MAELEZO
YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS SIKU YA MKESHA WA SIKU YA
UKIMWI DUNIANI TAREHE 30/11/2012
Ndugu
Wananchi,
Mwaka umetimia tangu tarehe kama ya leo mwaka
uliopita (2011) nilipotoa taarifa ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani kupitia vyombo vya
habari vya hapa nchini. Nategemea kwamba sote tunaelewa kuwa tarehe 1 Disemba
ya kila mwaka Dunia nzima huadhimisha siku hii kwa madhumuni ya kutafakari
mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazotukabili katika mapambano dhidi ya
janga hili la UKIMWI.
Ndugu
Wananchi,
Yapo mafanikio mengi yaliyopatikana duniani
kutokana na juhudi zilizofanyika ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita. Dunia
imeshuhudia kuwa juhudi kubwa za kitaalamu ambazo zinatokana na kufanyika kwa
tafiti mbali mbali katika maeneo ya kinga na tiba. Juhudi za kubuni mikakati
madhubuti inayotekelezeka na kuongezeka kwa uelewa wa jamii katika kulifahamu
tatizo linalowakabili, pamoja na ushiriki wao mzuri ni mambo yaliyosaidia sana
katika mafanikio yaliyopatikana.
Kwa mfano katika miaka hiyo kumi, maambukizo mapya
yamepungua, vifo vinavyotokana na UKIMWI
halikadhalika vimepungua na pia idadi ya watu wanaotumia dawa za kupunguza
makali ya VVU wameongezeka maradufu na sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi na
kwa matumaini.
Ndugu
Wananchi,
Mafanikio yaliyopatikana ni mengi na si rahisi
kuyataja yote hapa. Hata hivyo, pamoja
na mafanikio hayo bado changamoto zipo, nazo ni nyingi pia. Kwa mfano, pamoja
na kuona kwamba viwango vya maambukizo katika nchi nyingi kwa jumla vimepungua,
bado zipo nchi hasa kusini mwa jangwa la Sahara zenye viwango vya zaidi ya
asilimia kumi (>10%). Aidha, ndani ya baadhi ya nchi moja moja yako maeneo
yana viwango vikubwa vya maambukizi. Kwa mfano, wakati kiwango cha maambukizi
ya VVU nchini Tanzania ni asilimia tano nukta saba (5.7) baadhi ya mikoa
michache kiwango chake ni zaidi ya asilimia kumi (>10%).
Hapa Zanzibar wakati tunazungumzia kiwango cha
maambukizi cha chini ya asilimia moja
yaani zero nukta sita (0.6) (kwa kila watu 100,000 watu sita wameathirika na UKIMWI) bado katika baadhi ya makundi
ndani ya jamii yetu yana kiwango cha zaidi ya asilimia kumi.
(>10%). Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume
wenzao MSM) asilimia kumi na mbili nukta
tatu, (12.3), Wanaojidunga sindano za dawa za
kulevya (IDU) ni asilimia kumi na sita (16)
Wakinadada wanaojiuza miili yao ni
asilimia kumi nukta tatu (10.3) na kwa Wanafunzi walioko katika vyuo vya mafunzo ni asilimia mbili nukta tano (2.5).
Hali kama hiyo ni ya hatari kwani wakati
wowote, kama hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa maambukizi yanaweza kutokea
kutoka jamii yenye kiwango kikubwa kwenda kwenye ile yenye kiwango kidogo
na hatimae kusababisha mripuko. Hivyo,
inamaanisha kwamba bado tunayo kazi kubwa ya kufanya na wala tusidharau.
Kawaida kila mwaka tunapoadhimisha siku hii
adhimu. Umoja wa Mataifa hutoa kauli mbiu. Kauli mbiu inayotumika mwaka huu wa
2012 ni ile ile ya mwaka jana, yaani kuzifikia zero tatu, kwa maana ya kuwa na zero katika maambukizi mapya ya Virusi vya
UKIMWI, kuwa na zero katika unyanyapaa dhidi ya Watu wanaoishi na VVU na pia
kuwa na zero katika vifo vinavyotokana na UKIMWI. Tafsiri yake ni kwamba,
tunatakiwa tuongeze nguvu zaidi ili tufikie hali ya kutokuwepo maambukizi mapya,
kutokuwepo kwa unyanyapaa wa Watu wanaoishi na VVU na kutokuwepo kwa vifo
vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2015.
