Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Akiwakilisha Taarifa ya Utekelezaji Ilani ya CCM Kwa Serekali

Na Mwantanga Ame Dodoma
SERIKALI ya Zanzibar imesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali ya umoja wa Kitaifa imeimarisha hali ya utulivu wa kisiasa, uchumi na ustawi wa jamii na itahakikisha inalinda mafanikio hayo kwa gharama zozote.

Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, aliyasema hayo jana wakati akisoma utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Oktoba 2010 hadi 2012, katika ukumbi wa mikutano wa Chamwino Nje kidogo ya Mji wa Dodoma .

Makamu huyo alisema licha ya kujitokeza baadhi ya vitendo wa uvunjifu wa amani vilivyotokea lakini katika kipindi ambacho kumekuwa na utulivu CCM imeweza kuonyesha kuwapo kwa mafanikio ndani ya serikali ya awamu ya saba.

“Utulivu ulidumu kwa ufanisi mkubwa hadi siku za hivi karibuni palipozuka vikundi vichache vikaanza kuchafua amani na kuharibu miundombinu yetu ya uchumi, hapa ningependa kuarifu kuwa SMZ imeshajipanga na itasimamia vyema utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama na kulinda mafanikio yetu haya kwa gharama zozote” Alisema Balozi Seif.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita mchakato wa kujenga uchumi ulitekelezwa katika kwa kuleta umoja, mshikamano na maelewano miongoni mwa wananchi wote na jamii kwa jumla pamoja na kuimarisha elimu
Kuandaa rasilimali watu katika maarifa na muelekeo.

Mambo mengine ambayo aliyataja Balozi Seif, alisema ni kuimarisha mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi, kuimarisha mapinduzi ya viwanda, kuinua mapinduzi ya maarifa, ya sayansi na teknolojia katika uchumi wa wananchi, Upatikanaji wa nishati yenye uhakika na nishati mbadala na Kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.

Balozi Seif, alisema utekelezaji huo ulifanywa katika sura mpya ya Serikali ya Mapinduzi yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa jambo ambalo limeonekana kuzidi kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea 1964.

« Nachukua fursa hii kuwa SMZ ipo na ndio inayo iongoza Zanzibar, isipokuwa mfumo wake ndio uliobadilika na kuwa wa Kitaifa badala ya kuongozwa na Chama kimoja, sio kweli wala si sahihi kuuita Serikali ya Umoja wa Kitaifa tu, bila ya kuihusisha na mzizi wake wa Mapinduzi Matukufu ya Januari, 1964 » alisema Balozi Seif.

Akitoa mfano wa ufanisi huo Balozi Seif alisema ni kukua kwa thamani ya pato la Taifa kwa mwaka 2011, ambao umefikia shilingi bilioni 1,198 ikilinganishwa na thamani ya shilingi bilioni 587.5 ya mwaka 2007.

Ongezeko hili la pato la Taifa Balozi Seif, alisema limesababisha mafanikio katika kasi ya ukuaji wa hali ya uchumi kwa asilimia 6.8 mwaka 2011 ikilinganishwa na 6.5 iliyofikiwa mwaka 2007.

Alisema hali ya ukusanyaji wa mapato nayo imezidi kuimarika kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ambapo Serikali ilipanga kukusanya mapato ya ndani jumla ya Shilingi bilioni 221 ikiwemo bakaa ya shilingi bilioni 4.0 iliyoletwa kutoka mwaka wa fedha 2010/2011 na mapato halisi yaliyopatikana ni shilingi Bilioni 225 sawa na asilimia 102 ya makadirio.

Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi 2011/2012, Balozi Seif, alisema Serikali ya Zanzibar iliendelea kutekeleza Mapango wa Maendeleo katika sekta mbali mbali kwa dhamira ya kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II).

Alisema tathmini ya Hali ya Mahitaji ya Wataalamu nchini nao umekamilika, na Serikali imetayarisha Mpango wa miaka mitano wa Utekelezaji wa MKUZA II, ili uwe muongozo rahisi utakaoiwezesha Serikali na wadau wengine kutekeleza kwa pamoja mikakati, Programu na miradi ya Maendeleo.

Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi wa Oktoba 2010, imeendelea kuwa nzuri na yenye amani na utulivu mkubwa.

Alisema hivi sasa Viongozi na wananchi wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii bila ya kujali tofauti zao za itikadi za siasa kinyume na ilivyokuwa huko nyuma.

Kuhusu jitihada ya kuimarisha Muungano, Balozi Seif alisema mchakato wa Marekebisho ya Katiba, umeanza kwa kuweza kupatikana kwa Katiba mpya, ambapo wananchi wameanza kutoa maoni yao na kazi zake zimekuwa zikifanyika kwa ufanisi na kwa ushiriki mkubwa wa wananchi.

Pia Balozi Seif, alisema katika kipindi cha 2010 – 2012, uchumi wa Zanzibar umeonesha mafanikio makubwa katika ukuaji wake hasa katika maeneo ya uzalishaji, utalii, miundombinu ya kiuchumi na mawasiliano licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za mfumko wa bei uliosababishwa na ongezeko la bei za mafuta na chakula na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania.
Vile vile, Balozi Seif alisema katika kipindi hicho, Serikali ya Zanzibar imeweza kukamilisha mapitio na marekebisho ya Dira ya Zanzibar ya Maendeleo ya 2020.

Alisema Mapitio ya Dira hiyo yamedhihirisha na kumekuwepo na maendeleo katika sekta za jamii hususan elimu na afya pamoja na kupatikana kwa uhuru wa kujieleza, uwajibikaji na utulivu wa kisiasa nchini.

Akizungumzia juu ya mwenendo wa uchumi wa Zanzibar kwa ujumla Balozi Seif alisema ni wa kuridhisha licha ya kuweko kwa changamoto ya kuongezeka kwa mfumko wa bei kwa bidhaa hasa za chakula, ongezeko la bei za mafuta na kukosekana kwa umeme wa uhakika.

Thamani ya Pato la Taifa kwa mwaka 2011 alisema umefikia Shilingi Bilioni 1,198 ikilinganishwa na thamani ya Shilingi Bilioni 587.5 mwaka 2007 ambapo ongezeko hili la Pato la Taifa limesababisha mafanikio katika kasi ya ukuaji wa hali ya uchumi kwa asilimia 6.8 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 6.5 ya mwaka 2007.

Alisema Katika kipindi cha miaka mitano kumekuwa na ongezeko la Pato la Taifa katika kuimarika kwa sekta ya biashara kulikochangiwa zaidi na mazao ya kibishara hasa karafuu na ukuaji wa sekta hii umeongezeka kufikia asilimia 21.9 mwaka 2011, kutoka asilimia 7.5 mwaka 2007.

Kuhusu ongezeko la uwekezaji rasilimali alisema limekuwa kwa asilimia 69.12 kutoka Shilingi 108,321 millioni mwaka 2007 hadi kufikia Shilingi 183,201 milioni mwaka 2011.

Ongezeko hilo alisema limetokana na miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi na za biashara, ujenzi wa barabara na madaraja na uwekezaji katika zana za usafiri.

Aidha alisema vivutio vya utalii anavyo vimeweza kuongezeka kwa shughuli za hoteli na mikahawa kutoka asilimia 4.5 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 10.2 mwaka 2012.

Vile vile, idadi ya watalii alisema imekuwa ikiongezeka kutoka asilimia 4.5 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 31.8 mwaka 2012 na kuimarika kwa shughuli za kilimo kutoka ukuaji wa asilimia 0.4 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 2.7 mwaka 2011, ukuaji huu umetokana zaidi na ukuaji wa sekta ndogo za uvuvi na mazao ya baharini.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Serikali imepanga kukusanya mapato ya ndani yenye jumla ya Shilingi Bilioni 221 ikiwemo bakaa ya Shilingi Bilioni 4.0 iliyoletwa kutoka mwaka wa fedha 2010/2011.

Alisema mapato halisi yaliyopatikana yalifikia Shilingi bilioni 225 ambayo ni sawa na asilimia 102 ya makadirio na katika mapato hayo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilikusanya jumla ya Shilingi Bilioni 128.3 sawa na asilimia 106 ya makadirio ya Shilingi Bilioni 120.6.

Alisema mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) Zanzibar yalifikia Shilingi Bilioni 96.6 sawa na asilimia 96 ya makadirio ya Shilingi Bilioni 100.58. Mapato ya Mawizara yalifikia jumla ya Shilingi Bilioni 119 sawa na asilimia 116 ya makadirio ya Shilingi Bilioni 10.2 na mapato haya yanajumuisha Shilingi Bilioni 7.7 zilizopokelewa kama ni gawio kutoka Benki ya Tanzania.

Akizungumzia kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, Balozi Seif, alisema Serikali hivi sasa imechangia Shilingi Bilioni 34.4 sawa na asilimia 90 ya makadirio ya Shilingi Bilioni 37.9 na jumla ya Shilingi Bilioni 114.6 zilichangiwa na Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya Programu na miradi ya Maendeleo.

Aidha amaeneo mengine ambayo aliyataja kuweza kufanya vizuru ni yale yanayohusu kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuanzisha mashamba darasa na kukipa hadhi Chuo cha Kilimo cha Kizimbani.

Eneo jengine ambalo alilitaja linahusu adhma ya serikali kuanzisha shirika la nyumba ambalo litaongeza upatikanaji wa makazi kwa wananchi.

Kuhusu suala la kukabiliana ana rushwa Balozi Seif alisema tayari limeanza kushughulikiwa kwa serikali kuanzisha Tume ya Rushwa ikiwa ni hatua itayoweza kuondoa tatizo hilo.

Balozi seif alise eneo jengine ambalo limeonekana kuimarika ni katika sekta ya usafirihaji ambapo serikali katika kipindi hiko imeweza kushughulikia kukuza huduma katika bandari kuu ya Zanzibar na Pemba, viwanja vya ndege pamoja na kusimamia ujenzi wa barabara ambazo zimetengwa kujengwa kabla ya 2015.

Kuhusu suala la ufugaji Balozi Seif alisema SMZ kupitia Program ya kuimarisha huduma za mifugo ASDP-L, imetoa taaluma ya ufugaji bora kwa vikundi 155 vipya vya skuli za wafugaji na 180 vya zamani Unguja na Pemba.

Aidha, alisema wafugaji 3,020 wametembelewa na Maofisa mifugo na kupatiwa ushauri wa kitaalam juu ya ufugaji bora.

Akizungumzia sekta ya uvuvi alisema Serikali ya ya Zanzibar ilindelea kutoa kipaumbele kwa sekta hiyo na miongoni mwa hatua hizo ni kuanzisha vikundi vya uzalishaji kwa kutoa mafunzo kwa wavuvi wadogo wadogo na wakulima wa mwani.

Alisema Jumla ya vikundi 20, Kamati 80 na Jumuiya moja ya ukulima wa mwani (JUWAMWAZA) zimeanzishwa na kuendelezwa kwa lengo la kuimarisha Sekta ya Mazao ya Baharini.

Kiuhusu maendeleo ya uhifadhi wa wanyama pori, alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili imefuatilia kwa kina maisha na mwenendo wa wanyama wanaohifadhiwa ambao ni adimu duniani na ni vivutio vya utalii nchini.

Alisema ufuatiliaji huo ambao umefanywa katika misitu ya Jozani, Kiwengwa pamoja na Hifadhi ya Jamii katika ukanda wa Kusini Unguja, una nia ya kujua idadi yao ambapo Wanyama waliopatikana na kuhesabiwa ni Kimapunju 1,700 na Paa Nunga 400 kwa Unguja, na kwa upande wa Pemba, jumla ya Popo 28,778 walihesabiwa.

Vile vile, alisema Serikali imeandaa Mpango wa Usimamizi wa Ukanda wa Pwani pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Rasilimali za Ukanda huo ikiwa ani hatua ya kuimarisha suala la mazingira.

