakuwa dull hakuna shughuli za burudani kwa vijana na wengi wao wanakuwa kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na mambo mengine mabaya. Ninachosisitiza kuwa tusiwe wanafiki na kila jambo lifanywe kwa uwazi.

    ReplyDelete
    Replies
    1. MCHANGIAJI WA JUU BADO NAONA HUJAMUELEWA MUANDISHI ,HIVI MATATIZO YOTE AMBAYO WANAYAFANYA SERIKALI HII KWA KUWADHULUMU RAIA WAKE HUYAONI ? MIMI NAKUOMBA USIWE MJINGA WA MAWAZO zANZIBAR SERIKALI NA WATU KAMA NYINYI AMBAO HAMUTAKI MABADILIKO NDIO MULIOTUFIKISHA HAPA. NANI ASIE JUA KAMA SERIKALI HAITENDI HAKI ? MAWAZO KAMA HAYO YAKO NDIO YANATUFANYA wAZANZIBAR KUTOJIELEWA.

      Delete
    2. The issue here ni wewe kuja na uchambuzi wako ni kwa kiasi gani umemuelewa huyo mchangiaji, mimi nimefanyakazi yangu ya kukosoa na kuunga mkono pale palipohitajika kufanya hivyo. Huu si ukumbi wa malumbano bali ni wasaa wa kutoa hoja na fikra zako wewe binafsi ili tupige hatua.

      Delete
  2. Nawashukuru wote mliochangia pamoja na kukosoa kwani zote ni changamoto za kiuandishi.

    Nilipoiandaa hii makala ilikuwa kabla ya machafuko na vurugu kutokea na baada ya kutokea ndipo ulipoona mwisho wa makala tulijaribu kuonesha udhaifu wa pande zote na kwa kiasi fulani ninaweza kufahamu point ya kuchochea vurugu kutokana na kauli zilizokuwa zikitolewa katika viriri na viongozi wa uamsho ni kama propaganda ambayo imewasukuma hasa vijana kujiamulia na kuchukua sheria mikononi mwao.

    Au kwa maana nyengine kama UAMSHO wangetumia lugha na maneno yasiyoashiria kutishia au kuvunja amani vijana wasingeingiwa na munkari.


    Shukran kwa kuchangia,tupo pamoja katika kuchangia taifa letu kwa mawazo.

    A K Simai

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.