Habari za Punde

‘Vipaji vya michezo skulini viendelezwe’

Na Mbarouk Abdallah
 
IMEELEZWA kuwa, iwapo wanafunzi wa skuli za ngazi za chini wataandaliwa mapema kimichezo ikiwemo riadha, wataweza kujijengea msingi mzuri na kuliwakilisha vyema taifa.
 
Akizungumza katika bonanza maalumu lililoandaliwa katika skuli ya kituo cha kulelea watoto yatima Zanzibar SOS, mkufunzi mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mwalimu Hamad Said Ndee, alisema vipaji vya vijana ni lazima viibuliwe mapema na kuendelezwa.


Walimu na wanafunzi wa skuli mbalimbali walishiriki katika bonanza hilo la michezo tafauti, baada ya kuhitimisha mafunzo ya siku sita yaliyolenga kufufua michezo maskulini, ili kuwajengea wanafunzi misingi ya michezo inayotumia teknolojia za kisasa yenye kuleta uwiano katika nyanja za kimataifa.
 
Ndee, ambae pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Vyama vya Riadha Duniani, alieleza kuwa michezo mitatu iliyochezwa kwenye bonanza hilo, riadha, mpira wa wavu na wa miguu kwa wanawake, inakubalika duniani kote.
 
Aidha alisema, mchezo wa riadha kwa watoto (Kids Athletic) ndio mchezo mama miongoni mwa yote kwa kuwa unajumuisha mambo matatu, ambayo ni kukimbia, kuruka na kutupa.
 
Naye Mwalmu Othman Msabah alieleza kuhamasika kwake kutokana na hatua ya kuirejesha maskulini michezo hiyo kwa vile inalenga kuwajengea misingi mizuri vijana kielimu, utamaduni na michezo. “Mchezo huu ulikuwa mkubwa hapa Zanzibar na ulipendwa na watu wengi lakini kipindi cha katikati ulikufa kwa kutupwa na sasa British Council wameamua kuufufua, nasi tumehamasika”, alieleza.
 
Aliishauri Wizara ya Habari, Utali na Michezo, kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kutengeneza vipindi maalum maskulini, kuvisimamia na hivyo kufikia lengo lililokusudiwa, na kuweka walimu wa michezo maskulini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.