Na Aboud Mahmoud
WACHEZAJI wawili wa timu ya Taifa Zanzibar ya mchezo wa mpira wa wavu unaochezwa ufukweni, wanatarajiwa kwenda Uganda leo kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki yaliyopangwa kufanyika Novemba 17 na 18, mwaka huu.
Wachezaji hao ni Omar Ali Choum na Mohammed Ismail Omar, watakaoambatana na viongozi wawili ambao ni Mwanaisha Saidzain Abubakar, mkuu wa msafara, na Meneja wa timu Abubakar Mikidadi Othman.
Mapema, akiuaga msafara huo katika ofisi za Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar Mwanakwerekwe, Mjumbe wa baraza hilo Mussa Abdurabbi, amewataka wachezaji hao kuiwakilisha nchi ipasavyo na kuitangaza kiutalii.
Abdurabbi ambaye alikuwa akimuwakilisha Mwenyekiti wa BTMZ Sharifa Khamis Salim, alisema ipo haja kwa wachezaji hao kufanya vyema kwenye michuano hiyo ili kuiletea sifa nchi yao.
Aidha, alieleza kuwa kufanya kwao vizuri, kutaisaidia Zanzibar kujiuza kitalii kwani mchezo huo unapendwa sana na watalii.
"Mkiwa Uganda, nakuombeni mshindane badala ya kushiriki, mfanye vyema na kuitangaza nchi yetu ili tuweze kupata watalii wengi", alisisitiza.
Aidha aliwataka kuzingatia nidhamu wakati wote wakiwa uwanjani na katika sehemu mbalimbali watakazotembelea ili kuitunzia heshima Zanzibar pamoja na kuitangaza kuwa ni nchi ya amani.
Mmoja wa wachezaji hao Omar Ali Choum, alieleza matumaini yao ya kufanya vyema kwenye mashindano hayo na kurudi na ubingwa, kutokana na mazoezi waliyofanya, ingawa alisema hiyo ni mara yao ya kwanza kushiriki ngarambe hizo.
No comments:
Post a Comment