Aidha Balozi Seif alisema uimarishaji huo pia umeonekana kuimarika katika vyombo vya habari pamoja na kuanzisha studio mpya inayotarajiwa kufunguliwa rasmi katika sherehe za Mapinduzi mwakani.

Alisema sekta nyengine ambazo zimeonekana kufanya vizuri ni pamoja na ya Elimu, afya, na sekta ya michezo ambapo utekelezaji wake wa ilani umeonekana kuwa bora.

Nae Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda akitoa muhtasari wa utekelezaji wa Ilani kwa upande wa Tanzania bara, alisema ilani hiyo imeweza kufanikiwa katika maeneo mbali mbali na haitakuwa busara kuanza kuiona sekta binafsi ni sawa na shetani.

Alisema hiyo ni dhana potofu ya kuiona sekta binafsi kuwa ni sawa na shetani kwani inaweza kuwaharibia na ni vyema kuona wanaikubali ili iweze kufanya kazi vizuri.

Akizungumzia juu ya mpango wa Kilimo kwanza Pinda alisema, haina maana ya kushindanisha sekta ila ipo kwa ajili ya kuhimiza uzalishaji wa chakula utaoweza kuwafanya wananchi wa vijijini kujitosheleza kwa chakula.

Alisema hivi sasa wapo katika kutekeleza wazo la kuanzisha benki ya kilimo ambayo inahitaji kuungwa mkono kutokana na mtaji wake kuwa ni mkubwa.

Alisema utekelezaji huo wa ilani unaenda sambamba na kuinua sekta ya afya, elimu, ufigaji, kilimo, uvuvi na utandazaji wa miundo mbinu.

Hata hivyo Pinda aliwaataka viongozi kuona kuwa wanasimamia vyema mipango hiyo kwani haiwezekani kuwa na maendeleo ya kilimo ikiwa viongozi watabaki kuhimiza kilimo kwa maneno badala aya kushiriki kwa vitendo

Aidha, Pinda alisema wakati serikali ikiwa inafanya maendeleo hayo lakini bado kuna haja kuona Chama kinafuatilia shughuli za serikali za mitaa ikiwa ni hatua ya kuweza kutambua utekelezaji wa kazi za chama.

“Lazima Chama hivi sasa kiwe kinaiuliza serikali za mitaa kwani bila ya kuuliza hakuna litaloweza kujulikana nini kinachoendelea” Alisema Pinda.

Kuhusu Muungaano alisema ni lazima itafutwe namna ya kuimarisha Muungano na sio kufikiria kuuvunja jambo ambalo lisilowezekana.

Baadhi ya Mawaziri katika serikali ya Muungano walisema wameweza kufanikiwa katika kuimarisha sekta ya Mawasiliano ambapo Naibu Waziri wa Mawasiliano Chalers Tizeba alisema Wizara inakusidia kujenga bandari 16 katika bandari ya Mtwara.

Alisema ujenzi huo utafanyika kutokana na kuwafanya waingizaaji kuweza kutumia kwa kununulia gesi huku serikali ikifikiria kuijenga bandari ya Tanga pamoja na kuongeza vichwa vya treni.

Upande wa kiwanja cha ndege alisema wamo katika hatua za kujenga majengo ya terminal 3, Uwanja wa Mwalimu Nyerere na uwanja wa Kigoma utajengwa ili kuzifanya ndege za aina zote zinazotua Tanzania zitumie uwanja huo.

Pia Naibu huyo alisema wanakusudia kuimarisha uwanja wa sumbawanga na mwaka wa fedha ujao utaviweka viwanja 20 kuwa na hadhi njia zake na Uwanja wa Songwe ambacho kitaweza kukuza kilimo cha mauwa kwenda Ulaya na pia kutekeleza mradi wa kuziimarisha bandari

Nae Waziri wa Mawasilianao na Teknologia Profesa Mbarawa Mnyaa, alisema ujenzi wa Mkonga wa taifa tayari kilomita 760 zimeshafikiwa ambao utaweza kukuza upelekaji wa huduma za simu vijijini.