Kauli mbiu hiyo inaonekana kuwa itaendelea hadi
kufikia mwaka 2015 ambapo kila nchi itatakiwa ijitathmini imefikia wapi katika
utekelezaji wake.
Ndugu
Wananchi,
Wakati tunaelekea katika kilele cha maadhimisho ya
siku ya UKIMWI duniani hapo kesho, ni
vyema sote kwa pamoja, jamii na taasisi zote tukakumbuka kwamba tuna wajibu wa
kuchangia katika kufanikisha kuifikia kauli mbiu iliyowekwa yenye shabaha ya
kuzifikia zero tatu.
Kwa mara nyengine tena, ninatoa wito maalum kwa taasisi
mbali mbali na jamii kwa jumla kuwa lazima zitekeleze kwa vitendo, kwa kasi na
ufanisi zaidi programu za UKIMWI ili
kuhakikisha kwamba wanafikiwa lakini pia huduma za kinga na tiba wanazipata
bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile, yakiwemo makundi maalum yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi.
Makundi
haya ni yale ya wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao, wanawake
wanaojiuza miili yao na watumiaji wa dawa haramu za kulevya kwa njia ya
kujidunga sindano. Makundi yote haya ni
lazima kuyafikia kwa vile tafiti zinaonesha kuwa ndiyo yenye maambukizi makubwa
zaidi kuliko maambukizi katika jamii kwa jumla.
Ndugu
Wananchi,
Unayanyapaa ni kikwazo kikubwa bado kwenye jamii
yetu kinachokwamisha juhudi zetu katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Hivyo basi,
hatuna budi kuendeleza juhudi zetu za kupiga vita unyanyapaa kwa watu wanaoishi
na Virusi vya UKIMWI. Aidha, nachukua
nafasi hii kutoa wito maalum na kuwanasihi sana watoaji wa huduma za UKIMWI katika taasisi zote za Serikali
na za binafsi kuendelea kufuata
maadili ya kazi zao kutowabagua wala kuwanyanyapaa wateja wao wanaofika kwa
kutaka huduma mbalimbali kwani haki ya kila mtu kupata huduma. Natoa wito huo
pia kwa jamii kwa jumla kuacha tabia ya kuwanyanyapaa ndugu zetu wanaoishi na
virusi vya ukimwi tukifanya hivyo, na kama tutafanya kazi kwa kushirikiana
vizuri, tunaweza kupiga hatua kubwa katika kufanikisha malengo yetu ya zero
tatu.
Ndugu
Wananchi,
Huu ni mwaka wa 26 tokea UKIMWI ugundulike hapa Zanzibar. Kumekuwa na hatua nyingi sana zilizokwisha kuchukuliwa na
Serikali yetu kuhakikisha kwamba ugonjwa huu hauenei na huduma za kinga na tiba
zinapatikiana na pia misaada inayopatikana inawafikia wote wanaohitaji. Juhudi
nyengine zilizochukuliwa ni pamoja na kupanua huduma za kinga, ikiwemo ya
upimaji wa virusi, kuhakikisha usalama wa damu inayochangiwa wagonjwa na huduma
za kukinga maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto , tiba ya magonjwa nyemelezi, dawa
za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI.
Ushauri nasaha na mafunzo kwa wanaoishi na VVU. Hivyo, nataka nikiri kuwa yale
yote ambayo tumeyatekeleza yamewezekana tu kutokana na mashirikiano mazuri kati
ya Serikali, Washirika wa Maendeleo na taasisi zisizo za Serikali na wanajamii
walio katika ngazi za shehia mbali mbali (Unguja na Pemba).
Tunayashukuru mashirika na nchi wahisani kwa
misaada yao ya kifedha na utaalamu ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia sana
katika kupanua na kuimarisha muitiko dhidi ya UKMWI nchini mwetu. Nachukua fursa hii pia kuzipongeza na
kuzishukuru taasisi zote za ndani, za Serikali na zisizokuwa za Serikali
zikiwemo taasisi za kidini zinazoshiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya
UKIMWI. Tunawaomba wasichoke na badala
yake waendelee kushirikiana nasi katika vita hivi kwa maslahi ya taifa letu na
wananchi wetu kwa jumla.
