Mtayarishaji wa Vipindi ambae pia ni Mtangazaji wa Zenji F.M Mustapha Mussa akimuuliza swali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuhusiana na masuala mbali mbali ya Maendeleo, Kijamii na Kisiasa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu za Nchi wakati akifanya mahojiano na Kituo cha Matangazo ya Redio cha Zenji F.M.
Na Othman Khamis Ame , OMPR
Licha ya kuwepo kwa Uhuru wa kutosha wa Kuabudu na kupata Habari Miongoni mwa Jamii kufuatia kutanuka kwa Demokrasia Nchini lakini bado Wananchi wanapaswa kuzingatia kwa makini utumiaji wa fursa hiyo katika kulinda umoja na Mshikamano uliopo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo hapo Nyumbani Kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akizungumza na Kituo cha Matangazo ya Redio cha Zenji F.M kuhusiana na masuala mbali mbali ya Kijamii, Kisiasa, Maendeleo, Kiuchumi likiwemo pia suala kubwa la Amani ya Nchi.
Balozi Seif Alisema Zanzibar imepita katika majaribu mengi ya kukosa utulivu na amani hasa katika mivutano ya Kisiasa ndani ya mfumo wa vyama vingi na kuibuka kwa migogoro ya matokeo ya uchaguzi iliyopelekea kudumaza kwa Maendeleo na Ustawi wa Jamii.
Alishauri Uhuru huo wa kuabudu ukatumiwa vizuri ili kuwepuka upotoshaji unaoweza kuleta athari na hatimaye kuvurugika kwa amani ambayo huchukuwa muda mrefu kuirejesha.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayofuata Muundo wa Umoja wa Kitaifa imesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta utulivu wa Kisiasa uliokosekana kwa kipindi kirefu hali iliyochangia kuongezeka kwa wawekezaji kuweka vitega uchumi vyao hapa Zanzibar.
Aliwakebehi baadhi ya Watu wanaodhani kwamba yeye hauungi mkono muundo wa Serikali iliyopo hivi sasa wa Umoja wa Kitaifa jambao ambalo alikuwa na fursa na haki ya kujiuzulu kama alikuwa hakubaliani na Muundo huo.
“ Nilikuwa na haki ya kujiuzulu kama ningekuwa sikubaliana na Serikali hii. Wanaosema hivyo waelewe kwamba wamechelewa kwa vile wamesahau kwamba mimi tayari nimeshakula kiapo kuitumikia Serikali hii baada ya kuiridhia kwa karibu Miaka Miwili iliyopita”. Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia mchakato wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif alisema Wananchi lazima watumie kwa makini fursa hiyo ya kutoa Maoni yao kwa vile muundo wa katiba ipi inahitajika na Wananchi hao limo ndani ya uamuzi na mamlaka yao.
Alisema yapo mawazo tofauti yatakayotolewa na watu, taasisi na hata Jumaia za kiraia katika mchakato huo lakini cha kuzingatia zaidi kwa Wananchi ni kuendelea kuheshimu mawazo ya kila mtu na taasisi hizo ambapo tume ndio itakayokuwa na kazi ya mwisho ya kuratibu mchakato huo na kutoa mapendekezo yake.
“ Watu na Taasisi zote za Kijamii zinapaswa kuvumiliana kulingana na mawazo tofauti kuelekea katika mchakato wa katiba Mpya”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akigusia tuhuma alizobebeshwa za kuhusishwa na vurugu za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu Balozi Seif ameelezea kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya Vyombo vya Habari kutumia kalamu zao kumvurugia Heshima yake.
Alisema yeye kama Kiongozi daima hataweza kwenda kinyume na Maadili ya Uongozi kwa vile tayari ameshakubali kubeba dhima hiyo kwa kula Kiapo cha kuwatumikia Wananchi wote akiwa kama Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali.
“ Ingelivijengea sifa nzuri na mapenzi kwa Jamii vyombo hivyo vya Habari vilivyomtuhumu kama vingelitoa ushahidi hasa wa namna gani alihusika katika kusimamia vurugu hizo kwenye uchaguzi huo wa Jimbo la Bububu badala ya kuendeleza propaganda za kumvunjia Heshima”. Balozi Seif Alionyesha kusikitishwa kwake na Taarifa zilizochapishwa na baadhi ya Magazeti za kupotosha ukweli halisi.
No comments:
Post a Comment