Habari za Punde

Jamhuri uso kwa uso na St. George Afrika

CAIRO, Misri
 
WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) timu ya Jamhuri kutoka Pemba, itaanza resi hizo kwa kuivaa klabu ya St. George ya Ethiopia.
 
Jamhuri itakuwa wenyeji wa mchezo wa kwanza, kabla kurejeana na Wahabeshi hao mjini Adis Ababa wiki mbili baada ya mechi ya awali.
 
Ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Cairo mwishoni mwa wiki, inaonesha kuwa, timu itakayofuzu baada ya mechi mbili hizo, itakwaana na mabingwa wa Mali, klabu ya Djoliba.


Jamhuri ambao ni makamu bingwa wa Zanzibar msimu wa 2012, walistahiki kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho, lakini wamechukua nafasi ya mabingwa Super Falcon, ambayo imeshindwa kushiriki mwaka huu kutokana na ukosefu wa fedha.
 
Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kimeamua kuipa Jamhuri kofia hiyo baada ya kutojitokeza kwa timu nyengine kuchukua nafasi ya Super Falcon.
 
Katika ngarambe hizo, wawakilishi wa Tanzania Simba, wamepangwa kuanza na mabingwa wa Angola, klabu ya Recreativo do Libolo, ambapo mchezo wa kwanza utafanyika nchini Tanzania na ule wa marudiano, kuchezwa mjini Luanda.
 
Iwapo Simba itavuka kikwazo hicho,itapambana na El Merreikh ya Sudan, ambayo iko mbioni kumnunua mshambuliaji wa wekundu hao Mrisho Ngassa, ambaye alipelekwa Simba kwa mkopo na Azam FC.
 
Nayo Azam itaanzia nyumbani Dar es Salaam kujaribu bahati yake kushinda Kombe la Shirikisho, michuano ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza, dhidi ya Juba Al Nasir ya Sudan Kusini.
 
Kama itafanikiwa kuvuka, Azam itakabiliaana na mshindi kati ya Johansens ya Sierra Leone na Barrack Y. C. II ya Liberia.
 
Mechi za kwanza zinatarajiwa kuchezwa kati ya Februari 15, 16 na 17, mwakani, na zile za marudiano, kufanyika baina ya Maci 1, 2 na 3

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.