Ndugu
wananchi,
Ningependa kutanabahisha kuwa kwa muda wote wa
mapambano tumekuwa tukitegemea sana misaada ya wafadhili ambayo kwa kiasi
kikubwa sasa imepungua. Wakati umefika
sasa kuliona tatizo la UKIMWI ni letu na kwamba sisi tunawajibika kupambana
nalo kikamilifu kwa kutumia rasilimali zilizo ndani ya uwezo wetu, wafadhili
watusaidie kwa yale mambo yaliyo nje ya uwezo wetu. Ninashukuru sana kuona kwamba Kamati za
UKIMWI za baadhi ya Shehia zimeliona hilo na kutayarisha mipango madhubuti ya
kukabiliana na changamoto wanazoziibua wenyewe katika Shehia zao na kukabiliana
nazo, bila ya kutegemea wafadhili.
Ninatoa wito kwa Kamati za Shehia nyengine ambazo bado hazina mipango
hiyo zijifunze kwa wenzao ili ziandae mipango endelevu. Kwa kufanya hivyo hivyo vita vyetu na ushindi
wetu utakuwa wa uhakika zaidi.
Ndugu
Wananchi
Kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ndiyo
yenye mamlaka ya kusimamia uratibu wa shughuli za UKIMWI hapa Zanzibar, napenda
kutoa wito kwa wananchi na wadau wote kushiriki ipasavyo katika kilele cha
maadhimisho haya ya siku ya UKIMWI ambayo kwa mwaka huu wa 2012 yatafanyika
katika Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa
Kaskazini huko Mangapwani ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Afya wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Juma Duni Haji. Katika maadhimisho hayo kutakuwa na shughuli
mbali mbali zikiwemo huduma za kupima virusi vya UKIMWI bila ya malipo na
burudani zinazolenga maudhui ya maadhimisho yetu. Nyote mnakaribishwa.
Ndugu
wananchi,
Mwisho lakini sio kwa umuhimu , nachukua fursa hii
kutanguliza shukrani za dhati kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na
kutoka kwangu binafsi, kwa uongozi wote wa Mkoa wa Kaskazini na Wilaya zake
zote mbili kwa mashirikiano mazuri katika kufanikisha maadhimisho haya.
Tukumbuke kwamba:
ZANZIBAR
BILA YA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU
ZANZIBAR
BILA YA UNYANYAPAA WA WATU WANAOISHI NA
VVU NA
ZANZIBAR
BILA YA VIFO VINAVYOTOKANA NA UKIMWI
INAWEZEKANA.
AHSANTENI,
NAWASHUKURU KWA KUNISIKILIZA.
Hotuba nzuri lakini unyanyapaa (ubaguzi) hauko kwenye ukimwi tu bali ni kila sehemu. Jamii yetu inaishi katika mazingira ambayo unapoikosoa Serikali hata kama inafanya kosa wewe utanyanyapaliwa (kubaguliwa). Kwa vile jamii yetu imejengwa hivyo na watawala wetu mara nyingi wanaounga mkono Serikali huonekana wana haki zaidi na huwa wanatumia kila fursa kuwanyanyapaa wasiokubaliana na baadhi ya maamuzi ya Serikali ambayo hayana maslahi kwa Zanzibar.
ReplyDeletekutokana na hali hiyo sasa unyanyapaa (ubaguzi) miongoni mwa Wazanzibari unaonekana ni jambo la kawaida tu. Ni kama vile unavyommbagua mpemba, au mtu wa Nungwi kwa sababu ni cuf (mpinzani wa ccm), au ccm anaetaka mkataba , UAMSHO,haya yote ni mifano hai ambayo inapaliliwa na baadhi ya hao wanaohimiza kukomesha unyanyapaa wa ukimwi; Jee tujiulize katika mazingira kama haya itawezekana hilo?
Tunatakiwa tujirekebishe na sio lazima watu wote wakubaliane na mawazo yako, tutakapofika hapo, tunaweza kusema uwezekano wa kulifikia lengo letu upo, kinyume chake tutakuwa tunapoteza muda bure na kuzidanganya nafsi zetu.