Habari za Punde

African Kivumbi yaufyata Kizimbani

 
 
Na Abdi Suleiman, Pemba
               
KWA mara ya kwanza, timu ya soka ya Kizimbani, juzi ilianza kukalia kiti cha uongozi wa ligi daraja la kwanza Taifa Pemba , baada ya kuitandika African Kivumbi goli 1-0.
 
African Kivumbi ambayo ilikuwa ikikalia kiti hicho ikiwa na pointi 25, sasa imeteremka hadi nafasi ya pili.
 
Kizimbani ilishuka dimbani ikiwa na huzuni ya kuondokewa na kocha wao wa miaka ya themanini Dk. Kassim Suleiman (baba yake mchezaji Suleiman Kassim ‘Selembe’ wa Coastal Union na Zanzibar Heroes), ambaye hadi anafariki usiku wa kuamkia juzi, alikuwa daktari wa timu ya Mwenge.


Bao pekee la washindi katika mchezo huo uliokuwa mgumu kwa timu zote, lilifungwa na Ali Othman katika dakika ya 33.
 
Nayo FSC ikaitandika Selemu Rangers magoli 4-2 katika uwanja wa Gombani, huku Maendeleo Manta ya Makangale iliyonunua daraja ikiadhibiwa na Chuo Maendeleo kwa kuchapwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Kinyasini.
 
Matokeo mengine yalikuwa, Konde Stars kulivunja jabali la JWTZ, Hard Rock kwa kuilaza bao 1-0.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.