Alisema gharama za huduma hivi sasa zimeanza kupungua kutoka shilingi 147 kwa saa mpaka 197 kwa dakika moja hadi kufikia 2001.

Alisema Tanzania inakabiliwa na tatizo la kutokuwa na maeneo ya kupeleka huduma hasa vijijini kutokana na baadhi ya makampuni hayataki kwenda kutia huduma kutokana kuwepo idadi ndogo ya watu ambapo hivi sasa vijiji 3000 havina mawasiliano ya simu.

Alisema tatizo kubwa ambalo wanakabiliana nalo ni la ukosefu wa kuwa na chombo maalum cha kusimamia kodi katika huduma za simu kutokana na hivi sasa baadhi ya makampuni kuonekana kuwa wajanja wa kulipa kodi.

Upande wa Sekta ya Afya Waziri wa Wizara hiyo Dk. Hussen Mwinyi, alisema imekuwa kutokana na kuongezeka kwa vituo vya afya akatika maeneo mbali mbali ya Tanzania ikiwa pamoja na kuongeza idadi ya ajira za madaktari kutokana na kuwa tayari wameshapata kibali kufaya hivyo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawamba, alisema, Vyuo vya walimu vimekuwa kwa kufikia 71 kutoka 55 na hivi sasa serikali imeweka mkazo katika kuimarisha elimu ya ufundi ambapo tayari vyuo vinatarajiwa kuongezeka huku kukiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa kike wanaoingia vyuo vikuu.

Nae Naibu Waziri wa Nishati, Simba Chawene, alisema hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la nishati katika Mji wa Dar es Salaam, huku ikiwa na mpango wa kupeleka umeme vijijini ambapo watahakikisha unakuwa na punguzo ili kuwafanya wananchi kumudu kuunganisha huduma ya umeme ambapo watafikia vijiji 187 na mjini 320 .

Nae Waziri wa Miundo mbinu John Pombe Magufuli akitoa ufafanuzi, alisema sekta hiyo imekuwa kwa kufikia kilomita 22,214 kwa barabara za mikoa na pia hivi karibuni ujenzi wa Daraja la Kikwete litaweza kukamilika pamoja na daraja la Kivukoni na jumla ya barabara zenye thamani ya shilingi bilioni 9.8 zinajengwa katika Mji wa Dar es Salaam na madaraja ya barabara za juu katika eneo la Tazara.

Kazi hizo zimeweza kutoa ajira za watu 650,000 ambapo kumekuwa na vijana Tanzania akuwa ni nchi ya tano inayotumia fedha zaake za ndani kujenga barabara zake.

CCM haina sababu ya kuwa wanyonge kwa vile wanacho ahidi wanakitekeleza na wanaosema ni sawa na tamaa ya fisi mkono wake hauanguki.

Alisema mingi waliyoyafanya bado ni ya msingi na umoja wao ndio uliosaidia kufikia walipo kwani walitumia mtindo wa nguvu ya jeshi wa nyuma ndio wanakuwa na nguvu na haitawasumbua kwani kinachosumbua ni kupigwa na nguvu ya ndani.

Alisema ni lazima kwa wanachama wa CCM kuona wanasema yaliomo ndani ya CCM sio kuacha kuona hakuna kilichofanyika na lazima muendelee kukisemea Chama kwani wanapata nguvu ikiwa hamna wa kukisemea.

Kuacha hali hiyo ndio inayowafanya kuamini uongo unaoelezwa na upinzani kwani kila kinachofanyika kipo katika Wilaya na hakipo katika ngazi ya Taifa na ni vyema muwe na mnasema mnayoyatajua.

Mapema Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Wilson Mukama, alisema Chama cvha Mapinduzi katika kutekeleza majukumu yake kimeweza kufanya mabadiliko mbali mbali ya kukiimarisha chama ikiwa ni hatua itayoweza kukifanya kujiweka vizuri katika uchaguzi Mkuu wa 1015.

Hata hivyo, alisema Chama hicho bado kitaendelea kusimamia suala la rushwa kutokana na katiba yake bado inapinga vitendo vya rushwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.