Habari za Punde

Simba, Azam kimeeleweka lakini… kumuuza Ngassa

 
  DAR ES SALAAM
 
HATIMAYE Simba na Azam FC zimefikia makubaliano ya kumuuza kwa pamoja mshambuliaji Mrisho Ngassa kwenda El Merreikh ya Sudan, lakini mchezaji huyo amekuwa hapatikani kwenye simu ili kuhusishwa kwenye mpango huo.
 
Habari za uhakika zilizopatikana na gazeti hili kutoka kwenye kikao cha pamoja kati ya Simba na Azam jana, zimesema Merreikh imeongeza dau la kumnunua Ngassa kutoka dola za Kimarekani 70,000 hadi laki moja, ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 150 za Tanzania.


Baada ya kuongeza dau hilo, Azam ilikutana na Simba kujadili pamoja ofa hiyo mpya na kukubaliana kumuuza na kugawana nusu kwa nusu.
 
Upande wa Azam uliwakilishwa na mmoja wa Wakurugenzi wa bodi ya klabu hiyo, wakati kwa Simba waliwakilishwa na Makamu wao Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
 
Katika kumuuza Ngassa, maslahi yake yameimarishwa pia, ambapo sasa atapewa dola za Kimarekani 75,000 zaidi ya shilingi milioni 110,000 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na mshahara utabaki kuwa dola 4,000 (TSh milioni 6).
 
Habari zinasema kwamba, baada ya makubaliano hayo, leo Simba na Azam watasaini mkataba na Azam na kumuuza rasmi mchezaji huyo.
 
Hata hivyo, tangu wakati kikao hicho kinaendelea jioni ya leo, Ngassa alikuwa akitafutwa ili kuhusishwa, lakini hakupatikana kwenye simu.
 
Wasiwasi umeibuka kwamba huenda Ngassa anaweza akawa ameghairi mpango wa kwenda Merreikh kutokana na ushauri mbaya wa watu wake wa karibu.
 
Mchezaji mmoja wa timu ya taifa, amefichua kuwa Ngassa anafikiria kuachana na mpango wa kucheza Sudan, kwa sababu anasikia ni nchi ya Kiislamu na haina starehe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.