Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JARIBIO la baadhi ya wanachama wa Simba kutaka Mwenyekiti wa klabu hiyo Ismail Aden Rage ajiuzulu, limeshindwa baada ya kiongozi huyo kusema wanachama hao sio wenyewe.
Rage ameeleza kuwa, uongozi umebaini wengi wa wanachama wa tawi la Mpira Pesa waliojiorodhesha ili kushinikiza kufanyika kwa mkutano wa dharura wa klabu ni batili.
Hatua hiyo inafuatia wanachama hao kufanya maazimio ya kujiorodhesha ili kufikisha akidi itakayotimiza masharti ya kufanyika kwa mkutano ili kuwaomdoa madarakani viongozi wa sasa kwa madai ya kushindwa kuongoza.
Amefahamisha kuwa, pamoja na kubaini hilo, pia uongozi umegundua kwamba majina ya wanachama hao yamenakiliwa katika leja ya wanachama ambayo ilipotea mikononi mwa kiongozi mmoja wa zamani.
Alisema uongozi unaheshimu jitihada zinazofanywa na wanachama hao na kuzifanyia kazi, lakini hauwezi kutekeleza vitu ambavyo havikidhi vigezo vilivyopo katika katiba ya klabu hiyo.
Rage alisema, katiba ya sasa ya Simba haiwatambui wanachama waliopo kwenye leja, badala yake inawatambua wale waliosajiliwa katika kompyuta.
“Pamoja na wanachama hao kunakiliwa katika leja, tumebaini hata saini zilizowekwa ni za kughushi na tukifanya uchunguzi hasa tutabaini ni wengi tu hawana sifa, kitu ambacho kinakwenda kinyume na katiba ya Simba”, alisema Rage.
Rage aliongeza kuwa, wanaamini mchakato huo unafanywa na baadhi ya watu wanaotaka kuleta chokochoko ndani ya klabu hiyo kitu ambacho ni kigumu kukitimiza kwa vile uongozi upo imara na unafuata katiba ya klabu.
“Hatuwezi kujiuzulu kwa ajili ya shinikizo la watu ambao tunafahamu wanatumika, sisi tunaongoza kwa kufuata katiba na tutachukua uamuzi kwa mujibu wa katiba pindi inapostahili”, alisema.
Aidha, Rage aliongeza kwamba uongozi wa klabu hiyo ulitarajiwa kukutana jioni ya jana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom uliomalizika wiki iliyopita na Simba kushika nafasi ya tatu.
Hivi karibuni baadhi ya wanachama waliutaka uongozi wa Simba chini ya Rage kuachia ngazi baada ya timu hiyo ambayo ilikuwa ikiongoza ligi kwa kipindi kirefu kupoteza mwelekeo na kuruhusu kufungwa mara mbili.
No comments:
Post a Comment