Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sherehe na Mapambo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikiongoza Kikao cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa.
Kikao hicho kilichofanyika katika Jumba la Wananchi Forodhani kilikuwa kikipitia na kukamilisha ratiba ya maadhimisho ya sherehe ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar
Na Othman Khamis Ame
Jumla ya Miradi 54 ya Maendeleo, Uchumi na ile ya Kijamii inatarajiwa kuzinduliwa na mengine kuwekewa Mawe ya Msingi ndani ya wiki ya Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 49.
Maadhimisho ya sherehe hizo zitakazofikia kilele chake Januari 12 mwakani zinatarajiwa kuzinduliwa tarehe 4 Januari mwakani kwa kazi za usafi wa mazingira katika Wilaya zote za Zanzibar.
Kikao cha Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho kilikutana kwenye Ukumbi wa Jumba la Wananchi Forodhani chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika kufikia hatua za mwisho za kukamilisha ratiba ya maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nusu ya miradi yote itakayozinduliwa au kuwekwa mawe ya msingi inayokadiriwa kufikia zaidi ya asilimia 49% inatokana na sekta ya Elimu ikiwalenga zaidi wananachi waliowengi katika maeneo wanayoishi.
Kaimu Katibu wa Kamati ya Taifa ya Sherehe na Mapambo ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Said Shaaban alisema sekretarieti ya kamati hiyo imekamilisha mapitio kutokana na marekebisho yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo.
Nd. Said Shaaban alisema marekebisho hayo yalikwenda sambamba na mapitio ya bajeti na maependekezo ya sherehe hizo kuzingatia maagizo ya wajumbe wa Kamati ya Taifa ya sherehe na mapambo.
Akitoa nasaha zake Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sherehe na Mapambo Balozi Seif Ali Iddi alielezea matumaini yake kwamba maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar mwakani zinatarajiwa kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Balozi Seif aliomba kuendelezwa kwa ushirikiano zaidi kupitia Kamati zinazohusika pamoja na kushauri kuendelea kupokelewa kwa mawazo kutoka kwa wajumbe mbali mbali katika dhana nzima ya kufanikisha sherehe hizo.


Watu wana njaa nyie mko mapinduzi mapinduzu.Ujuwe halo balozi mtanganyika keshachukuwa % yake mfukoni hana wasi wasi.
ReplyDelete