Na Ramadhani Ali/Habari Maelezo Zanzibar 13/11/2012
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Joseph Meza ameeleza kuwa Zanzibar itajifunza kwa kiasi kikubwa kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 34 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Nchi za Afrika wa Usimamizi wa Huduma za Umma na Utawala bora (AAPAM) unaoendelea katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Amesema Mkutano huo unaowakutanisha wataalamu zaidi ya 500 wanaosimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawla Bora kutoka mataifa ya Áfrika, utawasadia sana viongozi wanaosimamia sekta hiyo hapa Zanzíbar.
Meza amesema viongozi wanaoshiriki mkutano huo wa situ tano, unaofanyika kwa mara ya kwanza hapa Zanzíbar, wameonyesha wazi kuwa nchi zao zimepiga hatua kubwa katika kusimamia huduma za utumishi wa umma na utawala bora, na imekuwa ni fursa nzuri kwa washiriki wa Zanzíbar kujifunza kutoka kwao na kuleta mabadiliko ndani ya taasisi za hapa nchini.
Pia amesema Mkutano huo utaisaidia Zanzíbar kutangaza vivutio vyake vya utalii kwa vile wajumbe hao watapata fursa ya kutembelea sehemu za mijini na mashamba na amewataka wananchi kuonyesha ukarimu wao kwa wageni hao watakapo watembelea ili kupata picha halisi ya nchi.
Akiwasilisha mada ya utendaji bora katika kuimarisha huduma za jamii zinazotolewa katika nchi za África, Makamu wa Rais wa AAPAM Afrika ya Kati Dk. Finlay Sama Doh amesema suala la kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wafanyakazi, kuwapa motisha na kuimarisha vitendea kazi ni mambo yanayosaidia kwa kiasi kikubwa ufanisi katika sekta za utumishi wa umma katika nchi.
Ameongeza kuwa suala la kuwajengea utamaduni wafanyakazi kuheshimu sheria za kazi na kuwapa fursa ya kujieleza wanapofikwa na matatizo ya kazi na kuyatafutia ufumbuzi ni miongoni mwa vichocheo vya kuimarisha utawala bora na utendaji mzuri wa kazi.
Ametoa wito kwa viongozi wa Áfrika wanaosimamia masuala ya utumishi wa umma na utawala bora wanaoshiriki mkutano huo kuweka mpango endelevu wa kufanya tathmini ya utendaji na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta hiyo katika nchi zao.
Mkutano huo unatarajiwa kumalizika Ijumaa ijayo na kabla ya kufungwa rasmi, viongozi wakuu wa AAPAM watatangaza nchi mwenyeji wa mkutano ujao wa 35 wa Jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment